Sunday, February 26, 2023

Nestory Njatile Mwangoka na Kili Marathon 2023

Mzee Nestory Mwangoka akiwa mjini Moshi baada ya kushiriki mbio za Kili Marathon 2023 kilometa 21 akitumia dakika 100 kumaliza. (Picha zote na Kija Elias)

Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Kilimanjaro Deodatus Ako akimpongeza Mzee Mwangoka baada ya kufika ofisini hapo alipoanzia kazi yake. 

 

Safari ya Maisha ni ya pekee na Kila mtu hupitia mambo kwa majira yake unaweza kusema  “Kila Mtu na Wakati wake”.

Unapojua safari ya maisha ni ya upekee basi unajifunza kufurahia hatua zako kila inapoitwa leo.

Utafurahia mafanikio unayofanikiwa, utafurahia unavyopitia changamoto na magumu maana unajua ni sehemu ya hadithi ya maisha yako.

Hivyo ndivyo Mzee Nestory Njatile Mwangoka alivyofurahia kukimbia kilometa 21 za Kili Marathon 2023 iliyofanyika mjini Moshi mnamo Februari 26, 2023.

Mwangoka (64) alikuwa imara katika mbio hizo akikimbia kwa dakika 100 sawa na saa moja na dakika 40.

Kinachovutia kwa mzee huyo ni pale anapokusimulia maisha ya mjii wa Moshi ulivyokuwa sehemu ya mafanikio ya maisha yake.

Mzee Mwangoka anasema, “Nimekuja Kilimanjaro kushiriki mbio za marathon kwasababu mwaka 1985 nilikuja hapa Kilimanjaro  nikiwa kijana mdogo na kuanza kazi hapa katika Shirika la Posta.”

Mwangoka anakumbusha kuwa wakati akitua katika viunga vya Moshi hakuwa kufikiri kama siku moja kutafanyika mbio za Kimataifa na kuvuta mamia ya watu kote ulimwenguni kama ilivyo sasa.

Mfanyakazi huyo wa zamani wa Shirika la Posta ameweka rekodi yake binafsi kwa furaha tele kwa mara ya kwanza alipokimbia mbio hizo akitokea mjini Mbeya.

“Nimeonyesha kwamba wazee tunaweza, natoa wito kwa wafanyakazi kote nchini kushiriki mazoezi kusaidia kuweka miili yetu vizuri na kuondokana na maradhi,” anasema Mwangoka.

Mwangoka anaweka bayana kuwa mbio za mwaka huu ni za kwanza katika miaka 21 ya Kili Marathon, licha ya ushiriki wake wa mbio nyingine za kilometa 21 zinapofanyika nchini hususani mkoani kwake Mbeya.

“Shukrani zangu za dhati ni kwa Shirika la Posta Tanzania kwa kuniwezesha kushiriki mbio za mwaka huu ni mfano wa kuigwa kwa uongozi mzima kwa maendeleo ya taifa,” aliongeza Mwangoka.  

Licha ya ujio wake katika Kili Marathon 2023, Mwangoka hakusita kufika katika Ofisi za Shirika la Posta mkoa wa Kilimanjaro ambako alikutana na Meneja wa Posta mkoani humo kwa sasa Ndugu Deodatus Silaa Ako.

Ako aliongeza, “ Ari na Hamasa alio nayo mzee Mwangoka ni somo kwetu, hata mwaka huu tumeshiriki mbio hizo hii imetokana na mwongozo ambao Shirika letu la Posta limekuwa na mwongozo kwa wafanyakazi wake kufanya mazoezi kila Ijumaa baada ya masaa ya kazi.”

Meneja huyo alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi pamoja kuimaraisha umoja wa kitaifa na maeneo ya kazi.”

Mataifa 55 yameshiriki mbio hizo mwaka huu katika kilometa 5, 21k na 42k, huku Waziri wa Maliasili na Utalii Mohammmed Mchengerwa akiwa mgeni wa heshima.







0 Comments:

Post a Comment