Monday, March 25, 2019

Watakiwa kupanda miti kwenye makaburi


Miti katika makaburi
Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kujengea makaburi pindi wapendwa wao wanapofariki na badala yake wapande miti ya matunda kama vile maparachichi juu ya kaburi hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti LEPAJE, Leonard Massawe, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi mkoani humo.

Massawe ambaye pia ni mwanaharakati wa mazingira Mkoani Kilimanjaro, ameanza kampeini ya upandaji wa miti ya matunda juu ya makaburi, lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema ameanzisha kampeni hiyo ya uoteshaji wa miti ya matunda juu makaburi ikiwa ni kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini kwa kubadili wafu kuwa mti wa matunda.

“Ninaishauri jamii kuanza kubadilisha mitazamo yao kuwa mpendwa wao anapofariki wanaanza maandalizi ya kumjengea kaburi, wanachotakiwa kwa sasa ni kujenga  mazoea ya kuoteshe miti ya maparachichi, machungwa na mipapai,”alisema.

Alifafanua kuwa uoteshaji wa miti ya matunda kwenye makaburi itasaidia kuyatunza mazingira na kuongeza kipato na lishe kwa familia.

Hata hivvyo Massawe, alisema kwamba shirika hilo limeanza kampeini ya upandaji miti ya miparachichi juu ya kaburi la Mama yake Mkangera Koyanga aliyezaliwa mwaka 1910 na kufariki dunia 2001, ikiwa ni kuihamasisha jamii kuacha kujengea makabuli na badala yake wapande miti ya matunda juu ya makaburi hayo.

Vilevile alisema LEPAJE amewataka watanzania kujenga mazoea ya kutunza mazingira ikiwemo kila mwananchi kupanda miti mahali anapoishi ili kusaidia kuweka mazingira katika mpangilio mzuri.

Alisema endapo mwananchi atajenga tabia hiyo itawezesha kulinda uoto wa asili ambao kwa sasa umeonekana kuharibiwa kwa kiasi kikubwa.

“Kwa mwaka jana LEPAJE tulipanda miti 10,000 wilayani Mwanga, na kwamba tumefanikiwa kuendesha zoezi hilo la uhamasishaji wa upandaji miti kila mwaka kwa njia mbalimbali,”alisema Massawe.

Story by: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment