Mweneyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Sept 25, 2018 |
“Mwanzoni mwa mwaka 1990 waasisi wa chama hiki, mimi nikiwa ni mmoja wao na ndio nilikuwa mdogo kuliko wote, tuliona siasa za ujamaa ambazo ndiyo ilikuwa sera ya CCM, hazifai na haziwezi kuwapelekea maendeleo Watanzania.
Kwa pamoja tukaamua njia pekee ni kuanzisha vuguvugu la vyama vingi tukiamini kama serikali itakubali, basi tuanzishe chama cha siasa ambacho kitakuwa na sera mbadala ya ile ya ujamaa.
“Kwa hiyo mfumo wa vyama vingi ulikubaliwa, haraka tulisajili chama cha siasa cha CHADEMA na ilipofika mwaka 1993, mara tu ya kupata cheti cha usajili, tuliandaa Sera mbadala ya taifa ya mlengo wa kati ambayo ilikuwa inatofautia na ile ya ujamaa,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Hai, amesema baada ya kuiandaa sera ya chama chao, walimpelekea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye baada ya kuisoma aliikubali na kusema kuwa sera hiyo ndiyo hasa italeta maendeleo kwa Watanzania.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati kuu ya Chadema wakiwemo Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Wabunge wanaotokana na chama hicho, wageni waalikwa wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali na wananchi wa kawaida, Mbowe alisema baada ya miaka 25, chama chake kimeamua kuandaa tena sera mbadala ya taifa.
“Chama changu kimeamua kuandaa tena Sera hizi ambazo tumegusia Nyanja 12 ambazo tuna Imani zina tija kwa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla wake.
“Tumegusia Katiba, Utawala, Uchumi wa Soko Jamii, Siasa za ndani, Siasa za Kijamii na Afya. Lakini pia tumeangazia kwenye masuala ya Usimamizi wa ardhi, Kilimo, Miundombinu, Mazingira na mambo ya nje. Na hii sera yetu tunaiweka wazi kwa umma ili Watanzania wajue nini tunachokipigania kwenye hii nchi,” aliongeza Mbowe.
Baada ya kuzindua Sera hiyo, Mbowe amesema chama chake kimefungua rasmi milango ya kupokea maoni na ushauri juu ya sera hiyo kutoka kwenye vyama vya siasa, mashirika ya umma, taasisi mbalimbali na raia wa kawaida.
0 Comments:
Post a Comment