Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga
marufuku Polisi jamii kukamata bodaboda zinazofanya makosa ya usalama
barabarani nchini.
Pia Waziri huyo amepiga marufuku polisi wa usalama
barabarani kukamata vyombo vya moto wakiwa hawajavaa sare za Jeshi.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mafisa, Kata ya Mwembesongo, mjini
Morgoro, jana, Lugola alisema Polisi Jamii hawana ujuzi wa kijeshi wa ukamataji
wa bodaboda hivyo kuendelea kuifanya kazi hiyo ni kuwanyanyasa wananchi.
“Nimepata malalamiko mengi ninapofanya ziara zangu hapa
nchini, wengi wanawalalamikia Polisi Jamii kuwaonea, kuwaomba rushwa na
kuwakamata pasipofuata utaratibu unaotakiwa kijeshi, hapa Morogoro pia, katika
mkutano huu wa hadhara mnayasema yale yale, sasa natangaza kuanzia leo,
marufuku Polisi Jamii kukamata bodaboda,” alisema Lugola.
Waziri Lugola pia alipiga marufuku baadhi ya Polisi wa
Usalama barabarani ambao wenye tabia ya kutovaa sare za Jeshi na kuingia barabarani
au mitaani na kuyakamata magari na bodaboda.
Lugola alisema lazima polisi wafate sheria za usalama
barabarani hasa wanapokamata magari yanayofanya makosa, uvaaji wa sare za Jeshi
ni muhimu na unapaswa kufutwa.
Waziri Lugola aliongeza kuwa, bodaboda au vyombo vingine vya
moto, zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila
kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata
ridhiki kupitia biashara hiyo.
“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia
ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha
bodaboda,” alisema Lugola.
Lugola alifafanua kuwa, bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo
cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda
zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika
katika ajali.
“Bodaboda hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini
kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii
nataka Polisi nchi nzima munielewe,” alisema Lugola.
Story by: Felix
Mwagara, MOHA-Morogoro
0 Comments:
Post a Comment