Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa imemteua Dkt.Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Dkt. Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo ambaye alijiuzulu.
Desemba 3, 2016, Nchimbi aliteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Balozi, baadaye alipangiwa kituo cha kazi Nchini Misri na kisha Agost 11, 2023 Rais Samia alimrejesha nyumbani. Leo Januari 15, 2024, Dkt. Nchimbi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akichukua nafasi ya Chongolo aliyejiuzulu nafasi hiyo.
WASIFU WA
DKT. EMMANUEL NCHIMBI
Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani
Mbeya, (atafikisha miaka 54 Desemba mwaka huu). Elimu yake ya Msingi aliianzia
jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 –
1986.
Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni
askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi
wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Mzee Nchimbi pia amewahi
kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la
majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa
mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.
Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya
Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia
Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.
Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya
masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM
Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).
Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.
Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo
Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka
2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya
uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.
MBIO ZA UBUNGE
Dkt. Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza
harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005,
aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa
Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa
wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.
Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu
kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira
na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008
kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi
Novemba 2010.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena
Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama
chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa
mwaka 2009.
Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa CHADEMA na
kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban
ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo,
alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.
Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi
Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba
2013.
0 Comments:
Post a Comment