Nyumba ya urithi ya Familia ya Jubilathe Macha, waliyokuwa wanaishi Gervas na Grace kabla ya Mchungaji Heriel Herimoyo Mawose kujitolea kuwajengea nyumba bora ya kisasa. |
Kuzaliwa katika Familia duni haina maana kuwa umepoteza sifa ya kufanikiwa katika maisha yako ndivyo unavyoweza kusema katika makala haya.
Aidha ni mara chache unaweza kusikia viongozi wa kidini
wakijitosa katika kusaidia familia zilizopo katika mazingira magumu hususani
ambazo zipo nje ya ushirika wa dini husika.
Pia yeyote anaweza kuweka nadhiri anavyopenda, lakini kuna
nadhiri zilizoratibiwa na sheria, hasa sheria za Kanisa, kama zile za kitawa na
kadhalika.
Swali moja linaweza kusalia katika ubongo wa kila mmoja wetu
ni kwa namna gani Mchungaji alivyojitosa kusaidia familia ya ndugu wawili
waliokuwa wakiisha katika nyumba mbovu ya urithi hadi nadhiri ilipotimizwa ya
kujengewa nyumba bora ya kisasa pamoja na choo na bafu?
Ilikuwa hivi!; Mchungaji Heriel Herimoyo Mawose anaishi
katika kijiji cha Shia, Kimocho kilichopo Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro
ambako familia hiyo duni nayo ipo huko.
Kama ujuavyo maeneo ya Moshi Vijijini baadhi yake ni ya
milima na mabonde ambako ukitaka kwenda hata nyumbani kwako unaweza kupita
katika eneo la mtu mwingine kisha kwenda uendako.
Changamoto iliyokuwapo kwa Mchungaji huyo ilikuwa ni
barabara ya kwenda nyumbani kwake katika kitongoji cha Manyeri ‘C’ ambapo gari
lake lilikuwa halilali nyumbani kwake isipokuwa kwa majirani.
Majirani wa karibu na Mchungaji huyo ambao walizoea kuwa
walinzi wa gari hilo ni familia ya Jubilathe Macha ambayo kwa sasa wamesalia
kaka na dada wanaoishi katika nyumba ya urithi waliyoachiwa na wazazi wao.
Mchungaji Heriel anasema mara ya kwanza aliwaomba familia
hiyo kulaza gari lake, hatimaye akazoea kulilaza hapo.
Hata hivyo liligeuka kero kwani familia ya Macha ilikosa
uvumilivu na kuamua kumweka wazi kuwa kutokana na changamoto walizonazo za
kifamilia gari hilo limekuwa likiwakosesha usingizi.
Aidha familia hiyo ambayo dada mtu anayefahamika kwa jina la
Grace ni mgonjwa wa kifafa na kaka mtu (Gervas) amekuwa akisumbuliwa na maradhi
ya kifua ilimweleza Mchungaji huyo na kwamba gari lake linaweza kuwazidishia
matatizo zaidi kwani wanaweza wezi wakaiba matairi au vifaa vingine katika gari
hilo au maisha yao kuwa mashakani zaidi.
Hata hivyo Gervas na Grace wakaamua kwa moyo wao kukata
kipande cha ardhi yao kuwa barabara ili mchungaji huyo aweze kupitisha gari
lake badala ya kulilaza nyumbani hapo.
Jambo la kutoa kipande cha ardhi bure katika ardhi ya Uchagani
ni jambo gumu kuliko kitu chochote lakini familia ya Jubilathe Macha imeonyesha
mfano wa kiutu.
Mchungaji Heriel anasema kitendo hicho kilimfanya amlilie
Mungu wake kwani ni jambo ambalo hakulitarajia katika maisha yake kutokana na
tabia za Uchagani zilivyo.
Pia Mchungaji huyo aliamua kujiwekea nadhiri ya kwamba
ataitunza familia hiyo kwa namna ya kipekee ambayo Mwenyezi Mungu atampa.
“Tuliwauliza majirani hawa (Gervas na Grace) kama tungeweza
kutoa chochote kwao kama shukrani , nakumbuka vizuri Gervas alisema tukiugua si
litatupeleka hospitali? Kwa kauli hiyo ya kiungwana mjadala wa malipo ama fidia
ukawa umefungwa hata hivyo dhamiri zetu ziliendelea kuwaka ndani ya mioyo yetu
kuwa tutaweza kufanya nini kuweza kutimiza nadhiri yetu,” anasema Mchungaji
Heriel.
Hata hivyo kabla hajaanza kufanya kile alichokusudia moyo
mwake, usiku mmoja Oktoba 2022 Grace alitoka kwenda kujisaidia ghafla choo
kilididimia na almanusura azame moja kwa moja kutokana na miti ya kuoza.
Grace alipiga kelele za kuomba msaada ndipo Gervas na
majirani wengine walipojitokeza na kumtoa katikati ya shimo la choo akining’inia
huko machozi tele yakimtoka.
“Baada ya zoezi la uokozi kutoka chooni tulikaa na kuwaza na
kusukumwa kuwa sasa ndio wakati wa Bwaka umefika ili tuweze kutimiza nadhiri
yetu,” anasema Mchungaji Heriel.
Unaweza kusema kilichokuwepo moyoni mwa Grace ni kuwa
amezaliwa kwa ajili ya taabu na shida, majanga mbalimbali au?
Mchungaji Heriel aliguswa moja kwa moja kuwajengea choo
hicho na bafu.
Haikutosha kadri siku zilivyozidi kwenda Mchungaji Heriel
amewajengea nyumba ya kisasa familia hiyo ambapo kwa sasa unaweza kusema shida
za mahali pa kulala zimekwisha.
“Kazi mnayoiona hapa leo ni sehemu ya nadhiri yangu na
familia yangu, maombi yetu yalikuwa ni kwamba Bwana Mungu atupe uwezo na
atuoneshe mahali sahihi pa kutumika,” anaongeza Mchungaji Heriel.
Kutoka nyumba ya urithi ya tope na paa lililochoka hadi paa bora la kisasa
maarufu kwa jina la ‘Msauzi’ Gervas na Grace wanasema.
Mnamo tarehe 16 Mei 2023 Mchungaji Heriel alifanya ibada ya
kuwakabidhi nyumba, choo na bafu familia ya Macha huku ibada ikisimamiwa na
Mchungaji Godlizen Shao wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika
wa Shia.
“Kuna kila sababu ya kumshirikisha Mungu kwa kila jambo
unalolifanya katika hatua zetu zote za maisha yetu. Mungu ndiye mlinzi wa
maisha yetu ya kila siku, ukimshirikisha Mungu , Mungu hataachi kutembea nawe
wakati wote,” anasema Mchungaji Shao.
Aidha Mchungaji Mstaafu Sifuel Macha wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT)Usharika wa Shia; anaongeza, “Kama Jumuiya baada ya
kuiona changamoto hii, tulikuwa tumepanga kuanza kuisaidia familia hii, na kwa
bahati nzuri alitokea mfadhili aliyeguswa na jambo hilo na kuweza kuwasaidia.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Shia Elisante
Philipo Marima anasema; “Familia hii
waliachwa na wazazi wao wakiwa wadogo, wamepitia katika changamoto nyingi, walikuwa
kwenye maisha duni ambayo walikuwa
wakiyaishi yeye na dada yake. Kwa niaba ya uongozi wa serikali ya kijiji
tunamshukuru sana mfadhili huyo kwa kuweza kuwajengea makazi bora familia hii,”
anasema Marima.
Tukio hilo halitakaa lifutike katika vichwa na mioyo ya
Gervas na Grace pamoja na majirani wa Manyeri ‘C’ licha ya kupewa nyumba ya
kulala ndani yake wamechongewa samani zinazoifanya nyumba hiyo ipendeze ikiwamo
vitanda na meza pia magodoro na mapazia.
“Sisi kama ukoo wa Macha Makipure Kero, hatungeweza lakini
kwa kupitia mfadhili huyo ameweza kuwa mwaminifu kwa Mungu kupitia nyumba hii,”
anasema Katibu wa Ukoo, Elingaya Macha.
Baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo Grace anasema, “Namshukuru
mfadhili huyo kwa kutujengea nyumba namshukuru sanasana; peke yetu tusingeweza
kutokana na changamoto tunazozipitia hususani wakati wa mvua.
Grace Jubilathe Macha |
0 Comments:
Post a Comment