|
Wanariadha katika mbio ndefu za Kili Marathon mwaka 2017. Photo by Rachel Ambrose |
Vita kuu ya kwanza ya dunia ilianza kutokana na ugomvi kati
ya Austria-Hungaria na Serbia.
Kutokana na muundo wa mikataba ya kusaidiana
kati ya nchi za Ulaya mwanzo huo ulisababisha mfululizo wa hali ya vita kati ya
mataifa, na mengine ya Balkani yalitafuta uhuru wao.
Juni 28, 1914 katika mji
wa Sarajevo, Bosnia, mwana wa Kaisari wa Austria aliyekuwa mfalme mteule
aliuawa pamoja na mke wake na gaidi Mserbia mwanachama wa kundi la "Mkono
Mweusi" lililopinga utawala wa Austria-Hungaria katika Bosnia.
Austria iliamuru
Serbia ifuate masharti makali katika uchunguzi wa tendo lile.
Serbia ilipokataa sehemu ya mwisho ya masharti, Austria
ilitangaza hali ya vita dhidi ya Serbia Julai 28, 1914. Agosti ya 1914 ulikuwa
ni mwezi ambao vita hii ilipanuka zaidi, Warusi walikuwa na mkataba wa usaidizi
na Serbia wakatangaza hali ya vita dhidi ya Austria-Hungaria.
Hapo wakaingia Wajerumani waliokuwa na mapatano ya usaidizi
na Austria-Hungaria wakitangaza hali ya vita dhidi ya Urusi.
Urusi kwa upande
wake ulikuwa na mkataba wa kusaidiana na Ufaransa, kwa hivyo hali ya vita
ikajitokeza pia kati ya Ufaransa na Ujerumani.
Uingereza ilijiunga na vita baada ya Wajerumani kuvamia eneo
la Ubelgiji kwa shabaha ya kupita eneo lake haraka kwa uvamizi wa Ufaransa
Kaskazini. Japan iliyokuwa na mkataba wa kusaidiana na Uingereza tangu mwaka
1902 iliona nafasi ya kukamata koloni za Ujerumani katika Pasifiki ikaingia
upande wa maadui wa Ujerumani.
Ilipofika Oktoba 1914 himaya ya Ottoman (Uturuki) ilijiunga
na vita hivyo kutokana na mkataba wake wa siri na Ujerumani.
Kwanini katika
vita hiyo Ujerumani inazungumzwa sana licha ya ugomvi kuanza sehemu nyingine?
Jambo la kujifunza hapo ni kwamba Ujerumani ilikuwa na kila sababu ya kujivunia
wakati wa vita hivyo kutokana na uimara na ukamilifu wake katika maandalizi.
Majeshi ya Ujerumani yalikuwa makini hadi ilifikia hatua
wanajeshi wa taifa hilo walikuwa wakipoteza maisha wakiwa na furaha tele kwa
ajili ya taifa lao pindi mapambano yalipokuwa magumu zaidi.
Sasa katika taifa
hilo kulikuwa na uungwaji mkono kutokana na misingi mizuri kupitia kauli mbiu
yao ‘Kultur.’
Kwa kiapo cha Kultur walifanikiwa sana kuyafagia majeshi ya
wapinzani katika vita hivyo.
Lakini siri kubwa ilikuwa kwa watu wawili ambao mara kadhaa
hawatajwi sana lakini waliiweka Ujerumani hapo ilipo.
Watu hao ni Adalbert Falk
ambaye alikuwa Waziri wa Elimu wa taifa hilo mwaka 1879 na Emperor wa wakati
huo William II ambao waliweka msingi wa ‘Kultur’. Kultur kwa lugha adhimu ya
Kiswahili ni utamaduni, Kultur iliingizwa katika akili za vijana na watoto wa
taifa hilo kwa hisia kubwa kiasi kwamba hakuwa mtu ambaye angeweza kulisaliti.
Mfumo wa Elimu uliwekwa uliifanya Ujerumani iwe imara na makini. Tukigeukia sera zetu za
michezo hususani riadha ni mfu hazina uhai wowote. Taifa linatamani wanamichezo
watakaofanya vizuri na kuipa sifa Tanzania.
Mchezo wa riadha ambao ni wa kwanza kuiletea medali ya
olimpiki Tanzania unapaswa kufunguka sasa kurudisha heshima yake, kwa uthubutu
usiokuwa wa kawaida. Ninapojaribu kutazama sioni juhudi za makusudi za miaka 20
ijayo katika riadha zaidi sana ni ni mambo ya zima moto yamekuwa yakitiliwa
mkazo, hivi kweli tutafika?
Kultur iliwasaidia wajerumani kuwa na uthubutu hata
kuushangaza ulimwengu. Mfumo wa elimu ya michezo ni mbovu nchini Tanzania ambao
hauwezi kutengeneza kizazi cha ushindani hivyo malalamiko, majungu, masengenyo,
unafiki havitakaa vimalizike katika riadha nchini zaidi sana ugomvi utaibuka
baina ya pande mbili.
Wadau wa riadha na Shirikisho la mchezo huo achaneni na fikra
kwamba mwanariadha ili afanikiwe lazima aende jeshini.
Tuwatengeneze wanariadha
ambao ajira yao itakuwa riadha badala ya kuwafikirisha akili zao kuwa ajira ipo
serikalini tu. Serikali haiwezi kuajiri wote lakini kwa wanariadha tuwasaidia
wakiwa na umri mdogo kuamini kuwa wanaweza kutoboa bila kwenda jeshini.
Pia ikumbukwe tukitengeneza mawazo hayo baada ya miongo
miwili au mitatu baadaye matunda yake yatakuwa makubwa mno. Uthubutu ndio dawa
pande zote kwa wadau, wanariadha, serikali na RT kuuponya mchezo huu.
Mwanafalsafa wa Ujerumani Immanuel Kant (1724-1804) aliibuka
na ufafanuzi wa binafsi wa "Falsafa ya mwangaza" akiulinganisha na
dhana ya bildung: "Kulingana naye, enzi ya nuru ni kule kutoka kwa
binadamu katika hali ya uchanga."
Alielezea ya kwamba hali ya uchanga
haitokani na kukosa kuelewa bali hutoka katika kukosa ujasiri wa kufikiria
huria.”
Thubutu inawezekana kuwa juu.
Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson. Kwa maoni au ushauri +255
768 096 793 au baruapepe: jaizmela2010@gmail.com
pia imetolewa katika gazeti la Tanzania Daima Aprili 22, 2019 uk. 12
|
Gazeti la Tanzania Daima Aprili 22, 2019 uk. 12 |