Tuesday, April 23, 2019

Viongozi wa dini ya Kiislamu watakiwa kuachana na utegemezi

Wito umetolewa kwa viongozi wa dini ya Kiislamu  katika mkoa wa  Kilimanjaro, kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi, ikiwemo miradi ya kilimo na ufugaji ili kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato.
Viongozi wa dini ya Kiislamu mkoa wa Kilimanjaro wakifuatilia mawaidha
Hayo yalibainishwa na mshauri wa mambo ya uchumi wa Baraza la Waislamu Tanzania mkoa wa Kilimanjaro (BAKWATA) Ibrahim Shayo, alipokutana na kuzungumza na uongozi wa misikiti kutoka wilaya za Siha, Moshi na Hai.

Shayo aliwashauri viongozi hao kuongeza maarifa  ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi itakayowawezesha kupunguza utegemezi wa wafadhili kutoka  nje badala yake wabadili fikra na kuanzisha miradi katika misikiti yao ikiwemo ile ya ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki na mingineyo.

“Nawaombeni Maimamu walioko kwenye misikiti, anzeni kubadili fikra zenu  kwa kuanzisha miradi ya kilimo na ufugaji, naamini kwa kufanya hivyo  mtakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato, itakayowezesha katika kusukuma mbele maendeleo ya Waislamu,”alisema Shayo.


Shayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa mabasi ya Ibra Line aliwataka Maimamu wa kila msikiti kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao  kwa kuanzisha miradi ya mbalimbali ya kiuchumi, itakayowasaidia kuleta mapato ya uhakika na kuondokana na hali ya kuwa omba omba.

Katika mkutano huo Mchumi huyo, alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wa Kiislamu kuachana na migogoro ya mara kwa mara iliyopo kwenye misikiti yao na badala yake waanzishe miradi ambayo itaweza kuwakwamua kiuchumi.

Akizungumza kwenye kikao cha viongozi hao wa dini, kilichowakutanisha Maimamu wa misikiti pamoja na Masheikhe wa wilaya za Moshi, Siha na Siha, Katibu wa BAKWATA wilaya ya Moshi, Sheikh Nuhu Mnango,  amewataka Maimamu pamoja na walimu wa Madrasa kujenga upendo ili kuondoa migogoro miongoni mwao.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa Sheikh  Shaaban Rashidi,  amewataka Waislamu kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya waislamu na Uislamu hapa nchini.

Aidha katika kikao hicho Mjumbe huyo wa Baraza la Ulamaa Taifa pia alizindua  kamati tendaji ya Da’awa, ya mkoa wa Kilimanjaro, ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia maadili,  walimu wa dini, kuandaa mawaidha ya kidini, kuwatembelea wajane, wagane, wazee wasiojiweza na watoto yatima.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Jabir Johnson

0 Comments:

Post a Comment