Wednesday, April 10, 2019

Mkojo wa Ngamia gumzo Kilimanjaro

Mwaka 2018 ulisikia kuhusu uvumbuzi wa watafiti katika chuo kimoja cha Cape Town nchini Afrika Kusini, walipotengeneza tofali kwa kutumia mkojo.
Mwandishi wa makala haya Jabir Johnson akiwa katika boma la ngamia wa Mzee Dahir Jamal Yusuf. PICHA NDOGO ni Mzee Dahir na kijana wake katika boma la ngamia huko Mtakuja, Hai mkoani Kilimanjaro.

Maswali yanaweza kuwa mengi kivipi wavumbuzi hao walifanikiwa kutengeneza tofali kwa kutumia mkojo na ni mkojo wa kiumbe kipi, walilitengenezaje tofali hilo, walichanganya na nini na tofali lililotoka hapo lilikuwa na harufu ya mkojo au nini kilitokea?

Pia wakati fulani huko mkoani Njombe ulisikia kuhusu mkojo wa sungura kutibu mazao. Haikutosha Chuo cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro kilifanya uvumbuzi wa mkojo wa paka ulivyowanufaisha wakulima dhidi ya mapambano na panya waliokuwa wakiharibu mazao. Hakika ilikuwa ni habari ya mkojo, mkojo, mkojo tu.

Tuanzie hapa mwandishi wa vitabu Enock Maregesi katika nukuu zake maridhawa anasema, “Kila sumu ina kiuasumu chake. Viuasumu vya 'cyanide' ni 'amyl nitrite', 'sodium nitrite', 'cyanokit', na 'sodium thiosulfate'. Kazi ya viuasumu hivi ni kuzalisha madini mengi ya chuma mwilini. Madini haya yatapambana na maada za rangi za uhai ('cytochromes') kwa ajili ya 'cyanide', ili 'cyanide' ing’ang’anie kwenye kiuasumu badala ya kung’ang’ania kwenye vimeng’enya vya seli za mwilini. Kiuasumu kinaposhinda mpambano huo; 'cyanide' hutolewa nje kwa njia ya mkojo, na mwathirika wa 'cyanide' hupona kabisa. 'Sodium thiosulfate' ndiyo bora zaidi kuliko 'amyl nitrite' au 'sodium nitrite', na ndiyo bora zaidi kuliko 'cyanokit'.”

Machi mwaka huu Mwana mitindo wa mavazi mwenye umri wa miaka 37 nchini Uingereza alijitokeza hadharani na kudai kuwa kila siku amekuwa akinywa mkojo wake.

Fabian Farguharson amekuwa akinywa matone kadhaa ya mkojo wake kwa muda sasa baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa mkojo una manufaa kiafya. Kiasi cha nusu lita kila siku amekuwa akitumia ili kumkinga na maradhi ya tumbo.

Alikaririwa akisema alianza kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka 2015 na kwamba baada ya dakika 30 huanza kujihisi kupata nguvu na maumivu ya tumbo hupungua taratibu.

Maendeleo ya kasi katika teknolojia ya mtandao wa intaneti yalimfanya mwanamitindo huyo mzaliwa wa Sheffield, South Yorkshire nchini Uingereza kupata suluhisho la matatizo ya tumbo. Anasema mwaka 2013 alianza kufanya utafiti hadi kufikia hapo. Hayo yote ni suala la mkojo.

MKOJO NI NINI?
Kwa mujibu wa kamusi ya wavuti ya Wikizero inasema, “ni kimiminika ambacho ni takamwili itokanayo na mwili na ambayo huzalishwa na figo, halafu hutolewa mwilini kupitia urethra.

Katika simulizi tofauti tofauti inaelezwa kuwa mkojo na urea kwa wanaotumia kama tiba mbadala inasaidia kupunguza maambukizi ya saratani mwilini.

Vimelea vya kansa vinaweza kusafirishwa kwa njia ya mkojo, sasa kwa kutumia mkojo kama kinywaji, vimelea hivi vinaweza kuingia kwenye mfumo wa kinga mwilini na kusaidia urutubishwaji wa kinga mwilini.

HALI IKOJE MKOANI KILIMANJARO
Mfugaji wa Ngamia katika kijiji cha Mtakuja wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Dahir Jama Yusuf (87) ameanza kujizolea umaarufu kupitia tiba yake inayotokana na mkojo wa ngamia.

Amekuwa mfugaji wa wanyama hao katika ardhi hiyo baada ya kuachana na ufugaji wa ng’ombe na mbuzi kutokana na uharibifu wa mazingira na uhaba wa vyakula vya wanyama hao; hali ambayo ilikuwa ikimfanya mzee huyo kutokuwa na makazi ya kudumu.

Alianza kufuga mwaka 1996. Alianza na ngamia saba lakini sasa anao 80. Lakini cha kustaajabisha kwa mzee huyo ni matumizi ya mkojo wa ngamia kwa tiba. 

Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan anasema katika tafsiri yake katika Firqatunnajia anasema, “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuunywa kwa yule aliyepatwa na homa. Inajuzu kuunywa kwa kuwa ni msafi. Mkojo wa ngamia ni msafi na inajuzu kujitibu nao na kuunywa.”

Dahir anasema, “ Mimea ambayo ngamia anakula ndiyo inayofanya mkojo kuwa imara kwa tiba, lakini ni mchungu wakati unapounywa.”

Mzee Dahir aliongeza kuwa yeye mwenyewe alikuwa anaumwa wakati fulani katika maisha yake lakini alipotumia alipona maradhi ya tumbo.

Hata hivyo Mzee Dahir alisema, “Nimeshuhudia mimi mwenyewe watu wakipona vidonda vya tumbo, pressure, kisukari, malaria, tumbo kuumwa, chango, miguu kuvimba na figo.”

USHUHUDA WA WALIOPONA KWA MKOJO WA NGAMIA
Mzee mwenye umri wa miaka 54 aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Simmeli anasema, “Siku ya kwanza ilitaka kunishinda, lakini baadaye nilizoea, haileweshi, hailegezi, ila ni chungu ikianza kufanya kazi kinachofuata ni kuharisha.”

Simmeli anasema alitumia mkojo huo kwa miezi mitatu hali ya vidonda vya tumbo ikawa imeisha kabisa. Simmeli anaongeza, “Mama yangu Anna Simmeli (75) alikuwa anaumwa asthma ilikuwa ikimtesa wakati wa masika baada ya kumpeleka kwa mzee wetu huyu baada ya miaka mitatu hatujasikia tena tatizo kwa mama yetu.”

Sasa baada ya kusikia habari za mkojo huo kuwa una manufaa kwa wenye magonjwa yaliyotajwa mkoani Kilimanjaro hususani Manispaa ya Moshi wameanza kumfuatilia mzee Dahir kwa siri kwa ajili kupata tiba kutokana na kushindika kwa madawa ya hospitalini.

Mmojawapo anasema, “Bibi yangu ana maradhi…vidonda vya tumbo kwa kweli vinamsumbua muda sasa…nitaenda kwa mzee huyo.”

Kuna uwezekano mkubwa mzee huyo akajipatia umaarufu kama wakati ule wa ‘Babu wa Loliondo’ kutokana na kundi kubwa la watu mkoani Kilimanjaro na nje yake kuwa na maradhi ambayo yanaweza kutibiwa kwa kutumia mkojo wa ngamia.

Lakini sharti la mkojo huo ni kuunywa wakati ngamia anapokojoa hususani majira ya asubuhi. Wataalam wa Fiziotherapia nchini Tanzania bado hawajafikiria kumwona Mzee Dahir Jama Yusuf na kutaka kujua kwa undani kuhusu mkojo wa ngamia unavyoweza kuwasaidia watu.

Chanzo kimoja kinasema mkojo una mamilioni ya chembechembe za homoni, metaboliti na corticosteroidi. Pia una virutubisho vingine vingi kama Vitamini C.

Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson; kwa maoni au ushauri 0768 096 793 au baruapepe: jaizmela2010@gmail.com

0 Comments:

Post a Comment