Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, December 31, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Mfalme Salman wa Saudia Arabia ni nani?



Desemba 31, 1935 alizaliwa mfalme wa Saudia Arabia na Waziri Mkuu wa taifa hilo la barani Asia Salman bin Abdulaziz Al Saud. 

Pia Mfalme Salman amekuwa mhudumu mkuu wa misikiti miwili mikubwa ule wa Mecca na Madinna tangu Januari 23, 2015. 

Mfalme Salman aliwahi kuwa Naibu Gavana wa Riyadh na baadaye Gavana wa Riyadh kwa miaka 48 tangu mwaka 1963 hadi mwaka 2011. 

Mfalme Salman aliwahi kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo la Kiislamu. Mnamo mwaka 2012 alitangazwa kuwa mrithi wa ufalme huo baada ya kifo cha kaka yake Nayef bin Abdulaziz. 

Salman alikuja kuwa Mfalme mpya wa Saudia Januari 23, 2015 baada ya kifo cha kaka yake Mfame Abdullah. Tangu mwaka 2019 Mfalme Salman ndiye mtoto pekee wa Ibn Saud aliye hai. 

Katika masuala ya kusimamia taifa hilo Mfalme Salman aliingia kati mzozo wa kivita wa Yemen na kutangaza kumtambua Abdrabbuh Mansur Hadi mwenye asili ya Saudia Arabia kuwa  kiongozi mkuu wa Yemen. 
Pia Mfalme Salman tangu aliposhika madaraka hayo anasimamia maono ya ifikipo 2030 taifa hilo lisiwe tegemezi katika biashara yake ya mafuta kuboresha sekta ya afya, elimu, miundombinu na utalii. 

Mnamo mwaka 2017 Mfalme Salman atakumbukwa kwa kuwaruhusu wanawake kuendesha magari kwani hapo awali kwa miaka mingi wanawake hawakuwa na uhuru wa kuendesha vyombo vya usafiri. 

Pia mwaka huo huo Mfalme Salman aliingia katika mkanganyiko kufuatia mauaji ya mwanahabari Jamal Kashoggi ambayo yanadaiwa kufanywa na familia hiyo ya Kifalme ya Saudi Arabia. 

Pia Mfalme Salman aliingia katika sintofahamu nyingine baada ya kuwakamata wanafamilia wa Kifalme, mawaziri wake, wafanyabiashara ikiwa ni majuma machache baada ya kuundwa kwa tume ya Mapambano dhidi ya Rushwa iliyoongozwa na Crown Prince Mohammad bin Salman maarufu MbS. 

Mfalme Salman anatajwa kuwa ni mtoto wa 25 wa Abdulaziz ibn Abdul Rahman ibn Faisal ibn Turki ibn Abdullah ibn Muhammad Al Saud kwa watu wa magharibi hufupisha Ibn Saud, ambaye ndiye mwasisi wa taifa hilo la Kiislamu. 

Salman alikulia katika jumba la kifalme la Murraba ambalo kwa sasa ni makumbusho  katika viunga vya Riyadh. Salman alisoma elimu ya awali katika shule ya Watoto wa Kifame ya Prince’s iliyopo katika mji mkuu wa Saudia Arabia Riyadh. 

Ibn Saud alianzisha shule hiyo kwa ajili ya watoto wake ili waweze kupata elimu. Salman alisoma elimu ya dini na Sayansi ya Kisasa.

Januari 23, 2015 Salman akiwa na umri wa miaka 79 alirithi kiti cha ufalme baada ya kifo cha kaka yake Abdullah ambaye alifariki dunia kwa ugonjwa pneumonia au kichomi akiwa na umri wa miaka 90.  

Alipoingia madarakani alifanya mabadiliko kadhaa ya utawala wake ambapo Khalid bin Ali bin Abdullah al-Humaidan alimfanya kuwa mkuu wa usalama wa taifa. 

Prince Bandar bin Sultan aliondolewa katika idara hiyo ya ulinzi. Baadaye katika utawala wake aliingia katika kashfa ya nyaraka za siri kuvuja kwa kile kilichofahamika kama Panama Papers ambapo ndani yake kulikuwa na makampuni makubwa mawili kutoka Britisha Virgin Islands pia Crown Prince Muhammad bin Nayef alitajwa katika kashfa hiyo. Salman ameoa mara tatu katika maisha yake. 

Hadi mwaka 2017 alikuwa na watoto 13 mkewe wa kwanza Sultana bint Turki Al Sudairi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 71 mapema Julai 2011, baadaye alimuoa Sarah binti Faisal Al Subai’ai ambaye waliachana na kwa sasa anaye Fahda bint Falah Al Hathleen. 

Mtoto wake wa kwanza Fahd bin Salman alifariki dunia akiwa na miaka 47mnamo Julai 2001 kwa ugonjwa wa moyo. Pia mtoto wake wa tatu wa kiume Ahmad naye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 43 mnamo Julai 2002 kwa ugonjwa wa moyo. 

Salman ndiye mwarabu wa kwanza na muislamu wa kwanza kusafiri katika anga za juu  akifanya hivyo kwa kutumia kifaa STS-51-G mnamo Juni 1985.

Saturday, December 28, 2019

Asili ya Afro-Cuban Jazz


Muziki wa Afro-Cuban Jazz ni miongoni mwa mazao ya muziki wa Cuba na pia ni miongoni mwa muziki wa mwanzoni kabisa katika Latin Jazz. 

Tunapozungumza kuhusu Muziki wa Cuba tunaingiza vyombo vya muziki wenyewe na muundo wa uchezaji wake ukitumia vifaa vya kipekee vya asili ya watu wa Cuba. 

Ikumbukwe kwamba muziki wa Cuba umekua kutokana na ujio wa watu kutoka Afrika Magharibi na barani Ulaya hususani Hispania. 

Afro-Cuban Jazz ilianza mwanzoni mwa miaka 1940 wakati ambao Charanga ilikuwa maarufu katika ardhi ya Cuba. 

Wanamuziki wa Cuba Mario Bauza (Aprili 28, 1911-Julai 11,1993) na Frank Grillo ‘Machito’ (Februar 16, 1908 – Aprili 19, 1984) ndio waanzilishi wakuu wa Afro-Cuban Jazz. Wasanii hawa waliupeleka muziki huo jijini New York ukiwa na vionjo vya mila na desturi za watu wa Cuba. 

Mnamo mwaka 1947  walikutana na wasanii wengine ambao walikuwa mahiri katika kutumia vyombo akiwa mpiga tarumbeta Dizz Gillespie na mpiga percussion Chano Pozo. 

Dizz na Chano waliongeza vyombo vingine Tumbadora na Bongo katika Afro-Cuban Jazz iliyokuwa imejikita katika Pwani ya Mashariki ya Marekani. 

Bauza aliuwa mpiga wa Saxofoni, clarinet, tarumbeta pia mtunzi na mwimbaji wa muziki wa Afro-Cuban Jazz. Katika miongo ya mwanzoni Afro-Cuban Jazz ilikuwa na nguvu sana nchini Marekani kuliko hata Cuba kwenyewe. 

Mwanzoni mwa miaka ya 1970 Kenny Dorham akiwa na Orquesta Cubana de Musica Moderna na baadaye Irakere walirudisha muziki huo katika ardhi ya Cuba. 

Joe Henderson alikusanya kazi za Kenny Dorham na kuziweka pamoja mnamo mwaka 1963 ambapo mkusanyiko huo wa pamoja aliuita Blue Bossa kwenye albamu ya Page One. Dorham aliurudisha Cuba ukiwa na staili (muundo) uliowavutia wengi wa Songo. 

Dorham alizaliwa Agosti 30, 1924 Fairfield katika kaunti ya Freestone jimboni Texas nchini Marekani na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 48, mnamo Desemba 5, 1972 jijini New York. 

Dorham alifanikiwa licha ya kutopewa nafasi ya kutambulika sana lakini alionyesha uwezo wake wa Afro-Cuban Jazz ya kutumia vifaa pekee yake (instrumental).

Imetayarishwa na Jabir Johnson.......Desemba 28, 2019.
Mario Bauza (1911-1993)
Frank Grillo 'Machito' (1908-1984)
Kenny Dorham (1924-1972)





Wednesday, December 25, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Muhammad Jinnah ni nani?


Desemba 25, 1876 alizaliwa mwanasheria, mwanasiasa na mwasisi wa taifa la Pakistan Muhammad Ali Jinnah maarufu Qaid-i-Azam ikiwa na maana Kiongozi Mkubwa. 

Ali Jinnah alizaliwa Karachi, wakati huo ikiwa India kwa sasa ni Pakistan na Kufariki dunia Septemba 11, 1948. 

Alikuwa mwanasiasa wa Kiislamu, mwasisi na gavana –jenerali wa kwanza wa Pakistan. 

Jinnah alikuwa mtoto wa kwanza kati ya saba wa mzee Jinnahbhai Poonja ambaye alikuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na mkewe Mithibai. 

Familia hiyo ilikuwa miongoni mwa wanachama wa ngome ya Khoja ambao ni Wahindu walioachana na imani hiyo na kujiunga na Uislam kwa karne nyingi zilizopita na pia Familia hiyo ilikuwa ni wafuasi wa Aga Khan. 

Tarehe rasmi ya kuzaliwa kwake inachanganya kwani rekodi za shule zinaonyesha alizaliwa Oktoba 25, 1875 lakini  Jinnah mwenyewe aliwahi kusema kuwa alizaliwa Desemba 25, 1876. 

Baada ya kupata mafunzo ya shule akiwa nyumbani mnamo mwaka 1887 Jinnah alipelekwa katika shule moja maarufu mjini Karachi ya Sind Madrasat al-Islam ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu kinachofahamika kwa jina la Sindh Madressatul Islam.  

Baada ya hapo Jinnah alikwenda kwenye shule ya Kikristo ya CMS. Akiwa hapo alifanikiwa kufanya mtihani uliompa kwenda Chuo Kikuu cha Bombay ambacho kwa sasa ni Mumbai nchini India. 

Kutokana na ushauri aliopewa na rafiki yake ambaye alikuwa Mwingereza, Baba yake mzee Poonja aliamua kumpeleka mtoto wake nchini England ili kupata uzoefu wa kibiashara. 

Lakini kabla hajaondoka wazazi wake walifanya mipango ya haraka ili aweze kuoa. 

Alitua London na kujiunga na Lincoln Inn ikiwa ni miongoni mwa taasisi ya kisheria ambayo ilikuwa ikiwaandaa wanafunzi kuwa wanasheria. Mnamo mwaka 1895 akiwa na umri wa miaka 19 alikuwa rasmi miongoni mwa waliokuwa vizuri katika taasisi hiyo. 

Akiwa bado jijini London Jinnah alipatwa na mfadhaiko baada ya kufiwa na mke wake na mama yake. 

Hata hivyo alifanikiwa kumaliza masomo yake ambayo alikuwa akisomea muundo wa Kisiasa wa Uingereza na mara kadhaa alikuwa akizuru katika baraza la wawakilishi au bunge dogo la Uingereza. 

Alivutiwa zaidi na falsafa ya Uliberali ya William E. Gladstone ambaye alikuja kuwa waziri mkuu wa nne wa Uingereza mnamo mwaka 1892 mwaka ambao Jinnah alikuwa akiwasili London. 

Hata hivyo Jinnah aliendelea kufuatilia kwa karibu maisha na masuala kadhaa ya Wahindi na wanafunzi wa Kihindi. 

Wakati kiongozi na mwanamapinduzi wa India Dadabhai Naoroji alipokuwa katika Bunge la Uingereza; Jinnah na wanafunzi wenzake wa Kihindi walikuwa wakifanya kazi usiku na mchana kwa ajili yake na matokeo yake alifanikiwa. 

Naoroji aliweka rekodi ya kuwa mhindi wa kwanza kukalia kiti katika bunge dogo la Uingereza. 

Mnamo mwaka 1896 Jinnah alirudi zake Karachi na kukuta biashara za baba yake zikiwa katika hali mbaya na hivyo kuanza kujitegemea. Jinnah aliamua kwenda zake Mumbai kwa ajili ya shughuli za kisheria ambako ilimchukua miaka mingi kuweka misingi ya kuwa mwanasheria imara. 

Takribani kwa miaka 10 baadaye Jinnah alikuwa amejiingiza vizuri katika masuala ya siasa. 

Hakuwa nah obi yoyote, hakuegemea sana katika dini aliweza kujigawa vizuri katika sheria na siasa. 

Pia Jinnah hakuwa mtu wa kupenda wanawake kwani alijinidhamisha kwa mwanadada Rattenbai (Rutti) binti wa Sir Dinshaw Petit ambaye alikuwa milionea wa Mumbai. 

Alimuoa mwanadada huyo mnamo mwaka 1918 licha ya upinzani mkali kutoka kwa wazazi wake na watu wengine wa karibu. Baadaye alifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike waliyempa jina la Dina. 

Kutokana na shinikizo kutoka kila upande hawakuweza kuwa na furaha hatimaye walitengana. 

Alikuwa ni dada yake aliyefahamika kwa jina la Fatima aliyeamua kumsaidia kwa kumpa msaada wa kisheria na kampuni. 

Katika masuala ya kisiasa kwa mara ya kwanza Jinnah alionekana mwaka 1906 akiwa na Chama cha Congress kwenye mkutano mkuu uliofanyika Kolkata na kuanzia hapo chama hicho kilianza kupigania uhuru wa taifa la India. 

Miaka minne baadaye alichaguliwa kuwamo katika baraza la kiheria  na ndio ukawa mwanzo wake katika kujiwekea mizizi ya kisiasa hadi kuwa kiongozi mkubwa. 

Jinnah alikuwa amedhamiria kuweka umoja na mshikamano baina ya Wahindu na Waislamu akiwa katika harakati hizo alipewa cheo cha kuwa balozi bora wa Muungano wa Wahindu na Waislamu ambacho alipewa na Gokhale. 

Wakati akiendelea ushawishi wa Mahtma Gandhi katika siasa za India ulianza kuwa juu hivyo aliamua kuachana na Chama cha Congress mnamo mwaka 1920. 

Alipojiondoa alitumia muda wake mwingi katika Muungano wa Kiislamu maarufu Muslim League. 

Katika siasa za Pakistan anachukuliwa kuwa ni baba kutokana na kufuatilia kwa karibu maandiko na mashairi ya Mwanafalsafa Sir Muhammad Iqbal. 

Mvutano wa upande ambao ulikuwa na waamini wengi wa Kiislamu ndio ulifanya kupatikana kwa taifa la Pakistan kwani Waingereza ilibidi waingilie kati ambapo Machi 22-23, 1940 mjini Lahore Muslim League ilifikia mwafaka wa kuanzisha taifa la Kiislamu la Pakistan hivyo ukawa mwanzo wa kujitenga kwake na India ambayo ilikuwa na wanaharakati wengine Mahtma Gandhi na Jawaharlal Nehru ambao walikuwa Wahindu. 

Waingereza walikubali kuwapo kwa taifa la Pakistan mnamo mwaka 1947 na Jinnah akawa kiongozi wa kwanza wa ardhi hiyo huru. 

Alikutana na changamoto nyingi kutokana na uchanga wa taifa hilo; watu wa ardhi hiyo hawakumchukulia Jinnah kama Gavana-Jenerali kama Waingereza walivyotaka wao walimwita Baba wa Taifa. 

Alifanya kazi kwa nguvu na kujituma hadi alipofariki dunia mnamo mwaka 1948 kutokana na umri na ugonjwa. Alizikwa jijini Karachi ambao ni mji mkuu wa Pakistan katika eneo alilozaliwa.



Monday, December 23, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Akihito ni nani?


Desemba 23, 1933 alizaliwa mtawala wa kimila wa Japan Akihito ambaye nashika rekodi ya kuwa Mtawala wa 125 wa Japan. 

Akihito alichukua madaraka hayo ya kimila Januari 7, 1989 hadi yalipokoma Aprili 30, 2019 na mtoto wake Prince Naruhito akishika madaraka hayo. Jina lake ni Tsugu Akihito wa utawala wa Heisei. 

Akihito alizaliwa Tokyo nchini Japan. Ukoo huo wa Heisei unakuwa miongoni mwa koo za kifalme zilizotawala kwa muda mrefu. Akihito ni mtoto wa tano na mtoto wa kwanza wa kiume wa Mtawala wa Japan Hirohito (Emperor Showa) na mama yake ambaye ni Malkia Nagako. 

Tangu akiwa mtoto alianza kuishi katika namna ya kijadi ya Japan kama mtoto wa kifalme ambapo mwaka 1940 alianza kusoma elimu yake katika shule ya Peers. 

Mwishoni mwa vita vya pili vya dunia Akihito alikuwa akiishi nje ya Tokyo lakini alirudi kuendelea na shule mnamo kwa 1949 baada ya vita kumalizika. 

Vita hivyo vilipomalizika viliondoa nguvu ya Mfalme kutawala katika kila sekta isipokuwa katika baadhi ya matukio na kusalia kuwa na nguvu katika sherehe tu.  

Akiwa shuleni Akihito alijitahidi kujifunza lugha ya kiingereza na utamaduni wa Magharibi. Mwalimu wake alikuwa Elizabeth Gray Vining ambaye alikuwa raia wa Marekani. 

Kama ilivyokuwa kwa baba yake Akihito alisomea masuala ya Baiolojia ya Majini. Mnamo mwaka 1952 alipokuwa na umri wa miaka 19 aliingia kama mrithi wa kiti cha Ufalme wa Japan. 

Miaka saba baadaye alivunja rekodi iliyokaa kwa miaka 1,500 alipomuoa mwanamke Shōda Michiko ambaye ni binti mfanyabiashara tajiri katika ardhi hiyo. 

Michiko alikuwa amemaliza elimu yake katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Wanawake jijini Tokyo. 

Akihito ana watoto Prince Naruhito aliyezaliwa Februari 23, 1960, Prince Akishino (Novemba 30, 1965) na Princess Nori (Aprili 18, 1969).  

Akihito alikuwa mtawala wa Japan Januari 7, 1989 baada ya kifo cha baba yake. Rasmi alitawazwa kukalia kiti hicho Novemba 12, 1990. Utawala wake umepewa jina la Heisei ikiwa na maana Kuipata Amani. 

Akihito na Michiko wamezuru maeneo mbalimbali hapa ulimwenguni  wakiwa ni mabalozi wenye nia njema wa Japan. Akihito alionekana kwa mara ya kwanza katika runinga mnamo mwaka 2011 baada ya tetemeko la ardhi na 

Tsunami lililoathiri zaidi upande wa Kaskazini Mashariki  mwa Honshu. 

Tetemeko hilo liliondoa maisha ya watu akali ya 20,000 na kuwa la pili kwa uharibifu baada ya ajali ya kinu cha nyukilia cha Fukushima Daiichi. 

Agosti 8, 2016 alionekana tena katika runinga akiweka bayana nia yake ya kuachia kiti hicho. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 82 Akihito alisema hali yake ya kiafya sio nzuri na kwamba ilikuwa ngumu kwake kubeba majukumu ya kiutawala.


Sunday, December 22, 2019

Hamasa katika Mchezo wa Masumbwi

Bondia Ali Baba Ramadhani kutoka mkoa wa Kilimanjaro

Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani.

Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji.

Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi

Katika kuucheza mchezo wa ngumi wachezaji wawili wanapanda kwenye ulingo uliozungushiwa kamba tatu au nne. Mara nyingi vipimo vya ulingo vinatofautiana kati ya ngumi za ridhaa na kulipwa. Lakini pamoja na tofauti hizo vipimo vya ulingo huanzia futi 12 hadi 20 nikiwa na maana ya 12 kwa 12 za mraba na kuendelea mpaka 20 kwa 20.

Ulingo mwingi wa ngumi za ridhaa ni futi 17 kwa 17 ambapo wa ngumi za kulipwa huwa ni 18 kwa 18. Lakini ulingo unaotumika kwa mapambano ya ngumi za uzito wa juu huwa kati ya futi 18 kwa 18 au 20 kwa 20!

Mchezo wa ngumi huwakutanisha mabondia wawili waliovaa glovu mikono yote miwili zenye uzito sawa kufuatana na uzito wao. Mabondia hawa  hurushiana masumbwi kwenye sehemu zilizokubalika. Sehemu hizi zinaanzia juu ya mkanda kiunoni hadi utosini. Bondia haruhusiwi kumpiga mwingine kwenye kisogo.

Mabondia wote wanatakiwa warushe ngumi zilizokunjwa vizuri na zinazopiga eneo lililolengwa barabara. Kuna majaji watatu ambao wanatakiwa wakae kwenye pembe tatu chini ya ulingo.

Hawa ndio watakuwa wanatoa pointi kwa kila bondia kufuatana na uchezaji wake. Kwenye ngumi za ridhaa pointi  huwa zinatolewa kwa kompyuta baada ya jaji mhusika kubonyeza kidude fulani kila bondia anapompiga mwenzie.

Katika ngumi za kulipwa majaji wanatakiwa waangalie jinsi mabondia wanapocheza na kutoa pointi kufuatana na wanavyocheza. Baada ya kila raundi bondia aliyeshinda hupewa pointi 10 dhidi ya 9 za aliyeshindwa.

Kama bondia mmoja aliangushwa au kuhesabiwa wakati akicheza kwa sababu ya kupigwa sana, pointi zake zinaweza kuwa 10 kwa aliyeshinda na 8 au 7 kwa aliyeshindwa raundi.

Kila baada ya raundi raferii hupita kwa kila jaji na kuchukua vifaratasi wanavyotumia kutoa pointi na kumpelekea kamisaa wa pambano ambaye kwa kawaida hujumlisha pointi za kila raundi na kutangaza mshindi. Refarii ndiye anayeweza kuamuru bondia akatwe pointi anapoona kuwa amecheza rafu!

Mbali na refarii na majaji kuna Kamisaa anayesimamia pambano na kujumlisha pointi zote toka kila jaji ili kumpata mshindi. Kamisaa ndiye kwa kawaida hutoa mshindi atakayetangazwa.

Mpiga kengele ambaye hutakiwa apige kengele kila raundi inapoanza na inapomalizika. Mtunza muda (Timekeeper) anayeangalia muda unaotumika kucheza na kupumzika kila raundi ya pambano.

Watu wengine muhimu kwenye mpambano ni makocha na masekonda wa kila bondia. Watu hawa husimama kwenye kona ya kila bondia kumpa huduma muhimu kama maji, kumfukuzia hewa, kumfuta jasho na kumpa ushauri wa  alivyocheza raundi iliyoisha na mawaidha ya jinsi atakavyocheza kila baada ya raundi.

Kuna pia madaktari ambao hutoa huduma kwa bondia wakati wa mpambano. Daktari pia ana uwezo wa kumshauri refarii amalize mpambano anapoona kwamba mmoja wa mabondia anaumia vibaya na maisha yake yapo hatarini.
Cutman ni mtu anayemhudumia bondia kwenye sehemu zilizokatika kichwani. Mara nyingi cutman ni watu walio na uwezo wa kuziponyeza mikatiko isitoe damu na kumdhuru bondia asiweze kuendelea na mpambano.

Katika nchi zilizoendelea kama nchi za Ulaya, Amerika, Asia na hata Afrika ya kusini karibu kila bondia ana Cutman wake. Hii inatokana na umuhimu wa kumjua bondia vizuri na umbile la uso wake hivyo kuifanya kazi ya cutman kuwa raisi kidogo. Cutman anajua fika jinsi ya kuziziba (kuzuia damu isitoke) majeraha ya usoni ya bondia wake.
Hamasa ya kupenda mchezo wa ngumi inatakiwa ianzie utotoni 
Imetayarishwa na Jabir Johnson kwa msaada wa Onesmo Ngowi, mtalaamu wa Masuala ya Ngumi nchini Tanzania, Desemba 22, 2019. Baruapepe: jaizmelanews@gmail.com

Friday, December 20, 2019

TCRA yasisitiza umuhimu wa usajili laini za simu


Mhandisi Imelda Salum; Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwasababu unawalinda watumiaji dhidi ya wahalifu wanaotumia mitandao sambamba na kuisaidia serikali kuwa na takwimu sahihi ya watumiaji wa huduma za simu za mkononi, zitakazosaidia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Hayo yamejiri Ijumaa ya Desemba 20 mwaka huu wakati wa zoezi la usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za vidole ikiwa ni mwendelezo wa mpango wa Mamlaka hiyo kutoa elimu ya usajili wa laini za simu kwa wafanyabiashara wa soko la Memorial  lililopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Imelda Salum.

“Lengo la kuendesha zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole ni kudhibiti vitendo vya uhalifu unaofanyika kwa njia ya mitandao ukiwepo utapeli  hivyo anasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kusajili laini zenu  za simu kabla ya Desemba 31 mwaka huu ambapo zoezi hilo litafungwa,” alisema Mhandisi Imelda.

“Zoezi hili la usajili wa laini za simu lilianza tangu mwezi Mei mwaka 2019 ambapo serikali ilianza rasmi kusajili laini za simu  kupitia Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA),kupitia mfumo huu wa laini za vidole serikali itaweza kudhibiti vitendo vinavyofanywa kwenye mitandao ya simu ambavyo ni vitendo vya kihalifu kwa sababu tunaamini kabisa wananchi wakisajili laini zao kwa mfumo huu wa alama za vidole tutaweza kuwatambua kwa urahisi watumiaji wote wa huduma za mawasiliano waliopo kwenye nchi yetu,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba, Afisa Tawala ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Moshi Natanael Mshana, amewataka wenye kapuni za simu kuhakikisha  wanakwenda zaidi maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna changamoto ya wananchi kusajiliwa laini zao za simu.

“Asilimia 75 ya wananchi walio wengi wapo maeneo ya vijijini, wananchi hawa  wanahitaji sana huduma hii, niwaombe wenye makampuni kutoka zaidi mjini na kwenda vijijini wazazi wetu walioko vijijini wakipata hii huduma ni rahisi kwao hata watoto wanaoishi mjini kuwatumia fedha,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa  jumla ya laini milioni 19.68, zimeshasajiliwa kwa alama za vidole ambazo sawa na asilimia 72 ya laini zote  zinazotumika  ambazo ni idadi ya laini milioni  47.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi wameiomba Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuharakisha zoezi la utoaji wa vitambulisho ili wananchi waweze kutumia katika zoezi hilo la usajili wa laini za simu.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Jabir Johnson
DATE: Desemba 20, 2019

Afisa Tawala wa Wilaya ya Moshi Natael Mshana akipokea zawadi ya simu kutoka kampuni ya mawasiliano nchini ya Halotel wakati wa usajili wa laini za simu za mkononi. 


Wednesday, December 18, 2019

Milioni 500 noti bandia zakamatwa Dar


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limekamata noti bandia kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 500 na kuwatia nguvuni watu watatu wanaosadikiwa kuwa na kiwanda chenye mitambo ya kufyatua noti bandia maeneo ya Chanika Mkoani humo.

Noti bandia zilizokamatwa ni za shilingi elfu kumi kumi ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 103, noti za shilingi elfu tano tano zaidi ya shilingi Milioni106, noti za shilingi elfu mbili zaidi ya Milioni 45, Dola za Marekani zaidi ya shilingi Milioni 300, fedha za Msumbiji zaidi ya shilingi Milioni 3 na fedha za DRC zaidi ya shilingi Milioni 7.

"Tutaendelea na Kampeni hii ya kuwabaini na kuwakamata wote wanaohusika na mtandao huu kisha kuwapeleka Mahakamani" amesema SACP Lazaro Mambosasa Kamishina wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam.

Akizungumzia tukio hilo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga amesema adhabu inayotolewa kwa mujibu wa sheria kwa sasa ni ndogo sana ambapo amependekeza kuwa kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ili wanaohusika na vitendo hivyo vya uhujumu uchumi kupata adhabu kali ikiwemo kutengwa katika jamii huku akitolea mfano baadhi ya nchi kunyonga wahusika wa makosa ya Uhujumu uchumi.

Hii imetokea zikiwa siku chache zimepita tangu Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Ole Sabaya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na maofisa wa BOT kukamata noti Bandia zaidi ya shilingi milioni 11 wilayani humo.

Basi la Harambee lafeli breki laparamia magari sita mjini Moshi

ACP Said Hamduni 

Zaidi ya abiria 100 wamenusurika kifo baada ya basi la Kampuni ya Harambee iliyokuwa inatokea Arusha kufeli breki na kuyaparamia magari sita ya abiria katikati ya mzunguko wa benki ya CRDB mjini Moshi na kusababisha majeruhi.

Kamishna Msaidizi wa Polisi  mkoa Kilimanjaro  Salumu Hamduni alisema kuwa basi la Kampuni ya harembee ilifeli breki na kuyaparamia magari zaidi sita na kusababisha ajali na  majeruhi wa ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya KCMC na Hospital ya Mawenzi.

Hamduni alisema ajali imetokea majira ya saa kumi na mbili jioni na kwamba jeshi la Polisi inaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kwamba hakuna vifo.

Baadhi ya manusura wa ajali hiyo walisema kuwa basi hilo ilikuwa na mwendo wa kawaida ambapo dereva wa basi la Harambee baada ya kushindwa kulimudu alianza kupiga kelele.

Monday, December 16, 2019

Wagonjwa wenye VVU/Ukimwi Moshi Vijijini wakimbia matibabu

Wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, wamedaiwa kukimbia kiliniki za dawa katika hospital na vituo vya afya, mara baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo,  jambo ambalo limepelekea kusuasua kwa utoaji wa huduma ya ufuatiliaji hasa kwa wagonjwa wanaoishi maeneo ya vijijini.

Aidha wagonjwa hao wengine wamedaiwa kwamba wamebadili hata majina yao halisi huku wengine wakihama kwenye  maeneo wanayoishi na kwenda kuishi katika  mikoa mingine ili wasijulikane hali inayodaiwa kutishia kuwepo kwa ongezeko kubwa la maambukizi ya VVU katika jamii.

Hayo yameelezwa jana na Muuguzi na mshauri nasaha Judith Shayo, ambaye pia ni Mratibu wa kikundi cha Ndekira kilichopo Kibosho  wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kituo kinacho hudumia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Alisema changamoto zinazowakabili wauguzi kwa sasa katika majukumu yao  ni kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa VVU ambao wamekimbia huduma hiyo  hali hiyo inachangia kufifisha juhudi zao katika kupunguza maambukizi .

“Hapa Kibosho kuna wagonjwa walioanza kiliniki vizuri, halafu wamepotea  ghafla wamekuwa hawaji tena kuchukua dawa, tumekuwa tukiwatumia wale walioelimishwa kuwatembelea wagonjwa vijijini, wanapokwenda kuwatafuta wale wagonjwa wanapofika kwa ndugu zao wanaambiwa kwamba huyu mtu alishafariki, au alihama na kwenda kuishi zake mkoani Singida hayupo tena hapa,"

aliongeza kuwa "Inabidi kuwafuatilia huko Singida unakuta hapatikani tena kwenye namba yake ya simu aliyoitoa, hivyo imekuwa changamoto kwetu kwani pia tumegundua wagonjwa wengine wanadanganya majina yao halisi,”alisema.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni kuwa kikundi hicho kimelemewa na watoto wenye mahitaji na hivyo kushindwa kuwahudumia kutokana na mashirika yaliyokuwa yakitoa misaada hiyo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum kujiondoa.

“Changamoto hii ni kubwa mashirika ambayo tulikuwa tukiyategemea yamejitoa hivyo hatuna tena uwezo wa kuwahudumia hawa watoto hii imetuathiri sana kwani fedha ambazo walikuwa wakitusaidia zilikuwa zikitumika kuwaibua watoto ambao wanamahitaji maalum,”asema.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo yalifanyika hivi karibuni, Prof. Patrick Ndakidemi, alisema serikali imeanza kuboresha mazingira katika sekta ya afya  ili kupunguza changamoto zilizopo kwa wauuguzi. “Tuendelee kuwapongeza watoa huduma wetu wa afya  waendelee kutoa elimu ya afya kwenye jamii kuhusiana na maambukizi ya virusi vya ukimwi, kwani takwimu kwa wilaya ya Moshi Vijijini ni asilimia 1.3 haya ni maambukizi makubwa sana  hivyo ni vyema walioko kwenye ndoa na wale ambao bado ni vyema wakawa waaminifu kwenye ndoa zao,”alisema

Vilevile Prof. Ndakidemi ameitaka jamii hususani waliko kwenye ndoa kuwa waaminifu na wenza wao huku wanaokaribia kuoa kuhakikisha kwamba wanachukua jukumu la kupima afya zao kwanza.

Akielezea namna alivyoupata ugonjwa huo mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo (jina tunalo), alisema kutokana na Mama yake mazazi kutokuhuduria kiliniki kwa wakati, “Mimi hapa mama yangu alipokuwa na ujauzito wangu, alikuwa hahudhurii kiliniki  mara kwa mara  alikuwa hajuia kama ana maambukizi ya VVU, nilikuja kujitambua nikiwa darasa la nne,”alielezea kijana huyo.

Katika harambee hiyo zaidi ya Sh milioni 8 zilipatikana pamoja na vyakula , nguo kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi na VVU.

Wednesday, December 11, 2019

LATRA: Usafiri wa treni Moshi utamaliza changamoto ya usafiri


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) Gilliard Ngewe, amesema kuwepo kwa usafiri wa gari Moshi kutaondoa changamoto ya usafiri kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya Kaskazini ambao wengi wao walikuwa wakijikuta wakipata adha kubwa ya usafiri hasa inapofika msimu wa siku za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Ngewe aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari muda  mfupi mara baada ya kuwasili kwa treni ya abiria ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika kituo cha Moshi, mkoani Kilimanjaro ikitokea Jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa miaka mingi abiria waliokuwa wakisafiri kwa kutumia usafiri wa sekta binafsi walikuwa wakilangulia nauli kutoka Sh 20,000 hadi Sh 100,000 hususani katika kipindi cha sikuu ya Krismasi na mwaka mpya.

Katika hatua nyingine  Mkurugenzi huyo alitoa maelekezo kwa TRC  kuhakikisha kwamba maeneo ambayo bado ni korofi kuhakikisha yanarekebishwa ili watumiaji wa usafiri huo waweze kufika kwa muda uliopangwa ili kuondoa usumbufu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TRL Prof. John Kondoro, alisema majaribio ya treni hiyo yanalenga kupima hali ya uhitaji wa usafiri wa treni kwa nyakati mbalimbali.

Prof. Kandoro alisema treni hiyo iliwasili mjini  Moshi  saa tano na nusu  ikitokea Jijini Dar es Salaam ikiwa na mabehewa tisa, saba yakiwa ni ya abiria wa madaraja mbalimbali, moja la mizigo na moja la chakula na kwamba liliwasili mjini Moshi, likiwa na abiria zaidi ya 260.
“Changamoto tuliyokumbana nayo wakati tunakuja na ndiyo imetufanya tuchelewe kuingia ni ile ya baadhi ya miundo mbinu ya reli kuwa ya mashaka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha”, alisema.

Aidha  Prof. Kondoro alisema ilibidi maeneo mengine treni hiyo iendeshwe kwa umakini kutokana na ukweli kuwa usalama wa abiria ni lazima upewe kipaumbele.

“Miundo mbinu hii ndiyo inaanza kutumika sasa baada ya kutokutumiwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, hivyo ni lazima kuwe na tahadhari”, alisema.

Naye  katibu wa Bodi ya (TRC) Hawa Mwenda, alisema tiketi zote za daraja la pili kulala na lile la daraja la pili kukaa, zilikwisha muda mfupi hata kabla baadhi ya abiria waliofika kituo cha Moshi wakitokea Dar es Salaam, hawajaondoka kituoni hapo.

“Taarifa zilizoko eneo la kukatia tiketi ni kwamba tiketi zote 48 za daraja la pili (kulala) na 60 za daraja la pili (kukaa) zimejaa”, alisema na kuongeza, tayari zile za daraja la tatu zilimalizika mapema huku  abiria wanaohitaji bado walikuwa ni wengi.

Bi Mwenda alisema mwitikio wa abiria umekuwa mkubwa kuliko matarajio ya shirika hilo na ilibidi maofisa wa shirika hilo walioko ofisi ya Moshi kuwasiliana na wenzao walioko katika vituo vya njiani kama vile Kisangiro, wilayani Mwanga na kwingeneko, ili kuangalia uwezekano wa kuuza tiketi ambazo hazijapata wateja katika maeneo hayo ili wauziwe wale walioko katika kituo cha Moshi.

Alisema tayari wateja wengi haswa wafanyabiashara wameonyesha nia ya kutumia usafiri huo kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao yakiwemo mazao ya kilimo kwa kile alichosema wameeleza ni kuepuka changamoto wanazokumbana nazo wanapotumia usafiri wa barabara kusafirishia mizigo yao.

Treni hiyo ya abiria, iliwasili Desemba 7 mwaka huu mjini Moshi majira ya saa tano za asubuhi na kupokewa na mamia ya wananchi, ambapo mbali na wale waliokwenda kuwapokea wageni wao, wengi wao walikuwa ni wananchi waliokwenda kushuhudia kuanza tena kwa huduma hiyo ya treni kati ya Moshi na Dar es Salaam, baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miaka 25.

STORY BY: Kija Elias
DATE: Desemba 11, 2019