Wednesday, July 5, 2023

Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa KCMC auawa.

KHUDHEIFA CHANGA (26), ENZI ZA UHAI WAKE

Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Muuguzi wa hospitali ya KCMC Moshi.

Wamekamatwa watuhumiwa watatu wanaume na wanawake wawili (majina yao yamehifadhiwa kwa sababu wengine wanaendelea kutafutwa) kwa tuhuma za kusababisha mauaji ya mwanaume mmoja aitwaye Khudheifa Changa, (26), Muuguzi katika Hospitali ya rufaa KCMC Moshi huko mtaa wa Malindi, kata ya Mawenzi, wilaya ya Moshi Manispaa usiku wa kuamkia Julai 2, 2023.

Inadaiwa siku ya tukio hilo marehemu alikuwa akipita eneo hilo kwenye njia ya uchochoro ndipo alivamiwa na watu hao kwa nia ya kumpora mali alizonazo.

Katika purukushani hizo marehemu alijeruhiwa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye mbavu upande wa kushoto usawa wa moyo na kupelekea kifo chake papo hapo.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Raia wema lilifanikiwa kupata taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao walitoweka baada ya kutenda unyama huo.

Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Rufaa KCMC Moshi kwa uchunguzi zaidi.

0 Comments:

Post a Comment