Kampuni
ya kuzalisha sukari ya TPC Limited ya mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwa
kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali kutoka Uholanzi FT Kilimanjaro
(FTK) inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 kila mwaka katika kusaidia
mchakato wa maendeleo ya jamii, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa elimu.
Hayo
yameelezwa katikati ya juma na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya FTK,
Jaffary Ally, alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi
hiyo kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC), mjini
Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema zaidi ya asilimia 50 ya fedha zinazotengwa
kila mwaka, zinatumika kusaidia sekta ya elimu katika maeneo yanayozunguka
kiwanda cha TPC Limited, hatua inayolenga kupongeza jitihada za serikali
zinazolenga kuboresha elimu nchini.
Ally
aliendelea kusema kuwa, taasisi hiyo ilitumia jumla ya milioni 300 kwa ajili ya
kuboresha miundombinu ya elimu katika shule ya sekondari Chewe iliyopo wilayani
Moshi, ambayo alisema kwa sasa ina wanafunzi 324, ambapo amesema mradi uliotekelezwa katika shule hiyo ulihusisha
ujenzi wa madarasa manne mapya, majengo mawili ya vyoo, jengo la jiko na
ununuzi wa madawati 120.
“Miradi
mingine inayohusiana na elimu ni pamoja na ujenzi wa shule ya msingi Miwaleni
uliogharimu shilingi milioni 73
ukarabati wa jengo la walimu wa shule ya sekondari Langasani uliogharimu
shilingi milioni 26 pamoja na ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa na ununuzi
wa madawati 25 kwa shule ya msingi Chemchem kwa gharama ya shilingi milioni 3.5,”alisema.
Ally
ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC Limited (Utawala) aliendelea kusema
kuwa mchango mwingine ni pamoja na ukarabati wa madarasa manne ya msingi katika
shule ya msingi Kiungi uliogharimu jumla ya shilingi milini 59 pamoja na ukarabati wa vyumba vya
madarasa na ujenzi mpya katika shule ya msingi ya Mawalla, mradi ambao amesema
gharama yake ilikuwa ni shilingi milioni 63.
Alifafanua
kuwa pamoja na hayo, FTK pia inachangia
ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao katika ngazi ya
Stashahada na Shahada ya Kwanza katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kwa
kuwasaidia katika kulipa ada, gharama za malazi na stationary huku wazazi na
walezi wakichangia chakula na mengine muhimu.
Alisema
katika mwaka wa masomo uliopita FTK ilisaidia jumla ya wanafunzi 41, msaada
ambao ulikuwa wa shilingi milioni
165,779,150/ pia jumla ya walimu 37
walipewa kazi ya kufundisha programu ya kujitolea katika shule za msingi
tofauti ambapo jumla ya shilingi milioni 81.6
zilitumika kuwezesha walimu hao kwenye programu hiyo ya kujitolea ya kusaidia kufundisha.
Aidha
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya FTK, Jaffary Ally, aliendelea kusema kuwa mbali na kuchangia
sekta ya elimu, FTK pia iliwezesha programu ya miezi miwili ya uhamasishaji wa
unyanyasaji wa watoto ambayo iligharimu shilingi milioni 7 programu ilianza kwa
kikao cha uwezeshaji kikihusisha maofisa wa tawala ngazi ya wilaya, viongozi
waliopo ngazi ya uongozi wa kata za Arusha Chini, Kahe na Msitu wa Tembo,
pamoja na viongozi wa vijiji vinavyozunguka kampuni ya TPC Limited. , maofisa
wa jeshi la polisi, wawakilishi kutoka taasisi za dini na wadau wengine katika
jamii.
0 Comments:
Post a Comment