Awali ya yote nitoe pole kwa
familia ya riadha kwa kuondokewa na wakongwe katika mchezo huo Zakaria Gwandu
na Samwel Tupa ambao wamefariki dunia Oktoba mwaka huu. Ni pigo kubwa katika mchezo
huu Mwenyezi Mungu Muumba wa vyote aifariji familia ya riadha. Amen.
Ron W. Davis (wa kwanza kushoto) akiwa na Filbert Bayi mwaka 2019 alipomtembelea Kibaha, Pwani. |
Makala yaliyopita tuliangazia namna
ambayo Ron Davis alivyopigiwa simu kutoka Tanzania kuwa amechaguliwa kuwa kocha
mkuu wa timu ya taifa ya riadha.
Pia tuliishia pale aliporudi Nigeria
na kwenda kuiaga timu ya taifa hilo na kuanza safari ya kuja Tanzania. Katika
safari yake kuja nchini, alitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam ambako alishangazwa na umati wa wanahabari waliokuwa
wakimsubiri kwa shauku.
Kilichomstaajabisha alikuwa
hajawahi kuona hapo kabla. Ilikuwa ngumu kuamini kwani watu hawakuficha shauku
na matarajio yao kwake katika medani ya riadha.
Katika makala haya tutaendelea
kumwangazia Ron Davis baada ya kufika nchini Tanzania katika nafasi yake mpya
ya kocha mkuu wa timu ya taifa kwenye mchezo wa riadha alianza vipi.
Ron Davis alisema, “Tangu siku ya
kwanza nilipowasili katika kazi ya ukocha, nilipata uungaji mkono mzuri kutoka
kwa mheshimiwa Chadiel Mgonja, aliyekuwa Waziri wa Utamaduni na Michezo wakati
huo.”
Mmarekani huyo aliongeza kusema
kupitia Mgonja aliunganishwa na maofisa mbalimbali wa riadha wa timu ya taifa
ya Tanzania. Pia Ron Davis alikumbusha kuwa uungwaji mkono katika
kila kitu katika ukocha wa riadha alipata kutoka kwa mtu mmoja aliyemtaja kwa
jina la Zambi.
Huyu Zambi wakati huo alikuwa
Katibu Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki (TOC) ambaye awali alikuwa akimnoa
mkongwe Filbert Bayi.
“Labda mtu ambaye alionyesha zaidi
ukaribu katika kazi ya ukocha alikuwa Profesa Sangui ambaye alikuwa Daktari wa
Timu ya Taifa ya Riadha ya Tanzania,” alisema Ron Davis.
Ron Davis aliongeza kuwa Profesa
Sangui alikuwa mbele kumpa taarifa zote kwa kina na kumshauri kuhusu riadha na
mazingira ya Tanzania hali ambayo ilimpa uzoefu mkubwa wa namna ya kuendana
mazingira na mafanikio makubwa kwa wanariadha nchini.
“Unapokuwa na mtu kama yule (Prof.
Sangui) ambaye anakuamini na anakuunga mkono katika kila njia, hali hiyo
inapunguza mahangaiko katika mazingira mapya ambayo yana changamoto zake,”
aliongeza Ron Davis.
MAANDALIZI KUELEKEA DAKAR 1979
Baada ya kuwasili nchini Ron Davis
alipewa taarifa kwamba wataanza safari ya kwenda Arusha ili kujiandaa na
Mashindano ya Afrika ya Riadha (ACA) ambayo yalifanyika Dakar kuanzia Agosti
2-5, 1979.
Timu ya taifa ya Riadha ilikuwa
kambini mkoani humo kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.
Ikumbukwe Nigeria iliongoza kutwaa
medali kati ya nchi 24 zilizoshiriki katika matukio 39 yaliyowaleta wanariadha
251 pale Stade Demba Diop jijini Dakar.
Katika michuano hiyo ya ACA,
Tanzania iling’ara katika mbio ndefu ambazo medali ya fedha ilibebwa na Gidamis
Shahanga aliyekimbia kwa saa 2:36:46 akizidiwa na raia wa Ethiopia Kebede
Balcha alikimbia kwa saa 2:29:53 aliyetwaa medali ya dhahabu.
Katika kurusha mkuki Tanzania ikiwakilishwa
na Zakayo Malekwa ilitwaa medali ya fedha. Malekwa alirusha mita 76.74 akiachwa
nyuma kwa sentimeta 68 na raia wa Ivory Coast Jacques Aye Abehi aliyetwaa
medali ya dhahabu.
Pia Tanzania katika michuano hiyo
ilianza kwa mara ya kwanza mwaka huo ilishika nafasi ya tatu katika mchuano wa
mbio za vijiti mita 400 kwa dakika 3:11.5a.
Baada ya historia hiyo ya
yaliyojiri wakati huo turudi katika mwaka ambao Ron Davis anafika Tanzania na
kupewa taarifa za kwenda Arusha iliko timu ya taifa. Viongozi wa riadha
walimwambia kuwa Arusha itakuwa kambi ya timu ya taifa ya riadha kwenye
michuano ya olimpiki mwaka 1980.
RON DAVIS, FILBERT BAYI WAKUTANA TANZANIA
Kabla ya kwenda Arusha alikaa
takribani siku saba na alipewa taarifa kwamba Bayi anataka kukutana naye
kipindi hicho Bayi alikuwa mwanariadha bado kijana tu.
“Nilifurahi sana kupata fursa ya
kukutana na Filbert uso kwa uso na nikaona ni fursa ya kuzungumza naye namna
ambavyo tutafanya kazi pamoja,” alisema Ron Davis.
Ron Davis aliongeza kuwa
walikubaliana kukutana katika mgahawa mmoja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
chai na biskuti. Hata hivyo alipenyezewa kuwa Bayi anataka kuzungumza naye
kwani hajafanya mazoezi yoyote tangu Michuano ya Jumuiya ya Madola 1978 ilipomalizika
kutokana na majeruhi.
Muda uliwadia Ron Davis akakutana
na Bayi, katika mazungumzo yao Bayi aliweka bayana kuwa hafahamu ni lini
atarudi katika mazoezi na alikuwa njiani kuelekea Ujerumani kwa matibabu.
Hata hivyo Bayi alimhakikishia kuwa
atakuwa sawa na ataweza kujiandaa kwa ajili ya mazoezi kuelekea michuano ya
olimpiki. Baada ya mazungumzo na nyota huyo Ron Davis alifurahi kuonana naye
kujua hatima ya changamoto iliyokuwa ikimkabili mwanariadha huyo wa kiwango cha
kimataifa na aliyeweka rekodi ya kimataifa.
“Ni kwa namna gani majeruhi yake
yataathiri mazoezi,” alijiuliza Ron Davis.
Pia Ron Davis alijiuliza baada ya
kupona majeruhi hayo ataweza kurudi katika kiwango chake bora na kama atarudi
katika kiwango chake atachukua muda gani.
Haikutosha Ron Davis alijiuliza
endapo Bayi ataweza kufundishika na kuamini mafunzo yake.
Hayo yote yalikuwa ni maswali
ambayo yalimsumbua kwa kiasi kikubwa Ron Davis ambaye alikuwa ameanza kazi yake
ya kuwanoa wanariadha wa Tanzania akiwamo Bayi ambaye alikuja kuweka rekodi ya
kwanza ya kuipa medali ya kwanza ya Olimpiki nchi ya Tanzania. Nini kilitokea
baada ya Bayi kwenda Ujerumani kupata matibabu? Tukutane Makala yajayo.
Makala haya
yametayarishwa na Jabir Johnson ambaye alipata fursa ya kuzungumza na Ron
Davis katika masuala mbalimbali ya maisha yake na medani ya riadha
alipotua nchini Tanzania. Kwa maoni ushauri barua pepe: jaizmela2010@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment