Madiwani wa Halmashauri ya Moshi katika picha ya pamoja kwenye Maporomoko ya Materuni |
Vivutio vya
utalii vinavyopatikana Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjro
vimetakiwa kuboreshwa zaidi hususan kwenye miundombinu ya barabara za kuelekea
kwenye vivutio hivyo, pamoja na kuwa na miundombinu ya vyoo na maeneo ya
kutupia taka nguvu.
Ushauri huo
umetolewa hivi karibuni na madiwani
wa Halmashauri hiyo waliotembelea
kivutio cha utalii cha maporomoko ya
maji Materuni kilichopo Kata ya Uru Mashariki, wilayani humo ikiwa ni sehemu ya
ziara ya kuhamasisha utalii wa ndani.
Wakizungumzia
kuhusu lengo la ziara hiyo Diwani wa
kata ya Old Moshi Mashariki Super Macha, Diwani
Kata ya Njia Panda Loveness
Mfinanga, na Diwani Kata ya Mwika Kaskazini Samuel shao, walisema ziara
hiyo ya siku moja ilikuwa imejikita kuhamasisha utalii wa ndani sanjari na kubaini vyanzo vipa vya mapato ya
halmashauri hiyo.
Katika ziara
hiyo Madiwani hao wameshauri mapato ya asilimia 40 yanapatikana katika eneo la
maporomoko ya maji Materuni yarudi kuboresha miundo mbinu ya barabara vyoo
pamoja na sehemu ya kutupa taka ngumu ili wageni wanaofika kutembelea eneo hilo
waweze kuvutiwa na mandhari nzuri iliyopo.
Diwani wa
Kata ya Uru Kusini Wilhard Kitali Diwani alisema upo umuhimu wa mkubwa wa
halmashauri ya Moshi, kuhakikisha vivutio vyote vya utalii vilivyopo wilayani humo vinatangazwa.
Kitali
alisema halmashauri ya Moshi ndio benki
na kitovu cha utalii katika mkoa wa Kilimanjaro, kwani inavyo vyanzo vingi vya
utalii ikiwemo soko la watumwa, mapango, mti uliotumika kumnyongea Mangi Meli,
malango ya kupandia mlima Kilimanjaro, mahandaki na mti mrefu Afrika kama vitatangazwa mapato ya halmashauri kwa
upande wa utalii yataweza kuongezeka zaidi.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Moris Makoi alisema ziara hiyo ilikuwa
imelenga kuvitambua vivutio ili kuongeza mapato ya halmashauri sambamba na
kuhamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kuvitembelea vivutio
vinavyowazunguka kwenye maeneo yao.
Aidha Makoi
alisema halmashauri hiyo itaanzisha program maalum ya mafunzo kwa vijana
wanaojishughulisha na kuwatembeza wageni
(Waongoza watalii) ili waweze kuwaelezea vizuri historia ya wilaya ya
Moshi na namna ilivyo na vivutio vingi vya utalii ili wageni wanapofika
Kilimanjaro kabla ya kupanda mlima huo waweze kwanza kuvitembelea vivutio hivyo
ikiwemo mti uliotumika kumnyongea Mangi mengi.
Awali Ofisa
mtendaji wa Kijiji cha Uru Mashariki Robert Soka, aliwaeleza madiwani hao
kuwa maporomoko ya maji Materuni ni moja
ya maporomoko ya maji yanayotoka katika mto Mware ambapo kimekuwa kivitio kibwa
cha wageni kutoka nje kutembelea eneo hilo.
Alisema
uwepo wa maporomoko hayo ya maji ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka
shilingi laki sita hadi laki nane kutokana na wageni wengi kutoka nje ya nchi
kuja kutembelea kivutio hicho huku takribani ya wakazi wa kijiji hicho 2,000
wanajishughulisha na shughuli za kuwatembeza watalii hao.
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dk. Alex Kazura alisema katika bajeti ya mwaka
ujao wa fedha 2023-2024 halmashauri imejiwekea mkakati wa kuongeza ukusanyaji
wa mapato kutoka sekta ya utalii, hivyo watakwenda kuviboresha vivutio hivyo
ili kuwa na mazingira mazuri ya watalii kupenda kuyatembelea.
Wilaya ya Moshi imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii wa aina mbalimbali ndiyo maana wilaya hiyo inaitwa ni Benki ya vivutio vya utalii ambavyo bado havijatangazwa kikamilifu ili kuwa moja ya vyanzo vya mapato ya halmashauri hiyo.
0 Comments:
Post a Comment