Tuesday, June 6, 2023

PICHA: Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM-Mawenzi, Moshi

 

Shule ya Msingi Mawenzi ikiwa katika maboresho baada ya kutengewa kiasi cha Shilingi Mil. 60 ambazo zitatumika kukarabati vyumba sita vya madarasa. Hata hivyo katika ziara hiyo iliyoongozwa na Diwani wa Kata ya Mawenzi Apaikunda Naburi waliukataa mradi huo.











Wajumbe wa Kamati ya Siasa Kata ya Mawenzi Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamesema hawajaridhishwa na vifaa vilivyo nunuliwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye vyumba vya madarasa shule ya msingi Mawenzi, kutokana na vifaa hivyo kuwa chini ya viwango.

Aidha Wajumbe hao wamesema endapo vifaa hivyo vitawekwa bila kubadilishwa hawatakuwa tayari kuupokea mradi huo na kumwagiza Mkuu wa shule ya Msingi Mawenzi pamoja na Mhandisi wa ujenzi, kuhakikisha vifaa hivyo vinabadilisha na kuletwa vipya ili viendane na thamani ya fedha.

Akizungumza katika eneo la tukio Diwani wa Kata ya Mawenzi Apaikunda Naburi, ameonesha kusikitishwa na madirisha yaliyonunuliwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye vyumba vya madarasa sita yanayokarabatiwa katika shule ya Msingi Mawenzi kwani hayaendani na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na seriakli kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.

Apaikunda Naburi alisema, serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba sita vya madarasa shule ya msingi Mawenzi na  kwamba katika ukaguzi walioufanya wamebaini kukuta madirisha ambayo yamenunuliwa yakiwa chini ya viwango.

Naburi alisema katika ziara hiyo pia Wajumbe hao walitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa shule ya msingi Uhuru, ujenzi wa ofisi ya Kata na ukarabati wa   kituo cha walimu Mawenzi (TRC), na kuridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata ya Mawenzi Thomas Temu, alisema Kamati haijaridhishwa na ubora wa madirisha yaliyotengenezwa kwani hayalingani na thamani ya fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kumshauri mhandisi wa ujenzi pamoja na mwalimu mkuu wa shule hiyo, kuyaondoa, ili yaweze kutengenezwa madirisha mengine ambayo yataendana na thamani ya fedha ambazo zimetolewa na serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mawenzi Mujibu Abeid, alisema ziara hiyo ilikuwa imelenga kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata hiyo.

Aidha alisema wajumbe wa kamati hiyo, walitembelea miradi mitatu ukiwemo, mradi wa ukarabati wa shule ya msingi Mawenzi na kubaini kasoro hizo na kwamba wajumbe wameyatolea maelekezo ya changamoto  zilizojitokeza.
Akizungumza Ofisa Elimu Kata ya Mawenzi Herry Christopher alisema Kata ya Mawenzi imepokea takribani shilingi milioni 200 ambapo fedha hizo zinakwenda kujenga na kukarabati miundombinu kwenye sekta ya elimu ndani ya kata hiyo.

"Tunaipongeza serikali kwa kutoa fedha hizi ambazo zinakwenda kutatua changamoto ya mlundikano wa wanafunzi madarasani kwenye shule jambo ambalo lilikuwa linasababisha walimu kushindwa kuwafundisha wanafunzi vizuri na kuweza kumuelewa,"alisema.

0 Comments:

Post a Comment