Friday, February 17, 2023

Wakazi wa Njiapanda-Moshi waepukana na adha ya maji, MUWSA yakamilisha

 

Mbunge anayewawakilisha Wanawake Mkoa wa Kilimanjaro Esther Maleko  akinywa maji safi na salama baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa  Mazingira (MUWSA) kukamilisha mradi huo kwa wakazi wa Njiapanda, Moshi Vijijini ambao utawahudumia takribani wakazi 14,000.


Kukamilika kwa mradi wa maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa  Mazingira (MUWSA), kunawafanya taribani watu 14,000 wa kata ya Njia Panda, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kuepukana na adha ya kufuata maji umbali mrefu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa  Mazingira (MUWSA). (MUWSA) Mhandisi Kija Limbe katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji safi na Usafi wa Mazingira wa taasisi hiyo Mhandisi Innocent Lugodisha, kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Moshi Vijijini.


"Kutokana na mafanikio iliyoyapata katika kutekeleza shghuli zake Moshi Mjini, MUWSA iliongezewa eneo la kutoa huduma ambapo ilijumuisha mji mdogo wa Himo na Njia Panda pamoja na kata zingine 12 katika halmashauri ya wilaya ya Moshi", alisema.

Alisema "Hadi sasa Serikali imesha elekeza  kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimmbali ya kuboresha huduma ya maji katika maeneo haya mapya, ambapo zaidi ya shilingi bnilioni 2.3 zimetumika kutekeleza mradi wa maji wa kata ya Njia Panda", alisema Mhandisi Lugodisha.

Aliendelea kusema kuwa mradi  huo unatarajiwa kuhudumia takribani watu 14,000 na kwamba una uwezo wa kuzalisha jumla ya lita za ujazo  milioni 2.5 kwa siku, ambapo alisema tayari umeshakamilika kwa asilimia 100.

"Kazi zilizofanyika wakati wa kutekeleza mradi huu ni pamoja na ujenzi wa chemba ya kukusanyia maji, ujenzi wa ofisi pamoja na control panel room pamoja na ujenzi wa storage tank lenye ukubwa wa mita za ujazo 100 katika eneo la Mabungo", alisema.

Alisema kazi nyingine ilikuwa ni ile ya ununuzi wa bomba, uchimbaji wa mtaro pamoja na ulazi wa bomba wenye urefu wa kilomita 13.6 kuanzia eneo la Miwaleni hadi kwenye matangi yaliyoko eneo la Kilema Pofo.

"Kazi zingine zilikuwa ni zile za ujenzi wa njia kuu ya umeme pamoja na kuweka transforma eneo la Miwaleni na Mabungo, kununua na kufunga pumps za kusukuma maji eneo la Miwaleni pamoja na Mabungo Buster Station pamoja na ujenzi wa vyoo eneo la mradi ya Miwaleni na Mabungo", alisema.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa  ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini  kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM,  Mbunge wa Mkoa wa Kilimanjaro anayewakilisha kundi la Wanawake, Esther Maleko, ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha hizo jambo ambalo alisema litawapa wananchi wa eneo hilo hususan wanawake muda wa kufanya shughuli nyingine badala ya kutumia muda mwingi kufuatillia maji mbali.

Aidha aliupongeza uongozi wa MUWSA kwa kuutekeleza mradi huo kwa kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa ambapo alisema utekelezaji huo unatarajiwa kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu ujao.

Aidha Diwani wa Kata ya Njia Panda Loveness Mfinanga alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa  maji Miwaleni -Njia Panda, umewezesha kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya maji iliyokuwepo katika kata hiyo kwa kipindi kirefu.

“Naishuikuru Serikali kupitia  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa  Mazingira (MUWSA) kwa jitihada za kutekeleza mradi huu wa maji na kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama  kwa wakati,”alisema Loveness.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Cyril Mushi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo wa Maji Miwaleni Njia Panda, kuondoa changamoto kubwa ya  maji  kwa wananchi waKata ya Njia Panda.

“Mradi huu  umeondoa changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa eneo hili,  niwaombe wakazi wote  eneo hili kuwa waangalifu wa miundombinu ya maji kwa kuitunza na kuisimamia ili huduma  hii ya maji iendelee kupatikana muda wote,” alisema Mushi.

Naye  Mkuu wa wilaya ya Moshi Kisare  Makori, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa eneo la Njia Panda ambapo alielezea matumaini yake ya kuwa miradi mingine ya maji inayoendelea kutekelezwa itakamilika kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na miradi inayotekelezwa na Serikali.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inalenga kufikisha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 90 ya maeneo ya vijijini ya idadi ya watu watakaopata maji safi na salama ifikapo mwaka 2025 sambamba na kuimarisha uwezo wa kusimamia rasilimali maji.


 






 

0 Comments:

Post a Comment