Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Wednesday, November 29, 2023

Kaburi lafukuliwa lakutwa na Sanda nyeusi, Nazi Tatu na Yai Viza



Wananchi wa Mtaa wa Mafuriko, iliyopo Kata ya Mzizima Mkoani Tanga wamepata taharuki baada ya kusambaa kwa taarifa za uwepo wa kaburi la Mwanamke mmoja mwenye asili ya kiarabu aliyeuawa na kuzikwa  kwenye eneo la Mwekezaji kitendo kilichopelekea Serikali kuamua kufukua kaburi hilo ili kujiridhisha.


Akiongea baada ya zoezi la uchimbaji wa kaburi hilo Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji amesema Mara baada ya kupata taarifa walichukua hatua za kufukua kaburi hilo kwa kibali cha Mahakama ambapo baada ya  kufukua kaburi wamekuta sanda nyeusi, nazi tatu na yai viza


“Ni kaburi ambalo lilionekana lipo ndani ya eneo la Mwekezaji lakini sambamba na hilo wakati tunaendela na ufukuaji tumekuta Wananchi wengi wamevamia eneo la Mwekezaji ambalo limepimwa viwanja kwa kisingizio kwamba hawana maeneo ni kana kwamba wametengeneza tukio hilo ili kumtisha Mwekezaji na Watu waliopimiwa viwanja”


DC Kaji amepiga marufuku Mwananchi yeyote kuonekana katika eneo hilo la Mwekezaji akisema kumekuwa na tabia ya Wananchi kuvamia maeneo ya wazi na baadaye kuomba fidia kwa Serikali jambo ambalo linapelekea matatizo makubwa ya migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi ni uvamizi wa Wananchi  kwenye maeneo yenye hati miliki


“Nimetoa onyo  na hatutamvumilia Mtu yeyote na wengi wamekuwa wakikimbilia kwa Wanasiasa kwamba ni Wapiga kura wetu hilo halitakuwepo na hatutalivumilia, Tanga tunaweza kuishi bila migogoro” amesema James Kaji


#Khadija Bagasha, Tanga.

Monday, November 27, 2023

TUGHE yataka wafanyakazi wachunguzwe Afya ya Akili kabla ya kupewa adhabu wanapokosa

Mkurugenzi wa Utawala na Meneja Rasilimali watu Wizara ya Mambo ya Ndani Miriam Mbaga akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Jeshi la Uhamiaji katika kikao cha Utekelezaji kilichofanyika Novemba 27, 2023 kwenye Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) mjini Moshi.


Wasimamizi wa Wafanyakazi mahali pa kazi wametakiwa kufanya uchunguzi wa kina pindi Wafanyakazi wanapokiuka kanuni, taratibu na Sheria za kazi kabla ya kutoa adhabu stahiki ili kubaini makosa yaliyofanyika yametokana na Afya ya Akili au Uzembe.



Akizungumza katika Kikao cha Utekelezaji cha Baraza la Wafanyakazi la Jeshi la Uhamiaji kilichofanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) Meneja Rasilimali watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Miriam Mbaga amesema kumekuwa na utoaji wa adhabu Kali kwa wafanyakazi pindi wanapokiuka kanuni, taratibu na Sheria za kazi pasipo kuchunguza Kama ni Afya ya Akili au la hatua ambayo imekuwa ikileta majanga mengi kwa baadhi ya wafanyakazi kujiua.

"Kwa mujibu wa taarifa za watalaamu linaonyesha tatizo hili ni kubwa kulingana na aina maisha tunayoishi sasa, maendeleo na mambo mengine, hatutaishia hapa tunao watumishi mikoa yote tutaweka utaratibu wa kuwafikia watumishi wetu ili waelewe tatizo lipo na namna gani wanaweza kujiepusha na tatizo hilo," alisema Mbaga

Katika utoaji wa mada Dkt.Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema changamoto ya Afya ya Akili nchini ni kubwa na hatua za makusudi kupambana na Hilo lazima zichukuliwe.

"Kuna watu tunaishi na watu ambao hatujawahi kuwatikisa na tunao na wana viashiria vyote vya kudhuru, siha njema ya akili ni muhimu, kila watu wanne mmoja anakuwa na changamoto ya afya ya akili," alisema Dkt. Kweka.

Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Uhamiaji Kamishna Gerald Kihinga amesema Mada ya Afya Akili imekuwa ya muhimu ili kuongeza ufahamu juu ya suala hilo ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

"Katika semina hii watu wameanza kujua, kumbe na mimi nina na tatizo la afya ya akili ni vema kuchukua hatua mapema Mtu anakuwa mlevi kupita kiasi, haendi kazini, anafanya kazi chini ya kiwango, wengine wanachukua hatua ya kujinyonga wanahitaji msaada kusaidiwa," alisema Kamishna Kihinga.

Mbali na hilo Mbaga amewataka Wafanyakazi nchini kuanza maandalizi ya Kustaafu ikiwamo kuishi na jamii vizuri wangali Bado makazi ili muda utakapofika wa kurudi uraia  wawe na mahusiano mazuri na jamii zao.

"Kuna wengine wanaondoka na vyeo vyao na nafasi zao ,  na wanapata taabu ya kuishi na jamii, wakiwa kazini akili zao hawaziweka kuwa kuna siku mishahara itakoma, posho zitakoma itabaki pensheni watahitaji kipato kingine, wanapata washauri wabaya matokeo yake maisha yao yanakuwa ni ya duni au mafupi zaidi," alisema Mbaga


Wakitoa shukrani zao za dhati kwa Uwepo wa kikao hicho cha kikatiba washiriki wamelitaka Baraza lizifanyie utatuzi wa haraka changamoto pindi zinapowafikia mezani.







Sunday, November 26, 2023

Umejiandikisha Uru Fun Run 2023?

 

Zoezi la kukimbia ndio linashika namba moja duniani kwa kuleta matokeo makubwa kwa afya ya mwili.
Ndio maana wakimbiaji wa wanaishi maisha marefu zaidi kwani wanaepukana na unene uliokithiri.Jicho la kitabibu linatazama zaidi faida za kiafya za mashindano haya ikiwamo uboresha
Afya ya Moyo na utimamu wa mwili ili kuleta matokeo makubwa na ya haraka
ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Miradi iliyopo Msomera mbioni kukamilika

Makatibu Wakuu wakipokea taarifa kuhusu ujenzi wa shule ya sekondari inayojengwa katika Kijiji cha Msomera wakati wa ziara  ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi nyumba na miundo mbinu ya kuhamisha wananchi wanaotoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika KIjiji hicho  Wilaya ya Handeni  mkoani Tanga


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi Dkt. Yonazi amesema Serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa wizara zote za kisekta zinashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa miradi iliyopo katika Kijiji cha Msomera inakamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhamia katika eneo hilo ili kuendelea shughuli zao.


Dkt. Yonazi aliyasema hayo wakati  wa ziara ya kikazi  ya Makatibu Wakuu wa Wizara za kisekta waliyoifanya katika  Kijiji cha Msomera, Wilaya, Handeni mkoani Tanga kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu  kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya kuhamisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari.


Amesema Makatibu Wakuu  hao wamekagua ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo maji, umeme, madaraja, barabara, shule, Nyumba za makazi na uboreshaji wa huduma za mawasiliano.


“Niwaombe wanaohamia eneo hili waiamini Serikali kwamba inawatengenezea mazingira yaliyo bora sana hapa Msomera, nyumba  zinazojengwa  na huduma zote zina ubora ili wananchi wetu wanufaike  na Serikali yao waachane na upotoshaji kwa sababu imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama,”Amesema Dkt. Yonazi.


Naye  Kamanda wa Kikosi  Kazi cha Ujenzi wa nyumba 5000  kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kila taasisi ya kisekta na Wizara  zinawajibika ipasavyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati  akisema kuwa  licha ya changamoto za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali lakini kazi inaendelea vizuri .


“Mpaka sasa ujenzi wa Msomera  ambao tumeugawanya katika vitalu kuanzia A mpaka D tuko katika hatua mbalimbali za ujenzi nyumba 1000 katika eneo la Msomera B kitalu F viwanja 768  taratibu zake zimekamilika eneo liko tayari kwa ajili ya uchimbaji na kuanza msingi na kuendelea na hatua za ujenzi,”Ameeleza Brigedia Jenerali Mabena.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando  amewashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kutembelea mradi huo hatua inayoongeza kasi yake kusonga mbele akiahidi kusimamia kwa karibu mradi huo ambao umefanyika kama hatua ya kuboresha maisha ya watanzania kila mwananchi kuishi katika hali ya ustawi pamoja na uwepo wa miundo mbinu muhimu pamoja na huduma za kijamii.


“Hii inaonyesha nia ya dhati ya Serikali  ya kukamilisha mradi huu muhimu kwa wakati siyo tu kuhamisha watu lakini unaenda kuboresha maisha ya watanzania tunaendelea kuwaahidi kwamba tutasimamia kwa karibu tunajua unatekelezwa wakati wa mvua ambapo kwetu ni fursa ya kuona namna ya kuyavuna maji  kwa ajili ya matumizi,”amebainisha  


Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Bw. Martin Oleikayo Paraketi amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mradi huo akisema umekuja kwa wakati muafaka kwani umesaidia  wakazi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo kupata huduma muhimu zikiwemo mawasiliano, ujenzi wa shule za sekondari, kituo cha afya na barabara.


“Hii kwetu ni neema kubwa sana Serikali inafanya kazi kubwa na niwaambie waliopo Ngorongoro wasikubali kupotoshwa na watu wachache wasio na nia njema  kijiji cha Msomera ni kijiji mojawapo  kati ya Vijiji 91 ndani ya Wilaya ya Handeni mradi huu umeleta faida kubwa kupitia wenzetu waliohamia kutoka Ngorongoro,”Amepongeza Mwenyekiti huyo.





Thursday, November 23, 2023

TRITA kuongoza wadau Uhamiaji kuzuru Arusha National Park


Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Tanzania(TRITA) kilichopo Moshi mjini Mkoa wa Kilimanjaro, kinatarajiwa kuongoza ujumbe wa Wadau wa Uhamiaji nchini kuzuru Hifadhi ya Taifa Arusha, ikiwa ni madhumuni ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini na kuchangia ukuaji wa mapato yanayotokana na utalii nchini.


Akizungumza jana na Mwandishi wa Tanzania Leo, Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji nchini, Mrakibu Paul John Msele, alisema lengo la ziara hiyo katika hifadhi ya Taifa Arusha ni kuhamasisha watanzania kujiwekea desturi ya kuzitembelea hifadhi za taifa zilizopo karibu na maeneo yao  ili kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya hifadhi hizo.


Mrakibu Msele alisema, ziara hiyo itaongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) SP Ignatius Mganga, ambapo ataongoza taasisi 100 ambao ni wadau wa Uhamiaji nchini, waliopo mkoani humo kwa ajili ya kushiriki warsha inayohusiana na Masuala ya Usimamizi wa Uhamiaji nchini yanayofanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA), Kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro.


Alisema imechukulia kwa umuhimu mkubwa tukio la uzinduzi wa Filamu ya The Royal Tour kwa sababu ni hatua ambayo Rais Samia mwenyewe alichukua jukumu la kuieleza dunia  vivutio  mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini ili kuweza kutoa Uwekezaji na masuala ya utalii katika kuongeza pato la Taifa.



Akifungua Warsha ya siku mbili ya Masuala ya Usimamizi wa Uhamiaji nchini iliyofanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA), Mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya, alisema Rais Samia amefanya jitihada kubwa sana ya kuitangaza nchi ya Tanzania duniani kuwaambia ni nchi yenye vivutio vingi, vya kiutalii nchi yenye fursa za kiuwekezaji, na kuna amani na utulivu.



“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya jitihada kubwa sana za kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kuwaambia kuwa ni nchi yenye vivutio vingi vya kiutalii, nchi yenye furza za kiuwekezaji na kuna amani na utulivu,”alisema Mmuya.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala alisema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.



“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,na idadi kubwa ya wageni imekuwa ikiongezeka,” alisema Dkt. Makakala.



Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Juma Dossa, kutoka  Hospitali ya Aga Khan anayesimamia vibali vya wageni wote wanaokuja kutoa huduma  katika  hospitali hiyo  kama  vile madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wa mitambo, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo ina vivutio vingi vya kutembelea kwa ajili ya utalii na watu wengi duniani wameitambua kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour.



Uru Fun Run 10K, 5K kufanyika Desemba 30

 


Mbio za Kilometa tano, na kumi za Uru Fun zinatarajiwa kufanyika Moshi Vijijini mnamo Desemba 30 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kufunga mwaka 2023.


Akizungumza na JAIZMELA Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wilhad Kitari alisema maandalizi yanaendelea.

 

Tuko kwenye maandalizi ya Mbio za riadha zinazofahamika kama Uru Fun Run,  ni mbio  ambazo ni za hiari  na kupitia mbio hizo zitasaidia zaidi kwa kuwaunganisha wananchi wa Uru  pamoja na Watanzania kutoka nje ya Uru kwa ajili ya kuwaleta pamoja,” alisema Kitari.

 

Aidha Kitari aliongeza kuwa mbio hizo zitakuwa sehemu ya kukuza uchumi wa wakazi wa Moshi Vijijini

 

“Mbio hizi zitasaidia sana kukuza uchumi wa wakazi wa Uru watakaokuja kushiriki mbio hipo, kwani wataweza kununua vitu mbalimbali lakini pia na kuvifahamu  vitu mbalimbali vya Ur,” aliongeza. 

 

Hata hivyo mbio hizo zitaenda sambamba na changizo kwa ajili ya maandalizi ya mbio za Uru Marathon ambayo itafanyika rasmi mwaka 2024 pia kusaidia ujenzi wa matundu ya choo katika shule, wasiojiweza na wajane.

 

“Kupitia mbio hizi tutawahamasisha watu kuchangia kwa maana ya kujisajili na tunategemea sehemu ya fedha hizo zitakapopatikana ziweze kwenda kuimarisha shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye kata yetu ya Uru. Ikiwemo ujenzi wa miundombinu  ya barabara, ujenzi wa matundu ya vyoo kwenye shule , kusaidia watu wenye mahitaji maalumu  kama vile wazee, watoto yatima na wajane.

 

Vyakula mbalimbali kama vile KITOLOLO, NDUTU, VIAZI VIKUU VYA KUCHEMSHA, NDUU, vitakuwa sehemu ya kuonyesha utamaduni wa wakazi wa Uru

 

“Tunarudi kuwahamasisha wananchi kurudi kwenye asili yetu, KISUSIO, kitakuwepo pia  kinywaji cha asili cha  pombe aina ya MBEGE, ili kudumisha tamaduni, mila na desturi za wachaga,” alisisitiza Kitari.

 

 

Huduma za Uhamiaji zinavyoweza kukuza uchumi wa Tanzania

Idara ya Huduma za Uhamiaji imeanzishwa chini ya Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 1995 Sura ya 54 iliyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2015.

Kifungu hicho kinaipa Idara mamlaka ya kudhibiti na kuwezesha masuala ya uhamiaji katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Idara hii ni moja ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Kazi kubwa ya Jeshi la Uhamiaji ni Kudumisha Usalama wa Taifa kupitia Udhibiti wa Uhamiaji. Kutoa hati za kusafiria na hati zingine za kusafiria kwa raia wa kweli. Kutoa Vibali vya Ukaazi na Pasi kwa wageni anaoishi nchini. Kurahisisha na kudhibiti mienendo ya watu ndani na nje ya nchi. Kuratibu na kuwezesha maombi ya Uraia wa Tanzania.


Siku hizi diplomasia hutumika kwa masuala ya biashara, uchumi na utamaduni pale nchi zikisainiana mikataba.


Diplomasia inamdai mhusika awe na utaalamu hasa upande wa sheria, pamoja na ustaarabu na sifa nyingine zinazorahisisha mafungamano.


Mnamo mwaka wa 2019, Afrika Mashariki ilikaribisha sehemu kubwa zaidi ya wahamiaji wa kimataifa wanaoishi Afrika (30%), ikifuatiwa na Afrika Magharibi (28%), Afrika Kusini (17%), Afrika ya Kati (14%) na Afrika Kaskazini (11%).


Uhamiaji ulioandaliwa na kupangwa unaweza kuleta maendeleo barani Afrika katika siku zijazo. Miaka michache ijayo, Tanzania itapata ongezeko la wawekezaji wa kigeni na pia watu kutoka mabara mengine; kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.


Dhana ya diplomasia ya uchumi inaweza kumaanisha uwakilishi wa nchi nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi. Mambo haya ni pamoja na yale yahusuyo uwekezaji na biashara. Kila moja kati ya haya ni muhimu kwa nchi yoyote inayojihusisha kiuchumi na mataifa mengine.


Kuna mambo ya msingi ambayo lazima yaeleweke vizuri na yazingatiwe ili diplomasia ya uchumi ifanikiwe.


Mosi; Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali. Ili kuvutia uwekezaji kunahitaji ujuzi maalumu. Pia, lazima kujua fursa na miradi ya uwekezaji iliyopo katika nchi.


Pili; kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kufanya biashara na nchi za nje kwa urahisi. Mambo haya ni pamoja na kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika. Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.


Tatu; shughuli za kuvutia watalii kutoka nje ya nchi kuingia nchini zinapaswa kuwemo.  Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu walio nje ya nchi wanapaswa kuwa wawezeshaji katika kuletwa watalii nchini.


Mnamo Novemba 22, 2023 Jeshi la Uhamiaji nchini  pamoja na wadau wa Uhamiaji ambao ni taasisi za umma na binafsi zipatazo 100 zilikutana katika Chuo cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) kilichopo mjini Moshi kwenye warsha ili kujadili namna Usimamizi wa Huduma za Uhamiaji unavyoweza kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi ya taifa.


Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku mbili Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya alisema udhaifu wa mtu mmoja isiwe sababu ya kuharibu diplomasia ya nchi.


Mmuya aliongeza kuwa utoaji wa Huduma za Uhamiaji unapaswa uwe rafiki kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya Utalii ambao ni muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi.


Hata hivyo Katika Warsha hiyo iliyojumuisha Taasisi 100 wadau wa Uhamiaji nchini Katibu Mkuu amekemea vitendo vya rushwa kwa ustawi wa uchumi wa nchi.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala alisema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.


“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,” amesema Dkt. Makakala


Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan alisema, “Uwekezaji ambao unaofanyika Tanzania Bara msije mwekezaji huyo huyo kama anataka kwenda Zanzibar msije mkapata kigugumizi itakuwaje kibali kimetoka Tanzania Bara kiende na Zanzibari ni barua tu muwe na amani msije mkadhani atatiwa ndani.”


Aidha Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji (TRITA) SP Ignatius Mganga amesema, “Hii ni forum pekee nchini ambayo inajadili mustakabili wa shughuli za uhamiaji nchini na kutafutya solutions kwa ajili ya Maendeleo ya nchi yetu.”


Akiwasilisha salamu za wadau wa Taasisi hizo Juma Dossa alisema muunganiko ambao wamefanya na Idara ya Uhamiaji umewasaidia kupata jukwaa la kuwadilisha kero zao na pia kusikia kwa ukaribu zaidi kutoka Uhamiaji.


Warsha hiyo ni ya tatu kufanyika kwa kuwaleta wadau wa Uhamiaji kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi na kuweka mazingira rafiki ya kulinda usalama wa nchi; kwa mara ya kwanza ilifanyika mnamo mwaka 2021.


Tanzania ni sisi, tunataka muungano, ustawi, amani, kupitia ujasiri wa watu mbalimbali. Pamoja tuna nguvu, na ili kubaki na nguvu ni  lazima tushirikiane, tubadilishane mawazo ujuzi, tufunzane, tuwe na mtazamo mmoja na tusonge mbele pamoja, tuwe na maono sambamba na tusonge pamoja katika njia moja, tuwe na mdundo mmoja.

Wednesday, November 22, 2023

Warsha ya Wadau wa Uhamiaji Tanzania wafanyika Moshi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani afungua

 


Jeshi la Uhamiaji na wadau wa Uhamiaji wametakiwa kusimamia mahusiano mazuri ya Kidiplomasia katika utoaji wa Huduma za Uhamiaji kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kwa ujumla.


Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku mbili ya masuala ya usimamizi wa Uhamiaji nchini yaliyofanyika katika chuo cha Uhamiaji mjini Moshi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya amesema udhaifu wa mtu mmoja isiwe sababu ya kuharibu diplomasia ya nchi.


Mmuya ameongeza kuwa utoaji wa Huduma za Uhamiaji unapaswa uwe rafiki kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya Utalii ambao ni muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi.


Hata hivyo Katika Warsha hiyo iliyojumuisha Taasisi 100 wadau wa Uhamiaji nchini Katibu Mkuu amekemea vitendo vya rushwa kwa ustawi wa uchumi wa nchi.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala amesema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.


“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,” amesema Dkt. Makakala


Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan amesema, “Uwekezaji ambao unaofanyika Tanzania Bara msije mwekezaji huyo huyo kama anataka kwenda Zanzibar msije mkapata kigugumizi itakuwaje kibali kimetoka Tanzania Bara kiende na Zanzibari ni barua tu muwe na amani msije mkadhani atatiwa ndani.”


Aidha Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji (TRITA) SP Ignatius Mganga amesema, “Hii ni forum pekee nchini ambayo inajadili mustakabili wa shughuli za uhamiaji nchini na kutafutya solutions kwa ajili ya Maendeleo ya nchi yetu.”


Akiwasilisha salamu za wadau wa Taasisi hizo Juma Dossa amesema muunganiko ambao wamefanya na Idara ya Uhamiaji umewasaidia kupata jukwaa la kuwadilisha kero zao na pia kusikia kwa ukaribu zaidi kutoka Uhamiaji.


Warsha hiyo ni ya Tatu kufanyika kwa kuwaleta wadau wa Uhamiaji kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi na kuweka mazingira rafiki ya kulinda usalama wa nchi; kwa mara ya kwanza ilifanyika mnamo mwaka 2021.








Tuesday, November 21, 2023

Mutatembwa ahimiza uzalishaji Bora wa vipi vya TV kuhusu Utalii



Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa amewahimiza wenye dhamana ya uzalishaji wa vipindi kuzingatia viwango vya kimataifa katika vipindi vinavyoandaliwa ili malengo ya uanzishwaji yatimie


Naibu  Katibu  Mkuu huyo  ameeleza  hayo  katika  kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu iliyokutana Jijini Dodoma kwa lengo la kujadili mikakati ya kuendeleza channel hiyo ambapo ametoa wito kwa Wizara zote zinazohusika na  wadau wa Chaneli hiyo kuhakikisha zinailea.


Amesema Channel hiyo ya kujivunia inatajwa kuwa na mvuto wa kipekee ambapo mipango na mikakati yake inapaswa kusimamiwa vizuri ili kufanikisha uendelezaji wa chaneli hiyo muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa.


“Kuanzishwa kwa chaneli hii inayotengeneza vipindi na kuonesha vivutio hivi ndani na nje ya Tanzania itasaidia watalii huko waliko kujua huu utajiri wetu na kuchagua kuja kutalii nchini.  Tuzingatie uandaaji wa vipindi vyenye ubunifu na ubora vinayovutia watazamaji,” Ameeleza Bw. Mutatembwa.


Akiwasilisha taarifa ya Utendaji Kazi  wa  Tanzania  Safari  Channel  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba amebainisha kwamba kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu waliotembelea chaneli hiyo katika mitandao ya kijamii kuanzia Julai 2023 hadi Oktoba 2023.


“Wafuatiliaji katika tovuti wamefikia 154, 996 kutoka 153,873 katika mitandao ya kijamii kama vile Youtube wamefikia 5,530 kutoka 5,030, Instagram kutoka 36,800 hadi 39, 704, facebook kutoka 26,582 hadi 27,907 wakati Twitter wakifikia 1,076 hadi 1,318 na Progamu tumizi wamefikia 137,399 kutoka 137, 297,”Amefafanua Dkt. Rioba.


Kwa upande wake Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Said Shaib Mussa ameleza kwamba Chaneli hiyo inaweza kutumika kubadilisha mtazamo wa  baadhi ya watalii kwa kuonyesha vivutio, utamaduni uliopo nchini bila kuathiri dini au mila za watu wengine.


Aidha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakele amepongeza hatua kubwa inayopigwa tangu kuanzishwa kwa chaneli hiyo licha ya uwepo wa changamoto hasa zinazotokana na bajeti ambapo amesema miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni kuendelea kuunga mkono uendeshwaji wake.


Tanzania Safari Channel,ni miongoni mwa channel za Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC) ambayo ilianzishwa Desemba  15 mwaka 2018, ikiwa ni channel pekee inayojikita katika suala zima la kutangaza  rasilimali za maliasili na utalii.







Monday, November 20, 2023

PICHA: Mahafali ya 26 Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi

Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii
(WMU). Chuo hiki kinapatika mtaa wa Viwanda, Kata ya Njoro Manispaa Moshi Kilomita 3 kutoka stendi kuu ya mabasi ya Moshi Mjini.

KOZI ZITOLEWAZO 

(a) Astashahada ya awali ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu (NTA 4) mwaka mmoja

(b) Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu (NTA 5) mwaka mmoja

(c) Stashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu (NTA 6) mwaka mmoja



















Magogo kupigwa 'STOP' kusafirishwa nje ya nchi

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inaendelea na mpango kazi wa kupunguza usafirishaji wa magogo nje ya nchi  ikiwa ni mkakati wa kupunguza bidhaa ghafi za mazao ya misitu na kuongeza uwekezaji wa ndani.


Katika ujumbe wake Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas Said uliowasilishwa katika Mahafali ya 26 ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi na Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema serikali imejielekeza zaidi katika kuanzisha viwanda hivyo ni lazima kupunguza usafiri wa mazao ghafi kwendanje ya nchi.


 “Ukiangalia sasa hivi serikali mpango wake ni kupunguza usafirishaji wa magogo nje ya nchi, kupunguza bidhaa ghafi za mazaoa ya misitu kwenda nje ya nchi ili kuwekeza zaidi ndani, wale wote wanaowekeza ndani wanapewa kipaumbele cha kupata hizo bidhaa ili waweze kuzalisha hapa” amesema Dkt. Abbas


Aidha Dkt. Abbas ameongeza kuwa viwanda mbalimbali nchini vipo mbioni kupatiwa leseni  kwa ajili ya kutumia mazao ghafi ya misitu hivyo kuongeza ajira kwa vijana nchini.


“Kwa sasa tayari maeneo ya Mufindi, Njombe, wameanza kujiandaa kupewa leseni kwa ajili ya viwanda ambavyo vitatumia malighafi hizo hapa nchini badala ya kusafirisha kwenda nje ya nchi, kwa hiyo kuna muda ambao umewekwa na serikali baada ya muda huo kupita hakutakuwa na huo usafirishaji wa magogo ghafi kwasababu viwanda vingi vitakuwa vimejengwa hapa nchini na vijana wetu wataendelea kupata ajira,” amesema Dkt. Abbas katika ujumbe wake uliowasilishwa na Dkt. Kohi.


Aidha Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Deusdeit  Bwoyo alisema kuhusu mabadiliko ya tabianchi kuwa ni suala ambalo kila mtanzania anapaswa kupambana nalo kwa kupanda miti kwa wingi ambayo itarudisha sura ya dunia kama awali.


“Misitu yetu imeathirika sana, leo unaposikia kuna mioto mingi misituni, ni sababu zingine zinachangiwa na mabadiliko ya tabianchi, ukame unakuwa ni mkubwa  kuliko ilivyokuwa awali. Leo unaposikia miti imeungua ikafa ni kwasababu ya mabadilio ya tabianchi, kuna Wadudu wengine wamekuja sasa ambao sio wazuri sana na wana athiri sana misitu yetu,” amesema Bwoyo.


Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) Dkt. Lupala Zacharia alisema tangu mwaka 1976 chuo hicho kilipojengwa idadi ya watoto wa kike katika masomo ilikuwa kidogo lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka kwa baadhi ya kozi jambo ambalo linatia moyo katika kumwinua mtoto wa kike.


“Rais Samia ameifungua nchi kwa utalii imekuwa kipaumbele, watalii wameongezeka sana, fursa za utalii ndani ya maeneo ya vijana wamekuwa wabunifu; Teknolojia ya viwanda vya misitu ilitawaliwa sana na mfumo dume , kutokana na hamasa iliyofanywa imehamasisha sana watoto wa kike kujitokeza kuziona fursa mbalimbali, kwa sasa kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa vijana wa kike kupenda kusoma masomo ya yetu,” amesema Dkt. Lupala.


Kwa upande wa wahitimu wa ngazi ya cheti na diploma walisema juhudi zinatakiwa kwa ajili ya kubadili miundombinu ikiwamo kuachana na teknolojia ya zamani katika masomo na kwenda na wakati ili kufikia malengo.


“Kwa upande wa mashine zetu, mashine ambazo tunazitumia ni mashine ambazo tayari zimeshapitwa na wakati kutokana na teknolojia kukua, tunapokwenda kwenye mazoezi ya vitendo, Unakuta masomo ya darasani tumefanya na mashine ambayo ni ya zamani, lakini tunapokwenda kwenye mazoezi ya vitendo tunakutana na mashine zingine ambazo ni mpya,” amesema Edina Kweka, mhitimu wa ngazi ya Astashahada Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi.


Wahitimu 200 wa astashahada na stahada walihitimu mafunzo katika Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi.