Tuesday, April 9, 2019

Bubu aua mwanafunzi, amfukia kwenye shimo la nyuki

Bubu mwenye umri wa miaka 17 amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mwanafunzi wa darasa la kwanza mkoani hapo.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Aprili 2 mwaka huu majira ya mchana wilayani Mwanga mkoani humo, baada ya baba mzazi wa mtoto aliyefahamika kwa jina la Joseph Ernest kuripoti katika kituo cha polisi cha Mwanga kuhusu kwa kupotea kwa mtoto wake aliyemtaja kwa jina la Ernest Joseph mwenye umri wa miaka minane.

Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Hamisi Issah alisema uchunguzi umefanyika na kubaini kuwa bubu huyo ni Mpare mkazi wa Kisangara anafahamika kwa jina la Jackson Jeremia. 

ACP Issah aliongeza kuwa baada ya kubaini mwili wa marehemu ulikofukiwa jeshi lake lilikwenda kwa ajili ya uchunguzi na kubaini kuwa maiti ilikuwa imelazwa kifudifudi na ilikuwa imeanza kuharibika hivyo hatua za kitaalamu zilichukuliwa na kisha kuukabidhi kwa ndugu wa marehemu kwa mazishi. 

Marehemu alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Chanjale iliyopo Kisangara wilayani Mwanga. 

Taarifa zaidi zilisema mara ya mwisho mtuhumiwa huyo alikuwa na marehemu katika machungo ya mbuzi. 

Aidha mazingira ya kuufukua mwili wa marehemu yalikubwa na changamoto baada ya timu ya wataalamu wa misitu, daktari na polisi kuukuta ukiwa umefukiwa kwenye shimo lililojaa nyuki. 

Kupitia wataalamu wa lugha ya alama mtuhumiwa alikiri kutekeleza mauaji hayo kwa madai kuwa mtoto huyo alimwimbia mbuzi wake. 

Chanzo kingine kilidai kuwa marehemu alifukiwa shimoni hapo akiwa bado hajafa. Hata hivyo bubu huyo sio mgeni kwa wakazi wa Kisangara kwani hii ni mara ya tatu kufanya mauaji na mara zote amekuwa akisamehewa kutokana na umri wake kuwa bado ni mtoto.

0 Comments:

Post a Comment