Thursday, May 4, 2023

Pongezi zatolewa ujenzi geti jipya la Ndea kuingia Hifadhi ya Taifa Mkomazi

Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwanga kutoka wilaya na kata katika picha ya pamoja wakiwa na Mbunge wa Mwanga Joseph Tadayo walipozuru geti jipya la kuingia Hifadhi ya Mkomazi. Geti jipya la Ndea, kata ya Toroha litarahisisha watalii kuingia katika hifadhi hiyo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo watalii walikuwa walazimika kupitia wilaya ya Same. 


MBUNGE wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, ameishukuru  Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia kutoa fedha zilizowezesha kujenga lango jipya la kuingia Wageni katika Hifadhi ya Taifa ya Mkoamazi kupitia kijiji cha Ndea kata ya Toroha Wilayani humo. 

Tadayo ameyasema hayo jana, wakati wa ziara yake ya kutembelea na kuangalia ujenzi wa lango lililojengwa eneo la Ndea ambalo liko ndani ya kata ya Toroha Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

 

"Tunamshukuru sana Rais Samia  kwa kusikia ombi letu la muda mrefu la kutujengea lango hili, ambalo litawezesha watalii wanaotaka kutembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi  waweze kufupisha safari yao kwa kutumia lango hili, tofauti na huko nyuma watalii walikuwa wakilazimika hadi Wilaya ya Same ndipo uweze kuingia hifadhi ya Mkomazi,"alisema Tadayo. 

 

Mbunge Tadayo alisema “Wilaya ya Mwanga, kama zilivyo wilaya zingine zinazopakana na hifadha,  ilikuwa hainufaiki na mapato yatokanayo na hifadhi ya Mkoamazi, kutokana na watalii wengi walikuwa wakipita wilaya ya Mwanga na kwenda wilaya jirani ya Same, licha ya kwamba inapakana kabisha na hifadhi ya Mkomazi.

 

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamishna msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi wa Taifa ya Mkomazi Emmanuel Moirana alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kuwapelekea fedha za Uviko ambazo ziliwezesha kujenga lango maalumu eneo la Ndea ambalo ni la kuingilia wageni wanaofika kutembelea hifadhi hiyo na kuweza kupata huduma nzuri za utalii.

 

Alisema kwamba kupitia fedha hizo wameweza kujenga barabara yenye urefu wa  kilomita 140, ujenzi  wa kiwanja kipya cha ndege na ukarabatiwa viwanja vya ndege cha zamani hali ambayo imewezesha wageni  wengi kuitembelea hifadhi hiyo.

 

"Kujengwa kwa uwanja mpya wa ndege ndani ya hifadhi ya Mkomazi, pamoja na kuukarabati uwanja wa ndege wa zamani, kumesaidia wageni wengi kusafiri kutumia ndege kufika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi moja kwa moja kutoka kwenye viwanja vyengine,"alisema Moirana.

 

Naye Diwani Kata ya Toroha Palesio Makange, alisema, kujengwa kwa lango hilo kutakwenda kutoa fursa za kiuchumi kwa wakazi maeneo hayo ambapo watawauzia watalii vitu mbalimbali vya asili, pamoja na  kupunguza kero ya tembo ambao walikuwa wakitoka ndani ya hifadhi hiyo na kuja kwenye makazi ya wananchi.

 

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi Tanapa Herman Batiho, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, kwa kuweka hamasa ya kufungua lango hilo ambalo litakuwa na sehemu ya kupokea watalii wanaoingia na kutoka, maegesho ya magari pamoja na vyoo vya kisasa.

 

"Hifadhi ya Taifa Mkomazi ilikuwa na lango moja tu la kuingia na kutoka, serikali ikaona kuna fursa za kuweza kufungua malango mengine zaidi, moja ya lango linalokwenda kufunguliwa ndani ya Mkomazi  ni pamoja na lango lililojengwa eneo la Ndea lililoko wilaya ya Mwanga na lango la Kamakota Wilaya ya Mkonga mkoani Tanga,".

0 Comments:

Post a Comment