Madiwani wa wilaya ya Moshi wameiomba halmashauri ya wilaya hiyo kutumia mifumo ya kielektroniki ikiwamo matumizi ya vishikwambi ili kupunguza gharama za maandalizi ya makabrasha ya vikao.
Hatua hiyo inajiri ikiwa ni mpango kazi wa madiwani wa Halmashauri ya Moshi kutaka kuwapunguzia mizigo wananchi waliowapa ridhaa ya kuongoza maeneo yao.
Pia madiwani hao wametaka baada ya taarifa za vikao kuandaliwa katika mfumo wa kidigitali watumiwe kwenye simu zao ili wasomee wakiwa majumbani mwao kabla ya kuingia kwenye vikao.
Wakichangia hoja kwenye kikao maalum kilichoketi kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya rasimu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2023/2024, iliyowasilishwa na Afisa Mipango wa halmashauri hiyo David Mgonjwa.
Madiwani hao walitoa hoja ya kutoipisha bajeti hiyo na kuomba iweze kurudishwa kwa ajili ya kuandaliwa upya ndipo waweze kuipitisha kwani bajeti hiyo haikuzingatia vipaumbele ambavyo madiwani wamekuwa wakivileta kwenye baraza hilo kutoka kwenye kata zao.
Akichangia hoja hiyo Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wakili Wilihard Kitary alisema bajeti iliyowasilishwa na Afisa Mipango kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, haikuzingatia uhitaji wa wananchi hivyo ni vizuri waatalam wanapoandaa bajeti kama hiyo waweze kuzingatia vipaumbele ambavyo vimekuwa vikiletwa na madiwani hao kutoka kwenye kila kata.
Akizungumzia suala la makabrasha Kitary alisema kiasi cha shilingi milioni sita zimekuwa zikitumika kwa kikao kimoja kwa ajili ya kuandaa taarifa za vikao vya halmashauri kwa kutumia makabrasa ya vikao hivyo ili kuweza kupunguza gharama za maandalizi ya makabrasha hayo ni vizuri vikaweza kununuliwa vishikwambi.
“Kuandaa makabrasha kwenye kikao kimoja ni zaidi ya shilingi milioni sita zimekuwa zikitumika kwa kila kikao kimoja, nina shauri kwenye bajeti hii kama tunataka tuipitishe hapa kuwepo na bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vishikwambi ndipo kura yangu nitaweza kuitoa,”alisema Kitary.
Diwani wa Tarafa ya Vunjo Magharibi Jenipha Nyambo, alisema limu moja ya karatasi inauzwa shilingi 20,000 kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya halmashauri, lakini pia ziko gharama mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika ikiwemo mafuta ya gari kwa ajili ya kusambaza makabrasha hayo kwa madiwani, jambo ambalo halmashauri imekuwa ikipata hasara kubwa.
“Madiwani tuko 43 kama halmashauri itaweza kununua vishikwambi itaweza kutumia kiasi cha shilingi milioni 21.5 kuliko hivi sasa kila kikao kimoja inatumia kiasi cha shilingi milioni sita kwa ajili ya maandalizi ya kikao kimoja,” alisema Nyambo.
Diwani wa Kata ya Kibosho Kati Bahati Mamboma, alisema madiwani wamekuwa wakiwasilisha kila baada ya miezi mitatu taarifa za vipaumbele ambavyo wananchi wanavipendekeza kwenye kata na madiwani kuziwasilisha kwenye vikao vya baraza lakini havifanyiwi kazi.
0 Comments:
Post a Comment