Katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini Mbunge wa Mkoa wa Kilimanjaro anayewakilisha Wanawake, Esther Maleko, amechangia kiasi cha shilingi milioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira iliyoko wilaya ya Moshi mkoani humo.
Msaada huo wa madawati ni sehemu ya jitihada za Mbunge huyo katika kusaidia jamii ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma kwa utulivu.
Katika ziara yake aliyoifanya Februari 16, 2023 Moshi Vijijini Mbunge Esther Maleko alisema ameamua kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia kiasi cha Shilingi milioni 1.6 kwa ajili ya kununua madawati ili watoto waweze kusoma vizuri.
“Katika ziara yetu ya kukagua Ilani ya CCM tumekagua miradi kadhaa ukiwemo mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa manne, mabweni mawili na bwalo moja kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira, tumeona kazi kubwa iliyofanyika Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa kiasi cha Sh miloni 400 na mimi katika kumuunga mkono nimeguswa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa madawati katika shule hii,” alisema.
“Elimu yetu ya sasa ni bure ili kuwawezesha watoto wote kusoma lakini sera hii imekuja na changamoto zake ambazo jamiii ni lazima tushirikiane kuzipatia ufumbuzi, kuna uhaba wa madawati, nyumba za walimu na vitendea kazi vingine,”amesema.
Akizungumzia changamoto ya uzio katika shule hiyo Mbunge Esther Maleko amesema atakwenda kushirikiana na uongozi wa shule hiyo ili kuweza kutatua changamoto hiyo ili waweze kumalizia ujenzi wa uzio huo.
Kuhusu suala la mikopo Mbunge Maleko amewataka kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kwa makundi ya Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Cyril Mushi alimpongeza Mbunge Esther Maleko kwa kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo na kuwa Mbunge anayewajibika kikamilifu kwa jamii yake.
Nimpongeze Mbunge Maleko kwa kazi kubwa anayoifanya kupigania
maendeleo kwenye wilaya ya Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla, ni
matarajio yangu mchango wako wa madawati haya yatakwenda saidia kuboresha
mazingira ya kujifunzia kwa
wanafunzi na kuchochea ongezeko la ufaulu.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori, amempongeza Mbunge Maleko kwa msaada huo na kumhakikishia kuwa madawati hayo yatatunzwa vizuri ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
“Utaendelea kukumbukwa daima kwa msaada huu ambao una manufaa
makubwa kwa watoto wetu,”amesema DC Makori.
0 Comments:
Post a Comment