Friday, April 12, 2019

Ujenzi wa Mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji watakiwa

Serikali imeshauriwa kuwekeza katika ujenzi wa mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupambana na mabadiliko tabianchi.
Bwawa la Kidunda
Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa kampuni ya Tudeley Estates Limited  Jensen Natai inayojushughulisha na kilimo cha Kahawa, alisema kutegemea mvua kila msimu ni kuchelewa kuwa na mazao kwa wakati.

Alisema endapo serikali itawekeza katika ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji  hali itakayo saidia kuzalisha chakula cha kutosha.

Mwekezaji wa Tudeley Estates Limited  mkoani Kilimanjaro alisema,  “Maji ni kitu cha jamii hivyo serikali ikijenga mabwawa ambayo yatakuwa yakikusanya maji kisha kuyatawanya kwa wakulima itapandisha ubora wa kilimo cha Tanzania, kutegemea mvua ni changamoto.”

Natai alisema joto likizidi katika baadhi ya mazao kama kahawa na ubora wake unapungua hivyo hasara inakuwa kubwa kwa mkulima.

“Ni kweli kabisa uwekezaji katika mabwawa ni ghali yapata kama bilioni moja ya Tanzania kwa bwawa moja,” alisema mwekezaji huyo.

Natai aliongeza kwa sasa katika mashamba yake anatumia maji yanayotoka katika miteremko ya mlima Kilimanjaro.

“Tanzania hii imefanyika utafiti kuwa ina maji mengi, lakini serikali pekee ndiyo yenye uwezo wa kuwekeza katika mabwawa hayo ili kukusanya maji hayo, hapo kilimo kitakuwa na maana hata Tanzania ya viwanda tunayoitaka itasonga mbele na kwa njia hiyo tutaacha utegemezi,” alisema Natai.

Story by: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment