Monday, March 11, 2019

Wanawake wahimizwa kuwania nafasi uchaguzi serikali za mitaa


Mkurugenzi wa Tusonge CDO Aginatha Rutazaa (mstari wa mbele aliyevaa batiki) akiwa katika maandamano na wanawake wa Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Machi 11, 2019 Korini Kusini, Kata ya Mbokomu mjini Moshi.
Wanawake mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu. 

Akizungumza na wanawake kwenye ofisi za kijiji cha Korini Kusini, Kata ya Mbokomu kwenye mkutano uliowakutanisha kuadhimisha siku ya wanawake duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Tusonge CDO Aginatha Rutazaa alisema wanawake wamekuwa nyuma kwenye maeneo mbalimbali ya jamii kutokana na mifumo potofu ambayo imekuwa ikiwanyima kuwa na usawa katika utoaji wa sauti katika ujenzi wa maendeleo. 

Rutazaa alisema uchaguzi wa serikali za mitaa ndio msingi mahususi wa kupata viongozi bora, hivyo maandalizi madhubuti ya kuwapata viongozi bora yanatakiwa huku wanawake nao wakiitazama fursa hiyo kuwa ni yao. “Mwanamke anajiandaaje kupata fursa katika uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema Rutazaa na kuongeza, “Nani atakayewasemea kama hamtaingia kuwania.” 

Hata hivyo Rutazaa alisema baadhi ya migogoro kwenye mitaa inasababishwa na maamuzi ya viongozi wabovu.  Aidha Rutazaa alisema ulevi umekuwa sababu kubwa ya kumnyima mwanamke nafasi. “Ulevi kupindukia unaweza kukutoa kwenye uwezo wako wa kufikiri,” alisema Rutazaa. 

Pia Rutazaa aliitaja sababu nyingine ya wanawake kushindwa kupenya katika jamii ni uelewa mdogo wa haki za msingi na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeingia kwa ajili ya kuleta usawa wa jinsia katika jamii. 

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kuwawezesha wanawake kiuchumi Haika Manase alisema Asilimia 75 ya wanufaika wa Miradi ya Tusonge CDO ni wanawake zaidi ya 175 katika kategori ya kilimo, ufugaji na mradi wa kutengeneza nguo aina ya batiki. 

Aidha Manase alisema umiliki wa ardhi kwa mwanamke ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika jamii hivyo wanawake wanapaswa kubadili fikra zao katika kuitazama jamii ili kuiletea maendeleo. 

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Korini Kusini Emmanuel Mrema alisema vipigo, ubakaji na ulevi kupindukia bado ni changamoto hali ambayo imekuwa ikizorotesha maendeleo endelevu katika jamii. 

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wanawake mwaka huu ilikuwa ni “Badili Fikra kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu.”
Mkurugenzi wa Tusonge CDO Aginatha Rutazaa (mstari wa mbele aliyevaa batiki) akiwa na wanawake wa Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi.
 Story by: Kija Elias, Moshi-Kilimanjaro (Machi 11, 2019)

0 Comments:

Post a Comment