Maajabu
hayawezi kwisha, Maajabu si tunayaona kila siku za maisha yetu? Maajabu, hakika
hayawezi kwisha, Maajabu kila mahali maajabu, Maajabu katika ardhi na katika
mbingu, Maajabu katika bahari, Maajabu kwako mwenyewe na mazingira
yanayokuzunguka, Maajabu katika Jua, mwezi na nyota, Maajabu katika miti na
nyasi, Maajabu katika vilivyo hai na visivyo hai, Maajabu hayawezi kwisha;
ndivyo makala haya yanavyoanza.
Reptilia ni
aina ya viumbe ambao hutambaa, kwa mujibu wa Wikipedia reptilia ni kundi la
wanyama wenye damu baridi, ngozi ya magamba badala ya nywele au manyoya
wakipumua kwa mapafu.
Huzaa kwa
njia ya mayai; wengine hutaga mayai na watoto wanatoka nje bila ngazi ya
kiluwiluwi au kwa spishi kadhaa mayai yanaiva ndani ya tumbo la mama na watoto
wanazaliwa hai.
Kibiolojia
ni ngeli ya vertebrata. Jina Reptilia limetokana na maumbile yao maana
wanatambaa na tumbo juu ya ardhi; ama kwa miguu mifupi kama mijusi au bila
miguu kama nyoka. Reptilia wanapatikana maeneo yote ulimwenguni isipokuwa
katika bara la Antaktika.
Shukrani za
pekee zimwendee mwanasayansi mwenye asili ya Italia Josephus Nicolaus Laurenti
(4 Desemba 1735 - 17 Februari 1805), ambaye alizaliwa na kufia jijini Vienna
huko Austria kwani ndiye aliyefanya ugunduzi wa neno hili Reptilia baada ya
utafiti wa muda mrefu.
Hata hivyo
mpaka sasa kumekuwa na makundi makubwa ya reptilia lakini miongoni mwa viumbe
hao ni Kobe.
KWANINI
KOBE?
Kobe/Makobe
ni wanyama wadogo hadi wakubwa wa oda ya Testudines katika ngeli ya Reptilia.
Spishi zinazoishi baharini huitwa kasa. Kiwiliwili chao kimefunikwa kwa gamba
gumu liitwalo galili.
Kwa kawaida
galili hii ni yabisi, lakini kuna spishi zilizo na galili nyumbufu, zote spishi
za maji. Kichwa, miguu na mkia inachomoza kutoka galili lakini katika spishi
nyingi inaweza kuvutwa ndani hususani spishi za nchi kavu. Bara la Afrika ni
miongoni mwa maeneo ambayo kobe hupatikana kwa wingi.
Vyanzo
mbalimbali vimetoa aina za kobe na majina yake hususani katika ‘Familia’ ya
Testudinidae kama vile Kobe Dubwana wa Aldabra, Kobe-bawaba wa Bell,
Kobe-bawaba Misitu, Kobe-bawaba wa Speke, Kobe-chapati, na Kobe-chui.
Kobe Tom ni mojawapo ya kobe ulimwenguni wa aina ya Aldabra ambao wanaweza kuishi miaka akali ya 250. |
KOBE DUBWANA
WA ALDABRA YUKOJE?
Hawa ni kobe
wenye maumbo makubwa ambao inadaiwa ndio wanaoishi muda mrefu kuliko kobe
wengine wote ulimwenguni. Imedaiwa kuwa wana uwezo wa kuishi ulimwenguni kwa
zaidi ya miaka 200 na wakati mwingine inakuwa vigumu kuwajua muda ambao
wameishi kutokana na kujificha wasionekana na wanadamu.
Barani
Afrika walio wengi waliingia wakitokea nchini India na kufikia katika visiwa
vya Ushelisheli wakiwa mikononi mwa walowezi kutoka Ulaya. Ushahidi mwingine wa
walowezi kutoka barani Ulaya kama Jan van Riebeeck alipogundua mji wa Cape Town
nchini Afrika Kusini mwaka 1652.
Vyanzo
vinasema mwishoni mwa miaka ya 1903 walowezi kutoka Ulaya wapatao 280 walitua
Afrika Kusini. Hali hiyo imekuwa tofauti kidogo wa kwa Kobe Dubwana wa Aldabra
aliyepo Kilimanjaro nchini Tanzania.
Mkoani
Kilimanjaro kobe huyo ambaye yupo hadi hii leo inadaiwa kuwa alifika katika
maeneo ya Masama katika mashamba ya walowezi miaka ya 1850. Mwaka 1844 ukanda
wa Afrika Mashariki ulifikiwa na walowezi kutoka Ujerumani Johann Ludwig Krapf
and Johannes Rebmann walipeleka taarifa za maeneo muhimu ya uwekezaji.
Hivyo kundi
kubwa miaka michache baadaye lilianza kuja Afrika Mashariki na miongoni mwa
maeneo waliyofika ni mkoa wa Kilimanjaro.
Kilimanjaro
ni miongoni mwa maeneo yenye mashamba makubwa ya kahawa, baada ya uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961 ardhi ilibidi ilirudi serikalini hadi leo ambapo serikali
ya Tanzania imekuwa ikiwapa wawekezaji kwa ajili ya kuyaendeleza.
Aldabra aliyepo katika Mashamba ya Tudeley,
Masama wilayani Hai katika mkoa wa Kilimanjaro anafahamika kwa jina la ‘Tom.’
‘Tom’ ni
kobe dume ambaye hadi tunavyoongea hajawahi kufanya mapenzi ili kuendeleza uzao
wake kutokana na kushindwa kupata jike la kumfariji kwa muda wote tangu kuonja
hali ya hewa ya dunia.
Mkurugenzi wa Tudeley Jesse Natai |
Mkurugenzi
wa Tudeley Jesse Natai alisema Tom amekuwa katika wakti mgumu wa kuendeleza
uzao wake kutokana na kukosekana kwa jike.
“ Wakati
nachukua mashamba haya ya kahawa nilimkuta, na historia yake imekuwa
ikitofautiana lakini ambayo inaaminiwa ni ile ya wakati walowezi walipofika
mkoani Kilimanjaro miaka ya 1800,” alisema Natai.
Pia mpaka
sasa Wizara ya Maliasili bado haijatilia mkazo uzito suala la Tom ili
ikiwezekana awe kivutio cha watalii. Pia
Natai ameshauri ikiwezekana atafutiwe jike ili mbegu yake isipotee.
Natai
aliongeza kuwa kuna wakati Tom hupiga kelele na kujigaragaza kwenye matope
akijichua kwa takribani saa mbili kutokana na kukosa huduma hiyo.
Kinachostaajabisha
kwa Kobe Tom ni kwamba anapendelea zaidi rangi nyeusi, pindi akiona mtu ameivaa
nguo ya rangi hiyo hutoa mlio wa kukubali na kuanza kumfuata mtu huyo.
Hayo ndiyo maajabu ya Kobe Dubwana wa Aldabra aliyepo Kilimanjaro maarufu Kobe Tom. Hakika Maajabu hayawezi kuisha.
Hayo ndiyo maajabu ya Kobe Dubwana wa Aldabra aliyepo Kilimanjaro maarufu Kobe Tom. Hakika Maajabu hayawezi kuisha.
Makala haya yametayarishwa na Jabir
Johnson, kwa maoni au ushauri 0768 096 793 au baruapepe: jaizmela2010@gmail.com
Pia ilitolewa katika gazeti la
Tanzania Daima
0 Comments:
Post a Comment