Friday, January 26, 2024

Katja Keul kutoka Ujerumani kuhudhuria maadhimisho ya miaka 122 ya Mangi Meli Makindara

Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka nchini Ujerumani Katja Keul, kutoka nchini Ujerumani, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 122 ya shujaa wa Wachagga Mangi Meli Makindara, aliyeuawa kwa kunyongwa na Wakoloni wa Kijerumani Machi 2 mwaka 1900 na kisha fuvu la kichwa chake kuchululiwa na Wajurumani hao.

Mratibu wa Taasisi ya Utalii ya Old Moshi Cultural Tourism Gabriel Mzei Orio, ameyasema hayo jana, wakati akizungumza na Tanzania Leo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro kuhusiana na maadhimisho hayo, ambayo yatafanyika  MAchi 2, mwaka huu katika eneo la Kolila Wilaya ya Moshi mkoani humo.


“Machi 2, ya kila mwaka huwa ni kumbukizi ya kuwakumbuka viongozi wa kimila na wasaidizi wao waliouawa kwa kunyongwa akiwemo, shujaa wa jamii ya Wachagga Mangi Meli Makindara, aliyeuawa kwa kunyongwa na kukatwa kichwa chake  na wakoloni wa Kijerumani,”amesema Orio.


Amesema katika kumbukizi hiyo pia Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki anatarajiwa kuungana katika tukio hilo, machifu kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, ndugu, jamaa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Ujerumani na Tanzania watashiriki katika kumbukizi hiyo.


Aidha amesema kamati ya maandalizi kwa ajili ya kushughulikia tukio hilo inaendelea kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mkuu wa Mkoa, Umoja wa Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na familia za ndugu wa viongozi waliouawa.


“Katika tukio hili litatanguliwa na dua itakayofanyika katika mnara kilipolazwa kiwiliwili cha Mangi Meli Makindara na kufuatiwa na uwekaji wa mashada ya maua pamoja na salamu fupi kutoka kwa viongozi mbalimbali na wageni waalikwa.”


Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Machifu mkoa wa Kilimanjaro Joseph Mselle, amesema maadhimisho  ya kumbukizi hizo ni sehemu ya kuwaenzi viongozi na mashujaa 17 ambao walikuwa viongozi wa mila na desturi pamoja na wasaidizi wao waliuawa  kikatili wakati wakipambana kuwatetea wananchi wao.


“Mkoa wa Kilimanjaro tuna kila sababu ya kushiriki katika kumbukizi hizi kwa utulivu mkubwa kwa kuwaombea viongozi hawa ili yanayotokea ya kiimani anayetakiwa kusamehewa asamehewe huko aliko.”amesema Mselle.


Katika kipindi cha ukoloni, wakoloni walifanya mambo mengi, katika nchi walizokuwa wakizitawala, Ujerumani ni nchi mojawapo iliyokuwa na makoloni Barani Afrika, mpaka kushindwa vita vya kwanza vya dunia na pia ilishiriki katika maovu  hayo;


Mfano ni kuwanyonga viongozi na watu waliokuwa wakiwasaidia viongozi hao, na kukata vichwa vyao na kuvipeleka Ujerumani  kwa ajii ya kuvifanyia utafiti na ubaguzi wa rangi, suala hili liliwafanya watu wengi kuwa na mitazamo tofauti kuhusu Ujerumani mpaka leo hii.


Tukio lililofanywa na Wajerumani ukiacha tu kuwanyonga na kukata vichwa vyao, pia walikuwa wakichemsha maji ya moto na kuviweka vichwa hivyo kwenye maji ya moto na kuondoa zile nyama ili wapate lile fuvu, tukio ambalo lilikuwa la kikatili sana.




0 Comments:

Post a Comment