Wednesday, April 24, 2019

Bandari ya Tanga kujenga bandari kavu Arusha


Meneja wa Bandari ya Tanga Percival Salama akizungumza kuhusu mkakati wa upanuzi wa bandari ya Tanga; kushoto ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Kilimanjaro (MEK), Bahati Nyakiraria na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Aisha Amour.
Bandari ya Jiji la Tanga, ina mpango wa kuanza kujenga bandari kavu katika  eneo la Malula lililopo  wilayani Arumeru Jijini Arusha, lengo likiwa ni  kuhudumia soko la mikoa ya Kanda ya Kaskazini na nje ya Tanzania.
Hayo yalielezwa na Meneja wa Bandari Tanga, Percival Salama, wakati akizungumza kwenye mkutano na wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro na  Arusha, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro jana.

Salama  alisema katika  kuboresha  utoaji wa huduma  bandari ya Tanga  imeona  kuwekeza bandari kavu katika kanda ya Kaskazini mikoa ya Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro  ili  kupanua wigo wa utoaji wa huduma katika bandari hiyo.

Salama alisema kuwa bandari hiyo bandari hiyo imenunua mitambo mipya ya kisasa 20 kati ya hiyo mitambo 16 imeshawasili katika bandari hiyoo.

“Bandari ya Tanga inaelezwa kuwa bandari ya kipekee na ya aina yake barani Afrika inayoweza kuhudumia nchi saba kwa kutumia mpaka mmoja”alisema Salama.
Meneja wa Bandari ya Tanga Percival Salama katika picha ya pamoja na waandishi wa habari.
Alisema mbali na kuwa na uwezo wa kuhudumia nchi saba bandari ya Tanga ina sifa ya kuwa bandari pekee ya asili kutokana na kuwa na kina cha maji cha asili cha kuanzia mita tano hadi 30.

  “Serikali ya awamu ya tano imayongozwa na Rais Dk John Magufuli, iliamua kutoa fedha za kuwekeza katika miradi ya uboreshaji wa bandari ili kuongeza ufanisi,” aliongeza Salama.

Alisema maboresho makubwa ya bandari hiyo kwa sasa inaongoza kuwa bandari inayohudumia mizigo kwa kasi Afrika Mashariki, yamefanyika katika nyanja ya ukarabati na ununuzi wa mitambo mipya, ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhia mizigo, na uboreshaji wa mifumo ya teknolojka ya habari na mawasiliano.

Alisema Bandari ya Tanga ambayo ina lango kubwa kuliko bandari yeyote Afrika Mashariki la mita 1200, inatarajia kuhudumia shehena ya mizigo tani 1,267,000 kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na tani 646,718 za mwaka 2017/2018.
Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro Aisha Amour akizungumza na waandishi wa habari.
“Mteja anakuja anakaa siku tano anatoa mzigo, kesho hawezi kuja tena lakini sisi hapa mtu akija kuchukua mzigo anaondoka siku hiyo hiyo na meli ikija hapa haisubirishwi kwenye eneo la bahari kama kwenye bandari zingine bali inaingia moja kwa moja kushusha au kupakia mzigo,” alisema Salama.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa semina hiyo ya siku moja Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Aisha Amour alisema itafungua fursa ya ajira kwa wakazi wa kanda ya kaskazini na kupunguza msongamano wa wafanyabiashara kwenda umbali mrefu kufuatilia mizigo yao.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Kilimanjaro (MECKI), Bahati Nyakiraria akiagana na Meneja wa bandari ya Tanga Percival Salama baada ya kuhitimisha semina ya siku moja kwa wanahabari wa mkoa wa Arusha na Kilimanjaro iliyofanyika mjini Moshi.

0 Comments:

Post a Comment