Pandashuka za kesi ya Mirathi Na.5 ya mwaka 2002 zimesababisha mrithi wa Mirathi hiyo kupambana kupata haki yake kwa mwaka wa 20 sasa.
Mrithi wa Mirathi ya Marehemu Paul Kyauka Njau, Bi. Catherine Kyauka amejikuta katika sintofahamu ya kupata haki yake huku akitakiwa kuondoka katika nyumba anayoishi kwa kigezo kwamba sio mrithi halali wa Mali za marehemu.
Nyumba Na. 17/18 aliyopo Bi Catherine ipo mtaa wa Market (maarufu Market Street-Kiusa) mjini Moshi ambapo Oktoba 27, 2023 mbele ya Jaji Andrea Kilimi wa Mahakama Kuu, Wakili Msomi Stella Simkoko akiwa upande wa Bi. Catherine aliiomba mahakama isimtoe mwanamke huyo katika nyumba hiyo akirejea kesi mbalimbali mpaka shauri la msingi liwe limefungwa ndipo utaratibu mwingine uendelee.
Upande unaotaka Bi. Catherine aondolewe ukisimamia hukumu zilizotolewa mnamo mwaka 2010 na 2014 na Jaji Edward Rutakangwa, wamekuwa wakiishinikiza mahakama imwondoe mwanamke huyo licha ya Rufaa zake zote kushindwa.
Hata hivyo mwanamke huyo ameendelea kusimama kidete ambapo mnamo Desemba 12, mwaka 2023 aliwasilisha ombi dogo mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Moshi la kutaka asiondolewe katika nyumba anayoishi mpaka kesi ya msingi itakapofungwa.
Bi. Catherine akiwasilisha na Wakili Msomi Stella Simkoko aliiambia mahakama kesi ya msingi itakapofungwa ndio itafanya kila upande upate haki, hasa ikizingatiwa watoto wa mke wa pili na watatu wa marehemu hawakuhusishwa kwenye kikao cha kufanya uteuzi wa Mirathi ya marehemu Paul Kyauka Njau.
Ombi hilo mbele ya Mahakama Kuu Moshi limekuja wakati ambapo faili la kesi ya Mirathi Na. 5 ya mwaka 2002 la Marehemu Paul Kyauka Njau likiwa halionekani hatua ambayo inafanya kesi hiyo kushindwa kufikia maamuzi.
Upande wa wanaoshinikiza mahakama kutupilia mbali suala la mrithi wa Mirathi ya Marehemu Paul ambaye ni baba yake mzazi wa Bi. Catherine uliongozwa na Wakili Msomi D. Gadau ambaye aliiomba mahakama impe muda wa kuwasilisha vielelezo kwa njia ya mtandao.
Ombi la Wakili Msomi Gadau lilikubaliwa na pande zote ambapo Jaji Kilimi alitaja tarehe za kuwasilisha vielelezo na kabla ya Februari 26, 2024 ataendesha shauri hilo kwa njia ya mtandao.
Aidha Jaji Kilimi alitaka siku ya hukumu mnamo Februari 26,2024, upande wa wanaoshinikiza mahakama usimpe haki ya urithi Bi. Catherine uwepo mubashara ili kujiridhisha na baadhi ya masuala yanayoleta utata katika kesi hiyo.
Kesi hii Na. 5 ya mwaka 2002 imechukua muda mrefu takribani miongo miwili hivyo kuipa wakati mgumu mahakama kuamua nani anayestahili kuwa mrithi halali wa mali za marehemu Paul K. N
Kesi hiyo ilifunguliwa mnamo Oktoba 27, 2003 na kuendeshwa na Jaji Edward Rutakangwa wa Mahakama Kuu Moshi, ambaye ndiye aliyetoa hukumu ya kuwa baadhi ya warithi akiwamo Bi. Catherine wasiwemo katika nyumba Na. 17/18 'K' mnamo 2010 na 2014.
Marehemu Paul Kyauka Njau alifariki dunia mnamo Februari 17, 2002 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na kuzikwa Februari 23, 2002 kijijini kwake Ndima, Mrao-Mashati wilayani Rombo akiacha kiasi cha zaidi shilingi milioni 80 na mali kama magari, mitambo mbalimbà li, viwanja na nyumba vyenye wastani wa zaidi ya shilingi milioni 400.
Aidha katika Kikao cha ukoo wa marehemu kilichoketi Mnamo Juni 23, 2002 kikiwa na madhumuni ya uteuzi wa mfuatiliaji wa mirathi hiyo kilianisha watoto wa marehemu walio hao wakati huo kufikia 15 huku wengine saba wakipoteza maisha hivyo kufikia jumla ya watoto aliowazaa marehemu enzi za uhai wake kufikia 22.
Mke mkubwa ambaye ni Mjane wa marehemu Pauli K.N, mama Kresensia Pauli Kyauka alikataa kuwa mfuatiliaji wa mirathi hiyo mbele ya wajumbe 49 waliohudhuria kikao hicho cha ukoo kwa kutaja sababu za yeye kuwa mzee na ugonjwa hivyo mtoto mkubwa Febronia Pauli Kyauka na mwingine aliyefahamika kwa jina la Emmanoel Pauli Kyauka Njau walipendekezwa kufuatilia.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa marehemu alizaa watoto 22 kutoka kwa wake watatu ambao ni Kresensia P.K.N, Kristina na Pulkeria P.K.N ambapo katika ufuatiliaji wa mirathi baadaye Febronia alifariki Dunia na jukumu lote kusalia kwa Emmanoel.
Mke mdogo wa tatu ambaye ni Pulkeria alifanikiwa kuzaa na marehemu Pauli watoto saba akiwamo Catherine ambae amejitosa kutaka haki itendeke kwa watoto wote wa marehemu na sio upande mmoja pekee.
Mnamo Desemba 12, 2023 wakati Jaji Kilimi wa Mahakama Kuu ya Moshi alitaka wakati wa uwasilishaji wa vielelezo vya ombi lao kwa njia ya mtandao, alitaka wahusika akiwa Emmanoel P.K.N wawepo na awaone mubashara kupitia intaneti kwa kuwa mnamo Januari kabla ya kufikia maamuzi mnamo Februari 26 ataendesha kwa njia ya mtandao.
Marehemu Pauli Kyauka Njau aliacha mali zinazokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 400 ambazo zimekuwa na sintofahamu nyingi kwa muda mrefu sasa, hivyo kuipa ugumu mahakama kufikia mwafaka wa shauri hilo
0 Comments:
Post a Comment