Friday, January 26, 2024

Wakandarasi watakiwa kuzingatia mikataba ya miradi ya Maendeleo


Wakandarasi wa miradi mbalimbali nchini wametakiwa kuzingatia mikataba waliyowekeana saini na serikali katika kuhakikisha miradi inamalizika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

 

Akizungumza katika hafla ya kushuhudia utilianaji saini mikataba ya upelekaji wa huduma za maji kwenye kata za Marangu Mashariki, Marangu Magharibi, Kibosho Kati na Kirima yenye jumla ya shilingi bilioni 2.76 Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori

 

“Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza nguvu kubwa sana katika kutoa huduma kwenye jamii ikiwamo barabara, maji, elimu na afya; Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama imepewa kipaumbele kikubwa sana,sisi tumekuwa tukipata fedha nyingi sana kwenye maeneo mengi kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Makori

 

“Kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 tumepokea bilioni 1.5 kwqa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa Ukaoni, Kibosho Kati na Kirua Vunjo Kusini; Kukamilika kwa mradi huu kutakwenda kupunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama na takribani watu 15,000 watanufaika,” aliongeza Makori.

 

Katika hafla hiyo wakandarasi walipata fursa ya kuzungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya Kisare Makori kuhusu namna watakavyotekeleza miradi waliyopata kwenye maeneo husika.

 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Miniac Construction Ltd Ramadhani Sangiwa amesema kamati za ulinzi na usalama ngazi ya vijiji na kata zitoe ushirikiano katika kulinda vifaa vya miradi.

 

Kwa upande wake Diwani wa Kibosho Kati Bahati Mamboma ambaye mradi wa maji utatekelezwa kwa manufaa ya wakazi 8,000 amesema kwa sasa maji hayatoshelezi wakazi hao hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaifanya kata yake kuondokana na changamoto hiyo. 


Kwa niaba ya madiwani wa halmashauri ya Moshi Vijijini Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Morris Makoi amewataka wakandarasi kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira katika maeneo ya mradi.

 

Katibu wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhani Mahanyu amewataka wakandarasi waishirikishe jamii ili kuondokana na sintofahamu ambayo mara kadhaa imefanya miradi baadhi isifanikiwe kama ilivyotakiwa

 

Maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya Moshi Vijijini ni asilimia 84.5 ambapo miradi hiyo itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji na kufikia asilimia 88 ifikapo Juni 2024.






0 Comments:

Post a Comment