MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi
Zubery Abdallah Kidumo, amelazimika kumtoa nje ya kikao cha Baraza la Madiwani,
diwani wa kata ya Mjimpya Abuu Shayo, kwa kile kilichoelezwa ni kutaka kuvuruga
kikao cha baraza hilo.
Kisa cha diwani Abuu kuondolewa kwenye kikao hicho cha Jumatano
Julai 26, kimetokana na yeye kutaka hoja zake zilizojadiliwa kwenye vikao vya
Kamati kujadiliwa kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani kilichokuwa
kinathibitisha mihutasari ya vikao vya kamati za madiwani na watendaji.
Akitolea ufafanuzi hatua hiyo Mwanasheria wa Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi Wakili Msomi Sifaeli Koyanga, amesema uamuzi huo
ulilenga kuondoa mvutano baada ya diwani Abuu Shayo kushindwa kutafsiri kanuni
aliyotumia kutaka hoja yake kujadiliwa kwenye kikao hicho.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo Mhandisi Zubery Abdallah
Kidumo, amesema uamuzi wake umetokana na mjumbe huyo wa Baraza la madiwani
kupingana na ufafanuzi wa kanuni uliotolewa na mwanasheria wa halmashauri ya
manispaa hiyo.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa ukuta kuzunguka majengo ya halmashauri
hiyo, yaliyotolewa na diwani Abuu, meya ametolea ufafanuzi wa fedha
zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo.
Katika hoja zake diwani wa kata ya Mjimpya Abuu Shayo ambaye pia
ni mjumbe wa kamati ya mipango miji amekuwa akihoji gharama za ujenzi wa ukuta
katika eneo la ofisi za halmashauri utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni
920, pamoja na mradi wa ujenzi wa shule ya msingi kwenye kata yake.
0 Comments:
Post a Comment