Mwandishi wa vitabu wa Ufaransa Charles de Brosses (1707-1777) analitaja kwa mara ya kwanza eneo la Kusini mwa Bahari ya Pasifiki kama Polynesia, ikiwa na maana ya eneo linaloundwa na visiwa 1,000.
De Brosses katika kitabu chake cha “Histoire des navigations aux terres australes, contenant ce que l'on sait des moeurs et des productions des contrées découvertes jusqu'à ce jour (1756)”, kinaweka bayana watu wa ukanda huo na utamaduni wao.
Miongoni mwa visiwa ni New Zealand, Tonga, Samoa, Tuvalu, French Polynesia, Norfolk na Hawaii; eneo hilo lina historia kubwa ya Miwa/Sukari.
Unafahamu kuwa sukari ni miongoni mwa bidhaa za mwanzo kutajwa tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia hii? Sasa kwa taarifa yako ni kwamba historia yake inaanza miaka 10,000 iliyopita katika ardhi ya Polynesia.
Unajua kuwa Miwa ni zao la kitropiki ambalo hustawi hadi kufikia kimo cha hatua 20, na kuvunwa ndani ya miezi 12?
Mwaka 8000 K.K, zao hilo lilionekana katika ardhi ya Polynesia, lilistawishwa kienyeji tu, sio kwa madhumuni ya kibiashara.
Familia za ukanda huo zilikuwa na utaratibu wa kustawisha kwa ajili ya matumizi ya ndani tu, mfumo ambao hadi miaka ya sasa kwenye maeneo ya vijijini nchini Tanzania unaweza kuona miwa ikistawishwa pembezoni mwa nyumba.
Kutoka hapo tamaduni mbalimbalimbali ulimwenguni zilipoanza kufunguka na kuanza kutafuta malighafi zao ndipo zao hili lilipopata umaarufu.
Kwa mfano enzi za ustaraabu wa Warumi na Wayunani, walitumia miwa katika mfumo wa sukari kwa matibabu, hususani kwa watu waliokuwa na matatizo ya mmeng’enyo wa chakula na matatizo ya tumbo kwa ujumla. Pia walitumia kwa kutibu vidonda.
Ustaarabu wa Milima ya Himalaya kwa upande wa mashariki ikiwa na maana ya China, wenyewe mnamo mwaka 640 BK walianza kulima mashamba makubwa ya miwa wakitumia teknolojia waliyoipata kutoka Ustaarabu wa Magharibi mwa Milima ya Himalaya (India).
Miaka ile ya 1096-1099 kundi kubwa la wapiganaji waliokuwa wakirudi barani Ulaya walibeba zawadi ikiwamo miwa/sukari, ambapo watu wa Ulaya walikuwa wakiita Chumvi Tamu.
Mnamo mwaka 1390, suala la miwa/sukari lilipiga hatua nyingine kubwa kwa kuanza kuchuja miwa ili kupata juisi, yaani juisi ya miwa.
Katika visiwa vya Madeira huko Ureno kati ya mwaka 1455 na 1480 kwa mara ya kwanza barani Ulaya kulionekana mashamba makubwa ya miwa . Mwishoni mwa miaka hiyo, inaelezwa kuwa meli 70 zilitia nanga katika kingo za kisiwa cha Madeira kwa ajili ya biashara ya miwa na sukari.
Kuitengeneza miwa hiyo kwa viwango vya juu na usambazaji kwingineko ilifanyika katika mji wa Antwerp nchini Ubelgiji.
Mnamo karne ya 15 kwa mara ya kwanza miwa ilionekana huko Amerika na ilianza kutua nchini Brazil ambako Wafanyabiashara wa Kireno walifika huko. Muwa wa kwanza ulipandwa nchini Marekani ikiwa ni zawadi kutoka kwa Gavana wa Visiwa vya Canary kwa mpelelezi Christopher Columbus.
Mnamo mwaka 1813 mgunduzi Edward Charles Howard alipiga hatua kubwa katika uzalishaji wa miwa na sukari pale alipogundua njia ya kuichakata miwa kwa moto.
Maboresho yaliendelea katika maeneo mbalimbali ikiwamo uvunaji ambapo mashine za uvunaji (16 whole-stalk harvesters) zilipotumika huko Louisiana mnamo mwaka 1938.
Matumizi ya mashine hizo yalikuja kutokana na ukosefu wa watu wakati na baada ya Vita vya Pili Dunia (1939-1945), ilipofika mwaka 1946 huko Louisiana mashine hizo zilifikia 422 na kufanya uvunaji wa miwa kufikia asilimia 63.
Kwa sasa zaidi ya nchi 80 zinalima miwa huko nchini Marekani majimbo ya Louisiana,Florida na Texas ndio maarufu kwa kilimo cha zao hilo.
Nchini Tanzania; mikoa ya Kagera, Morogoro na Kilimanjaro ndio maarufu kwa kilimo cha miwa ambapo makala haya yatajikita katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kunakopatikana mashamba makubwa ya miwa ya TPC.
Kwa miongo kadhaa sasa maeneo ya karibu na mashamba hayo ya TPC unapowadia msimu wa uvunaji wa miwa ilikuwa ni kero kubwa kutokana na moshi na majivu kuharibu mwonekano na hali ya hewa kutokana na uvunaji wa kutumia moto, ambao mashamba ya miwa yalikuwa yakichomwa na kusababisha uharibu wa mazingira na ikolojia yake.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC Jaffary Ali anasema uvunaji wa miwa duniani kote ni kwa kutumia wanadamu, muwa lazima uchomwe moto kwa ajili ya kumpa fursa mvunaji kuingia kuondoa wanyama wakali na wadudu ambao wanaweza kumdhuru wakati wa uvunaji.
“Utaratibu huo hutumika duniani kote, kutokana na mabadiliko ya mazingira na sheria za mazingira zinazohitajika kupunguza uchafuzi wa mazingira wavunaji wakulima wengi wameanza kutumia teknolojia ya kuvuna miwa bila ya kuichoma tukiwamo sisi,” anaongeza Jaffary Ali.
0 Comments:
Post a Comment