Waziri wa Maliasili na Utalii Mohammed Mchengerwa amewahakikishia wananchi wa wilaya Same mkoani Kilimanjaro tembo wote wanaozurura nje ya hifadhi ya Wanyamapori Mkomazi wataanza kurudishwa tena hifadhini humo.
Akizungumza
na wakazi wa kata ya Kalimawe wilayani
Same; Mchengerwa amesema zoezi hilo linakuja kutokana na idadi kubwa ya tembo
kuongezeka katika hifadhi.
“Tembo wote
tunawaondoa na kuwarudisha ndani ya hifadhi, tutahakikisha tunatatua kero zote
zinazowahusu wananchi hasa wananchi wa Same, kama kulikuwa na tembo wanazurura
hovyo hovyo nimekwishatoa maelekezo tembo wote warudi ndani ya hifadhi. Na ninaomba
niwadhibitishie kama miongoni mwetu walikuwa wanakata tamaa huu ni wakati wa
kujenga matumaini,” amesema Mchengerwa.
Aidha
Mchengerwa amesema baada ya zoezi hilo kukamilika serikali itaanza kuwalipa
fidia waathirika wa uvamizi wa tembo.
“Mbali na
hilo kuna wananchi wanadai fidia mazao yao yameliwa, kuna wananchi wamepoteza
maisha niwaambie serikali yenu inawapenda sana wananchi wa Same, inawapenda
sana watanzania; Tanzania ndiyo nchi pekee Afrika ambayo tunalipa fedha za
fidia, hauikuti Kenya, huikuti Uganda, huikuti sijui wapi; ni Tanzania pekee…fedha
ninayo, fedha ipo na niwathibitishie wananchi wa Same tutajitahidi wiki ijayo
walipwe fidia, tutajitahidi, “amesisitiza Waziri huyo wa Maliasili na Utalii.
Hata hivyo
Mchengerwa amewataka wale waliopata nafasi ya kuitimikia nchi hii katika nafasi
mbalimbali kufanya kazi kwa bidii.
“Yeyote aliyepata
nafasi ya kufanya kazi afanye kazi kwa bidii; watanzania wanatutegemea na sisi
tumepata nafasi hizi ni lazima tuwatumikie tufanye kazi hasa ili kila mmoja
wenu awe na furaha na serikali,” amesema Mchengerwa.
Zoezi la
kuwarudisha tembo katika hifadhi ya Mkomazi limeanza Julai 7 mwaka huu ambapo Hifadhi
za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na taasisi nyingine za uhifadhi wa
Wanyamapori zipo wilayani Same kuhakikisha tembo hao wanarudi hifadhini.
0 Comments:
Post a Comment