Thursday, April 11, 2019

Takukuru yawashikilia Maafisa wa NIDA na Mwalimu wa Sekondari

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Kilimanjaro inamshikilia mwalimu wa sekondari kwa kukutwa na vitambulisho vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mkuu wa Takukuru  Mkoa  wa Kilimanjaro Holle Makungu alisema Aprili 9 mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa mwananchi (jina limehifadhiwa), akieleza kudaiwa rushwa ya shilingi laki moja na maafisa wa NIDA ili apewe kitambulisho.

“Mwananchi (jina tunalihifadhi) alitueleza kitendo hicho kutakiwa kulipa shilingi laki moja na mafisa wa NIDA ili apewe kitambulisho chake, kitu ambacho ni kinyume na kifungu cha 15 cha sharia ya kuzuia na kupambana na Rushhwa Na. 11/2007,” alisema Makungu.

Makungu aliongeza kuwa mtego uliandaliwa uliofanikiwa kumnasa Hemed Shaban ambaye amekuwa akijitambulisha kuwa ni Afisa wa NIDA. 

Aidha mkuu huyo wa Takukuru alisema mtuhumiwa ambaye ni Mwalimu wa Sekondari ya Kiusa iliyopo katika Manispaa ya Moshi alipekuliwa na kukutwa na vitambulisho vya NIDA ambavyo havijawafikia walengwa. 

Hata hivyo Makungu alisema uchunguzi unaendelea kuwabaini Maafisa wa NIDA na wote waliohusika na uvunjaji wa sheria ili waweze kuchukuliwa hatua kali.

“Uchunguzi  zaidi unaendelea ili kubaini watumishi  wa NIDA wanaohusika kumpa Hemed  vitambulisho hivyo, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba  11/2007,” alisema Makungu.

0 Comments:

Post a Comment