Friday, August 30, 2019
MAKTABA YA JAIZMELA: Warren Buffett ni nani?
Agosti 30, 1930 Alizaliwa mwekezaji bilionea Warren
Buffet, Omaha Nebraska nchini Marekani.
Katika kitabu cha “The Warren Buffet Way” kutoka kwa
mwandishi Robert G. Hagstrom kinaelezea maisha ya bilionea Warren Buffett. Mwandishi
anatumia kitabu hiki kushirikisha jamii mbinu ambazo mwekezaji bilionea Warren
Buffet amekuwa akizitumia kukuza utajiri wake. Bilionea huyu ni mwekezaji
ambaye amewahi kuwa tajiri namba moja wa dunia kwa kipindi kirefu na amekuwa
kati ya matajiri watano wanaoongoza kwa muda sasa.
Warren Buffet amekuwa tajiri kupitia uwekezaji katika
kampuni yake ya Berkshire Hathaway ambayo inajihusisha na uwekezaji kwenye
biashara tofauti. Kwa ufupi Warren Buffet amekuwa ni mtu ambaye anachukua hatua
mapema kama tahadhari dhidi ya nyakati zinazokuja na hivyo nyakati hizo (mbaya
au nzuri) zinapowadia zinamkuta ameshajiandaa kiuwekezaji.
Alianza kupenda kilichomleta hapa duniani akiwa na
umri wa miaka sita . Akiwa na umri wa miaka sita, alinunua paketi sita za Coca
Cola kutoka dukani kwa babu yake na kwenda kuziuza ampapo alipata faida ya
senti 5 kila paketi.
Akiwa na umri wa miaka 11 alikuwa tayari amenunua
hisa, wakati huo watoto wenzie walikuwa wakiruka kamba, si jambo baya lakini
hata yeye alikuwa akiruka, yaani kucheza, lakini alichokuwa akikiona siyo fedha,
bali biashara. Suala la elimu kwake lilikuwa siyo la kipaumbele sana.
Mwaka 1947, akiwa na umri wa miaka 17, Buffet
alimaliza kidato cha sita. Hakutaka kuendelea na masomo ya chuo, ingawa alikuwa
na uwezo wa kufanya hivyo. Tayari wakati huo alikuwa na fedha kiasi kama
milioni 40, kiwango cha sasa cha Tanzania.
Hata hivyo Buffet alisoma na kumaliza elimu ya chuo
kikuu. Sehemu kubwa baba yake ndiye aliyemshawishi hasa kusoma masuala ya
biashara.
Akiwa na miaka 14 aliweza kununua shamba kutokana na
kuweka akiba ya kugawa magazeti.
Wakati hajagundulika na kujulikana kuwa yeye ni tajiri,
Warren Buffet hakujenga nyumba ya ghorofa ili watu wamjue yeye ni nani.
Alikuwa anaishi kwenye nyumba ndogo ya kawaida ya
vyumba vitatu- Omaha. Ndani ya nyumba yake hiyo kuna kila kitu anachokihitaji yaani
jiko, kitanda, meza, bafu, viti vya kukalia na television
Nyumba yake hiyo haikuwa na uzio. Huyu mzee hakuwa na dereva wala mlinzi. Alikuwa
anaendesha mwenyewe na likiharibika, anaingia uvunguni mwenyewe kulitengeneza
mwenyewe.
Warren Buffet haamini kuwa kuna bilionea duniani, bali
anaamini kuwa kuna watu wanaotafuta ndoto zao ili zitimie.
Mfanyabiashara huyu wa Marekani anajulikana hasa kwa
ajili ya falsafa yake ya ukarimu.
Tuesday, August 27, 2019
MAKTABA YA JAIZMELA: Lyndon B. Johnson ni nani?
Lyndon B. Johnson
alichaguliwa kuwa makamu wa Rais wa 37 wa Marekani mwaka 1960 na alikuja kuwa
Rais wa 36 taifa hilo mwaka 1963 baada ya kuuawa kwa Rais John Fitzgerald
Kennedy.
Lyndon Johnson alikuwa akifahamika na wananchi wake kama LB . Akiwa
kama Rais wa taifa hilo aliidhinisha Sheria ya Haki za Kiraia ya mwaka 1964 na
Sheria ya Kupiga Kura ya mwaka 1965. Pia LB alishinikiza kumalizika kwa Vita
vya Vietnam na ushiriki wa Marekani katika vita hivyo. Kabla ya kufa kwake kwa
Mshtuko wa Moyo Januari 22, 1973 siku moja kabla LB alikaririwa akisema anaona
amani inapatikana Vietnam. Alifariki akiwa na miaka 64. Lyndon alizaliwa
Stonewall, Texas Agosti 27, 1908 kutoka kwa wazazi Samuel Ealy Johnson Jr na
Rebekah Baines akiwa mtoto wa kwanza kati ya watano ambao walifanikiwa kuwa
nao. Familia yao ilikuwa ikijulikana kwa kilimo na ufugaji jimboni Texas. Baba yake alikuwa miongoni mwa
wajumbe wa Congress huko Texas akionyesha siasa safi kuliko hata
ufugaji licha ya kwamba alishawahi kupoteza shamba la familia wakati
Lyndon alipokuwa bado mdogo. Aliingia kwenye siasa baada ya Richard M. Kleberg
kushinda uchaguzi mwaka 1931 kuiwakilisha Texas katika Bunge la Wawakilishi.
Hivyo Kleberg Jr. aliamua kumteua LB kuwa katibu wake. LB alipata nafasi hiyo
baada ya ombi la baba yake na Seneta Welly Hopkins kwani alikuwa akimpigia kampeni
mwaka 1930. Mnamo mwaka 1948 Lyndon alishinda uchaguzi wa Bunge la Seneti na
mwaka 1951 alichaguliwa kushika wadhifa kuwa msemaji wa bunge hilo kwa watu.
Alizidi kupaa katika siasa kutokana na kujituma na hoja zenye msingi kwa tiketi
ya chama cha Demokrati. Mnamo mwaka 1960 aliwania uchaguzi wa urais ambao
hakufanikiwa kupita. Licha ya kushindwa kupata nafasi ya kuchaguliwa John F.
Kennedy alimwita awe makamu wake wakati wa kampeni. Wakati huo JKF alikuwa
seneta wa Massachussets. Hivyo wawili hao wakafanikiwa kuwashinda wa upande wa
Republican Richard Nixon na mwenzake Henry Cabot Lodge Jr. Novemba 22, 1963 JFK
aliuawa na LB akashika wadhifa huo kama Rais. LB aliapishwa ndani ya ndege Air
Force One baada ya kuuawa kwa JFK. Mwaka uliofuata LB alifanikiwa kumwangusha
seneta wa Arizona Barry Goldwater. Lyndon Johnson aliibuka mshindi kwa asilimia
61.1, kiwango amcho kinachukuliwa kuwa ni cha juu tangu uchaguzi wa mwaka 1820
ambao ulimweka madarakani James Monroe aliyeibuka mshindi kwa asilimia 80.6
dhidi ya chama cha Federalist.
Johnson anakumbukwa kwa mafanikio yake yote ya
kisheria na kutawala kwa makundi. Mnamo 1980, alipewa tuzo ya heshima ya Jimmy
Carter na Medali ya Rais ya Uhuru.
Monday, August 26, 2019
Asante Mama wa Kambo
Shamrashamra
zilizidi kurindima kwa fujo katika ukumbi maarufu sana wa Wikechi mjini
Makambako, hakika maharusi walikuwa wamependeza na utakuwa mchoyo wa kuzaliwa
usingewapongeza waliotumia ubunifu wa hali ya juu kuupamba ukumbi ule nao
ukapambika.
Kila
mmoja alitabasamu bila kujalisha linatoka moyoni ama ni la kuzugia!!
Wanawake
walipiga vigelegele na wanaume walipiga mbinja kila muda ambapo msema chochote
aliamuru!!
Naam!!
Ilikuwa sherehe ya aina yake ya kuwaunganisha Gladness na Jackson kuwa mwili
mmoja!!!
Jack
ambavyo wengi tulizoea kumwita alikuwa mwenye furaha sana alipopewa nafasai ya
kusema chochote, alizishukuru pande mbili akianza na ule upande wa ukweni
akawashukuru kwa zawadi ya mke mwema…..kisha akageukia upande wa pili na
kuwashukuru wazazi wake waliomkuza na kumpa elimu dunia pamoja na ile ya
darasani!!!
Hatimaye
msema chochote akamkabidhi kipaza sauti Glad!!
Ukumbi
mzima ulitambua kuwa Maria hakuwa akitabasamu kutoka moyoni lakini bado hakuna
aliyejua kwanini alikuwa katika hali ile.
Maria
akashika kipaza sauti mbele ya umati na kuanza kuzungumza.
“Imekuwa
safari ndefu sana hadi kuifikia siku hii ya leo…nikimtoa mwenyezi Mungu katika
safari hii ninaye mtu mwingine muhimu katika dunia hii wa kumshukuru!! Ni mtu
mmoja tu nasisitiza pasipokuwa na unafiki wowote!!
Namshukuru
mama yangu…mama yangu wa Kambo” akasita kidogo ukumbi nao ukawa kimya!! Kimya
kikuu…Glad akaendelea.
“Asante
sana mama wa kambo kwa matusi yote uliyonitukana maana ulinifanya niyazoee,
awali nilikuwa nakasirika sana ukunitukana, ukimtukana marehemu mama yangu,
ukinitukania baba yangu. Naam ukaniimarisha zaidi hata nilipokuwa nafanya kazi
za ndani sikuhangaishwa na matusi kutoka kwa watoto wa bosi wangu!!
Niliyapuuzia tu!!!
Asante
kwa kunilaza nje asante sana kwa jambo lile, nikalizoea giza, mbu wakaizoea
damu yangu!! Ukaniimarisha na hata nilipokosa pa kulala nikiwa mtaani stendi
ilikuwa sehemu sahihi kwangu na nililala bila hofu. Mama wa kambo siwezi
kusahau kukushukuru kwa kunilisha chakula ambacho watoto wako walilalamika kuwa
ni kibaya ama kimeharibika.
Ulikuwa sahihi mama maana hata kule majalalani
sikuhangaika tena kila kinachoitwa chakula mimi nilikula. Unadhani ungenidekeza
ningeweza vipi?
Siku
uliyoamua rasmi kunifukuza ukinizushia kuwa nakujazia choo na kukumalizia
godoro bila sababu za msingi ni hivyo hivyo niliwahi kufukuzwa na mabwana wengi
walaghai. Lakini sauti zao na yako zilifanana hivyo sikuogopa chochote kitu!!
Nikabaki kuwa imara huku nikihesabu kuwa haya ni mapito tu!!
Kulala
bila kula kwa siku mbili hadi tatu katika nyumba yako lilikuwa jambo la kawaida
sana hivyo niliweza kumvumilia Jack wangu alipokuwa hana pesa. Alinishangaa
sana kwa uvumilivu wangu lakini leo atambue kuwa bila wewe nisingeweza
kumvumilia.
Ulininyima
elimu mama wa kambo!! Vyema sana ukanifanya niishi kwa kutumia nguvu zangu tu
na akili ya ziada lakini si vyeti!! Sikuwa mtu wa kuchagua kazi, nilibeba
kokoto, nikafanya ubaamedi, nikafua nguo za watu, nikafagia barabara na kazi
zote zile ambazo zilihitaji watu kama mimi nisiyekuwa na elimu!! Asante mama wa
kambo!!!
Sijaisahau
ile siku uliyonimwagia maji ya moto na kuondoka na ngozi yangu usoni, tazama
ulinisaidia sana hakika, wanaume hawakunitamani!! Ndio…nani wa kumtamani na
kumthamini mwanamke asiyekuwa na mvuto.
Ulifanya
la maana sana mama maana maumivu niliyoyapata kuondokewa na wazazi wangu,
maumivu niliyoyapata kwa mateso yako, ni heri hayo yalitosha na ukaniepushia
maumivu ya kudanganywa na wanaume wakware kisa uzuri wangu kisha wanitelekeze
pasi na msaada. Ni heri waliidharau na kuichukia sura yangu hadi nilipokutana
na Jack. Hakujali sura akayajali maumivu yangu na akaamua kunipooza!!!
Hata
lile kovu uliloniachia kwa kunichoma na mkaa wa moto pajani, yeye hakujali pia.
Unadhani ni wanaume wangapi wanaweza kuwa na ujasiri wa Jack??
Nasema
nawe ewe mama uliyevaa nguo nyeupe pee!! Umeketi katika kiti cha tatu kutoka
kushoto, mama usiyekuwa na haya uliyenitukana huku ukisema kamwe kuwa
sitaolewa!!
Nimezisikia tetesi kuwa wale wanao wawili wa kike uliowabatiza cheo
cha umalikia walijazwa mimba na kuzaliwa nyumbani, sijui kama ni kweli kuwa
yule mwanao wa kiume alinibaka ukanitusi mimi kuwa namfunza tabia mbaya nasikia
na yeye ni teja na kila leo anakuibia vitu nyumbani!!
Natoa
shukrani kwako kwa mabaya yote uliyonitendea, natoa shukrani kwako kwa moyo
wako mgumu unaodhani kuwa niliyasahau yale yote na leo hii umeketi upande wa
ukoo wangu ukisubiri kunipa zawadi ya kunipongeza kwa sababu nimeolewa.
U
mnafiki ewe mama, u mkatili katika maana halisi ya kuitwa mkatili.
Nayasema
haya ili niwe na amani, nayasema haya bila unafiki wala tabasamu bandia la
kuigiza!!! Nilijua itafika siku ya kusema nd’o maana sikusema katika siku hizi
zote.
Ewe
mama wa kambo umenipa zawadi nyingi sana tena za kudunu, siihitaji zawadi yako
siku hii ya leo. Sihitaji chochote kitu katika maisha yangu kutoka kwako!!
Umenipa vingi na vinatosha sana!!!
Asante
sana mama wa kambo!! Mama mbaya unayesababisha hata wale mama wa kambo wenye
utu waonekane kuwa si lolote na si chochote kitu!!!”
Glad
alimaliza kuzungumza huku machozi yakiondoka na nuru yake asiweze kuona mbele
tena.
Mama
yule ambaye ukumbi mzima ulikuwa ukimtazama alibaki akiwa ameinama. Watu
walingoja sana anyanyuke waweze kuibaini walau sura yake. Lakini hakunyanyuka,
aliyeamua kumgusa bega mara kadhaa kwa kumsukuma ndo aliihitimisha safari yake
sakafuni. Mama yule hakuwa na fahamu zake!!!
Zikafuata
hekaheka za kumpepea lakini fahamu hazikurejea.
Glad
naye alifanya harakati hizo huku akiipuzia shela aliyokuwa ametinga. Hali
ilikuwa tete na ukumbi wa sherehe ukageuka kuwa ukumbi wa hekaheka!!
Wakati
mama yule anakimbizwa hospitali, Maria alipata fursa ya kukwapua bahasha ambayo
awali ilikuwa mikononi mwa mama wa kambo kabla hajaanguka!!
Akaifungua
na kukutana na kipande cha karatasi.
“Sina
zawadi yoyote ya kukupa Glad, japo ni wewe wa kunipa mimi zawadi kubwa ya
msamaha. Hakuna nikitegemeacho tena duniani zaidi ya msamaha wako!! Siwezi
kujieleza nikaeleweka kwa yote yaliyotokea miaka hiyo lakini waweza kunielewa!
Ninauhitaji msamaha wako kabla sijafa Glad.
CREDITED: Simulizi
hii fupi ya ‘Asante Mama wa Kambo’ ilitungwa na George Iron Mosenya, mwaka 2013.
JAIZMELA imeihariri kidogo kutoka kwa mtunzi ili kuleta maana iliyokusudiwa.
MAKTABA YA JAIZMELA: Edward Lowassa ni nani?
Edward Ngoyayi Lowassa ni
mwanasiasa nchini Tanzania. Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa 10 wa Tanzania Desemba 30, 2005 na akajiuzulu Februari 7, 2008
kwa kashifa ya Richmond.
Mwaka 2015 alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Alizaliwa Monduli mkoani Arusha Agosti 26,
1953. Alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, halafu shahada ya pili katika Sayansi ya Maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu
cha Hull nchini Uingereza.
Lowassa ni mwanasiasa mkongwe mwenye uzoefu
mbalimbali katika siasa za nchini Tanzania, kwa kuwa aliwahi kushika vyeo mbalimbali
katika serikali kama vile Waziri mdogo wa Mazingira na Mapambano dhidi ya Umaskini
katika ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000), Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano (1989-1990) na Waziri Mdogo wa Haki na Mambo ya Bunge katika Ofisi
ya Makamu wa Rais (1990-1993). Alikuwa mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990.
Mwaka
1995 Edward Lowassa aliamua kuingia katika mchakato wa kumpata mgombea urais
kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wakati huo Lowassa aliombwa na Umoja
wa Vijana kupitia kikao cha baraza kuu la Taifa achukue fomu akiwa miongoni mwa
wana CCM wanne ambao vijana waliamini wataweza kulisaidia Taifa kupiga hatua za
haraka kuelekea maendeleo endelevu, wengine waliokuwa wametajwa na Umoja wa vijana
ni Salim Ahmed Salim, Laurence Gama na Jaji mstaafu Mark Bomani. Katika hatua
ya kuchagua majina 3 kati ya majina 11 yaliyoomba nafasi hiyo, Lowassa akawa
hakupendekezwa. Vijana wa CCM walihoji kwa nini ameenguliwa, na yeye kwa utii
mkubwa kwa CCM aliwataka vijana na viongozi wengine waheshimu maamuzi ya chama
na kumuunga mkono atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya chama. Ikumbukwe kuwa
mwana-CCM mwingine aliyekuwa anakubalika kwa umma Augustino Lyatonga Mrema
aliondoka mapema CCM kwa sababu ndogo tu ya kubadilishiwa wizara na kuamua
kwenda chama cha NCCR Mageuzi ambako aligombea uraisi kwa chama hicho na kuleta
upinzani mkubwa. Yapo maneno ya baadhi ya wanasiasa kwamba kutoteuliwa kugombea
kwa Lowassa kulitokana na kuonekana anamiliki fedha nyingi akiwa na muda mfupi
kwenye utumishi wa umma, lakini pia inasemekana kuwa wale waliohoji kukatwa kwa
jina lake kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa, majibu yalikuwa, CCM
iliamua kupeleka majina matatu kwenye mkutano mkuu ili wachague moja katika
uwakilishi huo wa majina: walipenda apatikane mtu mzima mmoja, mwenye umri wa
kati mmoja na kijana mmoja, watu hao ni mzee David Msuya ambae ni mtu mzima,
Benjamini Mkapa ambae umri wake ulikuwa wa kati na kijana ambae ni Jakaya
Kikwete. Lakini maneno hayo ya baadhi ya wanasiasa hayakuishia hapo: wakadai
baada ya Rais Mkapa kuchaguliwa, hakumteua Lowassa kwa kuwa aliagizwa na
Mwalimu Nyerere asimteue mpaka achunguzwe kama uwezo kiasi wa fedha alionao
unatokana na mapato halali, kama siyo halali asimteue. Mwaka 1997 Rais Mkapa
akamteua Lowassa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais mazingira.
Februari
7, 2008 Lowassa alijiuzulu baada ya kushtakiwa kuwa ameshiriki katika kashfa ya
Richmond. Kamati ya bunge iliwahi kuchungulia mkataba baina ya kampuni ya
TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC kutoka Houston, Texas.
Kamati ya wabunge watano chini ya mwenyekiti Dkt. Harrison Mwakyembe ikaona
mkataba huu ilikuwa kidanganyifu. Richmond ilipewa kazi ya kutengeneza megawati
100 za umeme kila siku baada ya ukame wa mwaka 2006 uliopunguza uwezo wa TANESCO
kutoa umeme nchini kutokana na mitambo yake ya umememaji. Lakini mitambo ya
dharura ya Richmond ilichelewa kufika nchini pia haikufanya kazi jinsi
ilivyotakiwa. Hata hivyo serikali ikaendelea kulipa zaidi ya dolar za Marekani
100,000 kila siku.
Mwaka 2014 Lowassa alisimamishwa na kamati kuu ya CCM baada
ya kushtakiwa ya kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais
kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hiki.
Lowassa aliondoka katika CCM na
Julai 28, 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA. Lowassa alikaririwa
akisema,“Nitakuwa mnafiki nikisema bado nina imani na CCM.'' Pia mwanasiasa
huyo alisema, ''CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia” na kuongeza “Kama Watanzania
hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM.”
Siku chache
baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) alishindwa kwa
kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM John Pombe Magufuli alipata
58.46 Lowassa aliendelea kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.
Mwaka 2016
alitangaza ya kwamba hawezi kurudi kamwe CCM. Mnamo Januari 2018 aliwahi kuwa
na mazungumzo marefu na Rais Magufuli. Machi 1, 2019 Lowassa alirudi kwenye
chama chake cha awali Chama Cha Mapinduzi.
Friday, August 23, 2019
Alexei Navalny, mkosoaji mkuu wa Putin aachiwa
Mkosoaji wa serikali ya
Urusi, Alexei Navalny ameachiwa huru leo baada ya kutumikia kifungo cha siku 30
jela kwa kupanga maandamano ya upinzani, ambayo yamegeuka kuwa vuguvugu ambalo
limeitikisa serikali ya Urusi tangu mwezi uliopita.
Polisi walikuwa nje ya
gereza wakati akiachiwa huru lakini hawakuchukua hatua yoyote ya kumkamata
tena, kama walivyofanya wakati viongozi wengine wa upinzani walipoachiwa huru
hvii karibuni. Lakini Navalny ameendelea kuwataka wafuasi wake kuingia mitaani,
kitu kinachoweza kuwafanya polisi wamkamate tena.
Mara baada ya kutoka jea,
kiongozi huyo wa upinzani na mwanarakati wa kupinga rushwa mara moja alilaani
kile alichosema kuwa ni vitendo vya kigaidi vilivyofanywa na serikali ya Urusi
katika kuyazima maandamano mjini Moscow katika wiki za hivi karibuni.
CHANZO: DW
UWT yafagilia uwekezaji wa JPM sekta ya Afya
Kaimu mganga mkuu hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mawenzi Josephine akipokea msaada kutoka kwa Makamu Mwenyekiti UWT Taifa Thuwaybah Kisasi walipotembelea hospitali hiyo. |
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa
(CCM) Taifa (UWT) Thuwaybah Kisasi, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwekezaji mkubwa aliouweka katika sekta
ya afya nchini.
Kisasi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
wakati wakati (UWT), walipoteembelea katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi,
kwa lengo la kutoa misaada mbalimbali katika wodi ya wamama wajawazito pamoja
na kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa tatu la huduma ya afya ya
mama na mtoto.
Kisasi alisema ameridhishwa na kazi kubwa
ambayo inaendelea kutolea katika
hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi na kuwataka watoa huduma za afya kuendelea
kuwa wamoja, kupendana kila mtu na kuwataka kila mmoja kuendelea kutoa huduma
kwa nafasi yake.
“Katika siku za nyuma, madaktari wengi
walivunjika moyo wa kufanya kazi kwa
sababu kulikuwa hakuna vifaa, mazingira ya kufanyia kazi yalikuwa siyo mazuri,
lakini kutokana na kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya wamu ya tano tumeona kasi
kubwa ya utendaji kazi katika nyanja mbalimbali,"alisema.
Aliongeza kusema kuwa “Naomba niwaeleze wazi
nimeridhishwa sana na utendaji kazi wenu katika kuwahudimia wagonjwa, moyo wa kufanya kazi tumerudishiwa na rais wetu
Dkt. Magufuli, sio hospitali tu
bali katika sekta zote,”alisema
Makamu mwenyekiti UWT Taifa Thuwaybah Kisasi akimpatia msaada wa mche wa sabuni. |
Aidha Kisasi aliupongeza uongozi wa Manispaa
ya Manispaa ya Moshi kwa jinsi unavyovutia kwa usafi ambao umeendelea kusifika
nchini kote.
“Nimeelezwa kuwa mji huu umeendelea kuwa msafi
kutokana na kutunga sheria ndogo ndogo za kusimamia usafi ambazo zimepelekea
kuendelea kuongoza katika usafi kwenye Manipaa hapa nchini hongereni sana,”
alisema Kisasi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu (UWT) Taifa Mwl
Queen Mlozi, alisema Wanawake ndiyo wanufaikaji wakubwa wa huduma za afya,
hivyo, wanampongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Magufuli kwa
kasi kubwa ambayo anaendelea nayo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka
2015/2020, katika huduma za jamii.
Awali akitoa taarifa ya hospitali hiyo Kaimu
mganga mkuu Dkt. Josephine Rogath, alisema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na
upungufu wa watumishi 232 wa kada mbalimbali.
“Hospitali haina kabisa madaktari bingwa wa
dawa za usingizi, afisa utumishi, wataalam wa kada za wahudumu wa afya katika
chumba cha kuhifadhia maiti, mtaalamu wa Tehama, fundi vifaa tiba, fundi sanifu
wa dawa na fundi sanifu wa meno,"alisema Dkt. Rogath.
STORY BY: Kija Elias…..Agosti
22, 2019
Thursday, August 22, 2019
Afisa Utumishi adakwa na TAKUKURU akipokea rushwa ya laki moja
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoani Kilimanjaro, inamshikilia Afisa Utumishi Mwandamizi wa
halmashauri ya Wilaya ya Moshi Julius Kimaro kwa tuhuma za kudai na kupokea
rushwa ya shilingi 100,000.
Akizungumza na Waandishi wa habari
ofisini kwake Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Holle Makungu alisema
mtumishi huyo alitenda kitendo hicho kwa mfanyabiashara wa vinyago.
Makungu alisema alikamatwa na maafisa wa
Takukuru Agosti 20 mwaka huu katika maeneo ya baa iitwayo Forest, Manispaa ya
Moshi
“Afisa Utumishi huyo alipewa majukumu ya
kusimamia makusanyo ya maduhuli katika halmashauri ya Moshi, alipokea rushwa ya
shilingi laki moja kutoka kwa mfanyabishara wa vinyago ambaye baadaye
alituletea taarifaza kuombwa rushwa,” alisema Makungu.
Awali ilielezwa kuwa Kimaro alimkadiria
mfanyabiasharo huyo wa vinyago kuwa anatakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni
nne kwa mwezi.
Hata hivyo Afisa huyo, alimuahidi kuwa
angempunguzia mfanyabishara huyo hadi kufikia kiasi cha shilingi milioni moja
na laki mbili (TZS 1,200,000) endapo angempa kiasi cha shilingi laki moja.
“Baada ya mazungumzo na makubaliano ya
wawili hao ndipo mfanyabiashara huyo alikuja na kutupatia taarifa iliyofanya
tumkamate afisa huyo,” aliongeza Makungu.
Makungu alisema hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya mtumishi huyo baada ya uchnguzi kukamilika huku wananchi
wakitakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi
inapotokea kuna vitendo hivyo bila kujali wadhifa wa mtu au hadhi yake kwa
jamii.
Wednesday, August 21, 2019
Mwanamke mchawi akamatwa juu ya paa la Mchungaji
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia na kumhoji
mwanamke Kabula Masunga(41), anayedaiwa kufanya vitendo vya
kishirikiana(uchawi) baada mama huyo kukutwa ameganda kwenye paa la nyumba la
Mchungaji Jeremia Charles saa 11 alfajiri ya Agosti 18, 2019 akiwa amevalia
mavazi ya nusu utupu na ungo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Juma Bwire
amesema Agosti 20,2019 kuwa mwanamke huyo anatuhumiwa kufanya ushirikina
huo eneo la Isele Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa na kusababisha taharuki
kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amefafanua mwanamke huyo ambaye ni mpagani na mkazi
wa Morogoro alikutwa akiwa katika mazingira hayo akiwa amejifunga mavazi ya
rangi nyekundu na nyeusi lakini kifua aliacha wazi.
"Pia alikutwa akiwa na
ungo uliyofungwa kitambaa ya rangi nyeusi na nyekundu.Amekutwa pia na pembe la
ng'ombe na alijifunga hirizi mikononi. Mwanamke huyo alikuwa na wenzake wanne
inaodaiwa alikuwa anasafiri nao kwa kutumia ungo,"amesema .
Kamanda Bwire
amesema kwa sasa wanaendelea kumhoji zaidi ili kufahamu lengo la kufanya
ushirikina huo.
Tuesday, August 20, 2019
MAKTABA YA JAIZMELA: Slobodan Milosevic ni nani?
Slobodan Milosevic alikuwa
Rais wa Serbia kuanzia 1989 hadi 2000. Pia Milosevic alikuwa Rais wa Jamhuri ya
Shirikisho la Yugoslavia kutoka 1997 hadi 2000.
Aliongoza Chama cha Kijamaa cha
Serbia kutoka msingi wake mnamo 1990 na aliibuka na kuwa Rais wa Serbia wakati
ambao juhudi za kurekebisha Katiba ya Yugoslavia ya mwaka 1974 zilikuwa
zikianza.
Katiba hiyo ilikuwa haina uwezo wa kisiasa kuzuia mizozo katika
Albania na jimbo la Kosovo la Serbia yaliyokuwa yakitaka kujitenga tangu awali.
Asili ya Milosevic ilianzia katika
kijiji cha Lijeva Rijeka pale Podgorica na ukoo kutoka Montenegro.
Alizaliwa
Agosti 20, 1941 katika mji ambao upo kati ya mito mitatu ya Danube, Great
Morava na Mlava wa Požarevac. Milosevic alizaliwa miezi minne baada ya uvamizi
wa Falme ya Yugoslavia uliofanywa na mataifa Ujerumani, Italia na Japan
yalikuwa yakifahamika kama Roberto.
Milosevic alikuwa na kaka yake ambaye
baadaye alikuja kuwa Mwanadiplomasia. Baba yake Milosevic alijiua mwaka 1962.
Pia mama yake aliyekuwa akifahamika kwa jina la Stanislava ambaye alikuwa
mwalimu wa shule na mwanachama hai wa Chama cha Kijamaa alijiua mwaka 1972.
Milosevic alisoma sheria katika Chuo Kikuu cha Belgrade.
Milosevic anakumbukwa
kutokana na kuwa chanzo cha anguko la Shirikisho la kijamaa la Jamhuri ya watu
wa Yugoslavia mwanasiasa huyu wa Serbia mwenye msimamo mkali aliingia
madarakani kupitia harakati kali za utaifa wa Serbia, baada ya kushika hatamu
ya madaraka ya rais wa urais wa Jamhuri ya kijamaa ya Serbia mnamo Mei 8, 1989
hadi Januari 11, 1991 na Urais wa Jamhuri ya Serbia kuanzia Januari 11, 1991–
Julai 23 1997.
Kitendo chake cha kutaka kuwapa nguvu kubwa raia wachache wenye
asili ya Serbia ambao ni Wakristo katika jimbo la Kosovo dhidi ya raia wenye
asili ya Albania walio wengi na ambao pia ni Waislamu kwa madai kuwa raia wenye
asili ya Serbia ambao ni Wakristo walikuwa wanabaguliwa katika jimbo hilo.
Pia
hatua yake ya kupingana na jamhuri nyingine zilizokuwa zinaunda shirikisho la
kijamaa la Yugoslavia katika mpango wa kulifanyia mageuzi shirikisho hilo
kulipelekea kuibuka kwa chuki kali dhidi ya raia wenye asili ya Serbia
waliokuwa wakiishi katika Jamhuri nyingine za shirikisho. Akiungwa mkono na
wanaharakati wa utaifa wa Serbia walio wachache kutoka Kosovo na
Bosnia-Herzegovina pia kwa kupewa msaada na washirika wake katika television ya
Taifa ya Serbia, aliendelea kueneza chuki miongoni wa raia wenye asili ya
Serbia walio wachache katika jamhuri za Croatia na Bosnia.
Television ya Serbia
ilikuwa ikionyesha matukio ya mauaji ya kutisha yaliyofanywa na mafashisti wa
Croatia dhidi ya Waserb wakati wa vita kuu ya pili ya Dunia. Hofu ilitawala
miongoni mwa jamii ya Waserb huko Croatia na Bosnia kwamba hatima kama hiyo
iliyowakuta wenzao na wao inawasubiri.
Hali hii ilipelekea kuibuka kwa itikadi
za kuweka msingi wa uanzishwaji wa Serbia kubwa "Greater Serbia"
taifa ambalo halitakuwa Serbia tu, bali litakalojumuisha na maeneo ya Bosnia na
Croatia yenye idadi kubwa ya wakazi wenye asili ya Serbia.
Ili kufanikisha
mpango huo, mkakati uliokuwa umewekwa ilikuwa ni kuwaondoa raia wote wasiokuwa
Waserb ( Ethnic Cleansing) katika Serbia na miji inayokaliwa na Waserb wengi
katika jamhuri za Croatia na Bosnia.
Mnamo Machi 26, 1990 uongozi wa Serbia
chini ya Rais Slobadan Milosevic ulikutana kujadili hali ya uhasama ulivyokuwa
ikiendelea ndani ya shirikisho la Yugoslavia na kufikia makubaliano rasmi kuwa
vita katika Jamhuri za Croatia na Bosnia-Herzegovina ni suala lisiloepukika.
Julai 2, 1990 bunge la Kosovo nalo lilitangaza kuwa Kosovo ni Jamhuri
yenye hadhi kama zilivyo jamhuri nyingine sita zilizokuwa zikiunda shirikisho
la Yugoslavia. Kufuatia tangazo hilo, Bunge la Serbia lilipiga kura kuweka
marufuku kwa jimbo la Kosovo lenye Waislamu wengi ambao ni wakazi wenye asili
ya Albania kuwa na Bunge lake.
Milosevic alifariki dunia Machi 11, 2006. Milošević
alikutwa amekufa katika seli yake ya gereza katika Mahakama ya Uhalifu wa
Kivita ya ICC, The Hague, Uholanzi.
Imetayarishwa na Jabir Johnson,.....Agosti 20, 2019
Monday, August 19, 2019
Afghanistan yaadhimisha miaka 100 ya uhuru wake
Afghanistan
inasherehekea miaka 100 ya uhuru wake. Agosti 1919, baada ya vita vya tatu vya
Uingereza na Afghanistan na baada ya miaka 60 ya utawala wa Uingereza, nchi
hiyo ilitambuliwa kama taifa huru.
"Sina matumaini
tena na nchi yangu. Nimempoteza kaka yangu, marafiki waliokuja kwenye harusi
yangu. Sina hamu tena na sherehe za uhuru wa nchi yetu. Waache wapambe mji na
wauangaze. Sherehe za uhuru ni kwa ajili ya matajiri tu. Kwenye harusi yangu
walikuwepo wafanyakazi na watu wa kawaida tu."
Wafghanistan wengi
hawajihisi kusherehekea. Mmoja wa wasiosherehekea ni Mirwais Alani,
bwanaharusi, ambaye harusi yake ililengwa na shambulizi la kundi la kigaidi la
Dola la Kiislamu mwishoni mwa wiki.
Zaidi ya wageni 60 na
wanafamilia waliuawa na zaidi ya 180 walijeruhiwa. Wakati wahanga wa kwanza
wakizikwa jana mjini Kabul, Mirwais alizugumza na ripota kutokea ofisi za
shirika la habari la reuters.
CHANZO: DW
Dkt. Mghwira atoa mifuko 100 ya saruji Same
Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule akikabidhi mifuko ya saruji kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kiimanjaro Dkt. Anna Mghwira. |
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira, ametoa msaada wa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mtii na ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Magulunde iliyopo wilaya ya Same mkoani hapa.
Dkt. Mghwira alisema,
ameamua kutoa msaada huo wa saruji, ili kuwaunga mkono wananchi wa kata hiyo,
waliojitolea kuanza ujenzi wa madarasa katika shule hiyo pamoja na kituo
cha afya ili waweze kukamilisha ujenzi huo.
Dc Senyamule pia
alitoa rai kwa kamati ya ujenzi kuhakikisha kwamba saruji
iliyotolewa wanaitumia kwa lengo yaliyokusudiwa na endapo atabainika mtu
yeyote kujihusisha na uchakachuaji wa saruji hiyo hata sita kumchukulia hatua
kali za kisheria.
“Msaada huu wa mifuko
100 ya saruji ambayo nimewakabidhi hivi punde kwenu leo ni kwa ajili ya
kusaidia ujenzi wa kituo cha afya Mtii na ujenzi wa madarasa katika sule ya
msingi Magulunde,
nawaomba saruji hii itumike kwa kujenga kituo cha afya na madarasa, sitaki
kusikia imebadilishiwa matumizi wala kusikia kwamba imeibiwa,”alisema DC Senyamule.
Dc Senyamule
alisema hakuna taifa lolote duniani ambalo linaweza kuendelea bila kuwekeza
katika sekta ya elimu, hivyo ninatoa wito kwa wazazi na walezi kuwekeza kwa
watoto wao kwa kuwapatia elimu ambayo itakuwa msingi wa maisha yao ya baadae.
Aliongeza kusema kuwa
“Napenda kuona watoto wanasoma katika mazingira mazuri ili watimize ndoto
zao hatimaye baadae wawe viongozi wazuri wa taifa hili, walimu wakikaa
katika ofisi zilizo bora hata moyo wa kufundisha wanakuwa nao,”alisema Dc Senyamule.
STORY BY: Kija Elias….Agosti
2019
Wananchi wamlilia DC Senyamule mikutano ya serikali ya Kijiji
Wananchi wa kijiji cha Mhero Kata ya Chome, Wilaya ya Same
mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kitendo cha kutoitishwa mikutano ya kijiji
mara kwa mara pamoja na kusomewa taarifa za mapato na matumizi ni moja ya
sababu kubwa inayokwamisha shughuli za maendeleo katika kijiji hicho.
Wakizungumza katika mkutano wa kijiji ambao uliitishwa na Mkuu
wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule kwa malengo ya kutatua kero za
wananchi, pamoja na kujadili changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja
na shughuli za maendeleo, wananchi hao wamewatupia lawama wenyeviti
wa vijiji kwa kutoitisha mikutano ya serikali ya kijiji chao.
Kufuatia kuwepo kwa tuhuma hizo, Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka
Wenyeviti wa Vijiji wilayani humo, kuhakikisha kwamba wanasoma taarifa ya
mapato na matumizi kwa wananchi kabla ya Agosti 30 mwaka huu.
DC Senyamule
alilazimika kutoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na kwenye mkutano wa
hadhara na wananchi wa kijiji cha Mhero Kata ya Chome ikiwa
ni ziara yake ya kutatua kero za wananchi ambapo baadhi ya wananchi
walionyeshwa kukerwa na viongozi wa vijiji kwa kushindwa kutoa taarifa za
mapato na matuzi kwa muda mrefu.
“Naomba kutoa maagizo
ya serikali hapa, ifikapo Agosti 30 mwaka huu, nataka wenyeviti wa vijiji muwe
mmeshasoma taarifa za mapatio na matumizi na tarifa hizo ziweke kwenye
matangazo ili kila mwananchi aweze kuisoma taarifa hiyo,” alisema DC Senyamule.
Alisema Mwenyekiti
yeyote wa serikali ya kijiji asiondoke madarakani kabla hajasoma taarifa za
mapato na matumizi, ikiwemo michango ya wananchi walivyoshirika katika
kuchangia shughuli za maendeleo katika eneo husika.
Aidha DC Senyamule
alimwagiza Mkaguzi wa ndani ahakikishe ndani anafanya ukaguzi na kumpelekea
taarifa hizo baada ya wiki mbili ofisini kwake.
Pia Mkuu huyo wa
wilaya alitoa maelekezo kwa mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha Kituo cha
afya cha Shengena kinaanza kutoa huduma ifikapo Septemba mosi mwaka huu,
hususani katika upande wa wodi ya mama na mtoto.
Thursday, August 15, 2019
MAKTABA YA JAIZMELA: Napoleon Bonaparte ni nani?
Napoleon Bonaparte alikuwa
mwanajeshi wa Ufaransa na kiongozi wa kijeshi wa asili ya Italia ambaye
aliibuka juu wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa na aliongoza kampeni kadhaa
zilizofanikiwa wakati wa Vita vya Mapinduzi vya Ufaransa.
Alikuwa Mtawala wa
Mfaransa kama Napoleon I kutoka 1804 hadi 1814 na tena kwa ufupi mnamo 1815
wakati wa Siku Hizi. Napoleon alitawala mambo ya Ulaya na kimataifa kwa zaidi
ya muongo mmoja wakati akiiongoza Ufaransa dhidi ya safu ya umoja katika Vita
vya Napoleon. Alishinda zaidi ya vita hivi na idadi kubwa ya vita vyake,
akijenga himaya kubwa ambayo ilitawala sehemu nyingi za Ulaya kabla ya
kuangushwa kwa mwisho mnamo 1815.
Anachukuliwa kuwa mmoja wa makamanda wakubwa katika historia, na vita vyake na kampeni zake zimesomwa. kwenye shule za kijeshi ulimwenguni. Urithi wa kisiasa na kitamaduni wa Napoleon umeendelea kuwa mmoja wa viongozi wanaosherehekea na wenye utata katika historia ya wanadamu.
Anachukuliwa kuwa mmoja wa makamanda wakubwa katika historia, na vita vyake na kampeni zake zimesomwa. kwenye shule za kijeshi ulimwenguni. Urithi wa kisiasa na kitamaduni wa Napoleon umeendelea kuwa mmoja wa viongozi wanaosherehekea na wenye utata katika historia ya wanadamu.
Napoleon alizaliwa Agosti 15,
1769 huko Corsica kwa familia ya wastani kutoka kwa ukuu mdogo wa Italia na
kufariki Mei 5, 1821.
Alikuwa akihudumu kama afisa wa shughuli za sanaa katika jeshi la Ufaransa wakati Mapinduzi ya Ufaransa yalipotokea mnamo 1789. Aliongezeka haraka kupitia safu ya jeshi, akachukua fursa mpya zilizowasilishwa na Mapinduzi na kuwa mkuu akiwa na miaka 24.
Alikuwa akihudumu kama afisa wa shughuli za sanaa katika jeshi la Ufaransa wakati Mapinduzi ya Ufaransa yalipotokea mnamo 1789. Aliongezeka haraka kupitia safu ya jeshi, akachukua fursa mpya zilizowasilishwa na Mapinduzi na kuwa mkuu akiwa na miaka 24.
Same yapokea msaada wa vitabu vya Sayansi kutoka Uingereza
Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imepokea shehena ya vitabu vya masomo ya Hisabati, Baiolojia, Chemistry na Fizikia vilivyotolewa na wadau kutoka nchini Uingereza kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi.
Akizungumza katika
hafla ya kupokea msaada huo iliyoenda sanjari na uzinduzi wa Maktaba maalumu ya
Sayansi iliyopo katika kijiji cha Goma kata ya Mshewa, Mkuu wa Wilaya ya Same Senyamule
amewashukuru wadau wa Word Expedition Exchange kutoka nchini Uingereza kwa
msada walioutoa kwani uwepo wa vitabu hivyo, vitahamasisha masomo ya Sayansi
kwa wanafunzi wa shule za sekondari za maeneo ya vijijini.
DC Senyamule
aliwaomba wadau hao kuendelea kuifadhili wilaya ya Same katika nyanja
mbalimbali ikiwemo sekta ya maji na afya huku pia akitoa wito kwa
walimu wa shule za sekondari zilizopo kwenye ukanda huo kuhakikisha kuwa vitabu
hivyo vinatumika kuleta matokeo chanya.
“Uwepo wa vitabu
hivi utasaidia kupata wataalamu watakaotusaidia kuleta maendeleo katika misingi
ya kuwajengea uwezo wa elimu, kwani tutakuwa na uhakika wa madaktari
, mainjinia, tutakuwa na mafundi katika sekta ya kilimo, mifugo na maji hivyo
changamoto za wataalamu kwenye maeneo yetu haya tutakuwa tumezitatua ,”alisema
DC Senyamule.
Aliongeza kuwa
“Nawaomba wanafunzi muwape muda waje wasome vitabu hivi, mimi nilituma
wataalamu wangu waje kuviangalia kama vinafaa kwenye mitaala yetu, walinipatia
majibu kwamba vitabu hivyo vinavyofaa,”alisema DC Senyamule.
Alifaanua kwamba
kama wataalamu walinithibitishia kwamba ni vitabu vinavyofaa ni wazi kuwa
tunawezo wa kuvitunza vitabu hivyo ili vitumike hata wenzetu waliotusaidia
kuleta vitabu hivi waweze kuona kuwa kazi yao imekuwa na faida kwa watoto wetu
kufaulu vizuri.
Kwa upande wake
Mwalimu Gisela Trimo, alisema kuwa uwepo wa vitabu hivyo utasaidia kuinua
ufaulu kwa wanafunzi kwenye masomo ya Sayansi kwa sababu walikuwa na
upungufu mkubwa wa vitabu hivyo.
“Vitabu hivi
vitaleta mapinduzi makubwa katika ufundishaji na ufundishwaji kwani
mashuleni unakuta wanafunzi wana kitabu kimoja lakini wanaotumia ni wanafunzi
kati ya watatu hadi watano,”alisema Mwl Tarimo.
Naye Mratibu wa
Utalii wa Asili wa milima ya Chome na Shengena Elly Kimbwereza, ambaye alikuwa
mwenyeji wa wageni hao, alieleza jinsi Utalii wa Asili unavyoweza kuunganishwa
na shughuli za jamii husika na kuleta maendeleo .