Wakazi wa Manispaa ya Moshi wanaendelea kupambanana changamoto ya bei ya sukari ambapo hadi sasa kilogramu imekuwa ikiuzwa kati ya shilingi 3,000 hadi 5,000.
Hatua hiyo imewafanya baadhi ya wakazi
wa manispaa hiyo kutafuta njia mbadala ya namna ya kuipata sukari kwa ajili ya
matumizi ya familia zao.
Wakizungumza na gazeti hilo wakazi hao
wamesema bei ya sukari ipo juu hatua ambayo imekuwa ikiathiri familia zao
ambazo zilizoea kuitumia sukari katika chai au uji kwa ajili ya watoto
wanaosoma shule.
“kilo ya sukari ilikuwa inauzwa Sh 3,000 hadi 3,200, lakini kwa
sasa unapokwenda unauziwa Sh 4,500 hadi 5,000, hivyo hakuna bein elekezi ambayo
unaweza kuipata sukari,” alisema Gadson Sadick Mdee, mkazi wa Majengo, Moshi.
Aidha mkazi huyo aliwanyooshea kidole
cha lawama wafanyabiashara wanaokiuka taratibu za serikali ambapo imeweka bei
elekezi ya bidhaa hiyo.
“Changamoto ya sukari imekuwa ni kubwa kwa wakazi wa moshi,
unakuta bei elekezi ya serikali ni tofauti na pale unapokwenda madukani
kununua. Kama ulizoea kununua sukari kwa mteja wa duka ambaye umemzoea ,
unapokwenda kununua na kumkuta hana bidhaa hiyo, unapoenda sehemu nyingine
unauziwa kwa bei ya kulanguliwa na si kwa bei ambayo tumekuwa tumeizoea,”
aliongeza
Mdee.
Hata hivyo kuwafanya watoto wao
waridhike na kifungua kinywa wamekuwa wakinunua muwa kisha kuukamua na kuongeza
maji kidogo na majani yanachanganywa ili kutengeneza chai.
“Tumelazimika kutafuta njia mbadala
kwa ajili ya kuwafanya watoto wetu waridhike waweze kwenda shuleni. Tumekuwa
tukinunua muwa tunaukamua tunachanganya maji na majani ya chai kidogo
unamdanganyia mtoto anakunywa anakwenda shuleni.
Saimon Msumari, mkazi wa Kata ya
Mawenzi katika Manispaa ya Moshi alisema miwa hiyo wamekuwa wakiipata kutoka
wilayani Mwanga, Hai na Moshi Vijijini
na imekuwa rahisi kuliko kununua sukari kilogram moja.
“Tumerudi kule kwenye miaka ya 70 hadi 80 tuliwahi kutumia miwa
na kwa sasa miwa na yenyewe imepanda bei, tunaitumia tunaikamua ili mtoto
asubuhi aweze kupata chai. Miwa kwa sasa hivi imepanda bei kutoka Sh
1,000 hadi 1,500,” alisema Msumari
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjaro Nurdin Babu aliwataka wafanyabiashara kuacha mara moja mchezo wa
kuficha sukari na kisha kuipandisha kinyemela
“Sukari ipo na sisi kama serikali ya mkoa tukimkamata
mfanyabiashara yeyote ameficha sukari, tutachukua sukari yake, huwezi kuwaonea
wananchi. Tutapita kwenye maduka kukagua wanaojipangia bei yao na kuwaumiza
wananchi. Wafanyabiashara msitake kugombana na serikali kwa sababu ya sukari,”
alisema Babu.
0 Comments:
Post a Comment