Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, Dkt. Leonard Subi, amesema hatua ya utoaji wa huduma za matibabu kupitia hospitali hiyo katika ngazi za serikali za mitaa, imesaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza mapambano dhidi ya kifua kikuu sugu nchini.
Akizungumza wakati akipokea ugeni wa makatibu wakuu barani Afrika hususani zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu zipatazo 12, Dkt. Subi amesema teknolojia ya masafa ambayo huwawezesha kuwafikia wagonjwa wa kifua kikuu sugu wakiwa mbali imekuwa silaha kubwa kudhibiti maradhi hayo.
“Tumegatua utoaji wa huduma za matibabu katika ngazi za serikali za mitaa, sasa hospitali yetu ya Kibong’oto imekuwa ikitoa mafunzo lakini pia tunajadiliana wenzetu waliopo katika mamlaka zinazohusika za mitaa katika matibabu ya wagonjwa; kwa mwaka 2022 tuliweza kuwahudumia wagonjwa 42 kwa njia ya teknolojia ya masafa, kwa maana tunatoa huduma wakiwa kule mbali,” amesema Dkt. Subi.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Anna Chongolo, amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wa kifua kikuu wa aina tofauti wakiwemo wale ambao wameathirika baada ya kupona kifua kikuu, sambamba na walioathirika na vumbi la mgodi ambao wengi wao wamekuwa wakikohoa damu.
“Mara zote tumekuwa tukipima mapafu ufanyaji kazi wake, tunaangalia uwezo wa pafu kufanya kazi tukiona kwamba kuna mapungufu tunaendelea klufanya counseling kwa mgonjwa kwani tutakuwa tukimfuatilia mara kwa mara,” amesema Dkt. Chongolo.
Kwa upande wake Mkuu wa kifua kikuu kutoka Global Fund, Dkt. Eliud Wandwalo, ameipongeza Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, kwa kuwa na mpango wa kuwafuatilia wagonjwa wa kifua kikuu waliopona ili kujua maendeleo ya hali zao tofauti na nchi zingine.
Aidha amesema ugonjwa wa kifua kikuu unaua watu wengi zaidi duniani hasa nchi maskini ambazo zina watu wengi, ambapo kila mwaka watu zaidi ya milioni 1.6 wanakufa kutokana na kifua kikuu ambayo ni sawa na wagonjwa 4,000 kwa siku hufariki dunia.
“Mgonjwa mmoja asipogundulika na
kifua kikuu kwa muda wa mwaka mmoja anaambukiza wengine 15 mpaka 20,” amesema
Dkt. Wandwalo.
Ugeni huo uliambatana na mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani
(WHO), madaktari bingwa kutoka India, na wawakilishi kutoka Mfuko wa Kudhibiti
Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund).
Taarifa hii imetayarishwa na Kija Elias na Jabir Johnson, Julai 6, 2023
0 Comments:
Post a Comment