TEMEKE, DAR ES
SALAAM
MKAZI wa Buza wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam Isaack
Ernest (16), miongoni mwa wahalifu wa kundi la ‘Panya Road’ amefufuka katika
Chumba cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Temeke siku chache baada ya
kufikishwa hapo kama maiti.
Tukio hilo la aina yake lililotokea siku chache baada ya
kijana huyo kufikishwa hospitalini hapo kutokana na kupata kipigo kutoka kwa
wananchi wenye hasira kali baada ya kuhusika matukio ya kuiba, kujeruhi na kuharibu
mali.
Oktoba 15 mwaka huu katika maeneo ya Sabasaba, Mbagala
vijana sita walikamatwa na kushambuliwa na wananchi kwa tuhuma za kupora watu
waliokuwa wakipita maeneo hayo.
Kikundi hicho cha vijana kilichojitambulisha kwa jina la
Taifa Jipya kilianza kufanya uhalifu huo baada ya kumalizika kwa Tamasha la
Kuinua Vipaji vya Muziki liliandaliwa na Clouds FM katika viwanja vya Zakheim
jijini hapa.
Katika tukio hilo mkazi wa Yombo na mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Nuruakim Kelvin Nyambocha (14), aliuawa kwa kuchomwa moto huku
watano wakijeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hicho.
Aidha miongoni mwao mkazi wa Kilungule Seleman Hamis (16),
alifariki dunia akiwa katika chumba cha upasuaji mdogo katika Hospitali ya
Wilaya ya Temeke huku mkazi wa Buza kwa Lugenge ambaye ni fundi gereji Faraji
Suleiman (19) alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu
zaidi ambako yupo hadi sasa.
Akisimulia mkasa huo jana jijini hapa katika Kituo cha
Polisi cha Chang’ombe Isaack (miongoni mwa waliopokea kichapo na kudhaniwa kuwa
amekufa kisha kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya
Wilaya ya Temeke) akiwa mikononi mwa polisi jinsi alivyoshawishiwa kujiunga na ‘Panya
Road’ hadi kukutwa na masahibu hayo
anasimulia kuhusu namna ‘Panya Road’ walivyomshawishi
kujiunga nao.
“Mimi nakaa Buza, Jumamosi tulikuwa Zakheim kulikuwa na shoo
tulikwenda na wenzangu wakati wa kuondoka, wakaniambia kama kula tunakula mimi
nikawaambiaje, kula mi sijiwezi kama kula kuleni,” alisema Isaack kuongeza
“Wakaanza kuniambia kuwa mimi nina under fear (ninaogopa),
na wakasema na tukila hatukugei mali nikwaambia kama kula kuleni mi sijiwezi…mi
nikapita njia nyingine na wenyewe kivyao, kila walipopita walikuwa wanaiba.”
Pia kijana huyo mwanafunzi wa kidato cha tatu katika
sekondari ya Lumo jijini hapa anaendelea kusema, “Walivyopita njia nyingine
mmoja wakamwitia kelele za mwizi, akapigwa asa mi nikawa nipo ng’ambo nyingine,
nikamwona mwingine wengine wakavuka ng’ambo nilikuwapo mimi na kutangulia
wengine wakaangukia bondeni, sasa nikaonekana mimi wakaniitia kelele za mwizi
kustuka nikajikuta nipo mochwari.”
Isaack anahitimisha kwa kusema, “Mpaka dakika hii nipo
hapa…sitarudia vitendo vya wizi kwani nilishawakataa na kwasababu mimi bado
mwanafunzi…bado napenda maisha yangu.”
Kwa upande wake mzazi wa Isaack ambaye ni mjumbe wa Serikali
ya Mtaa wa Buza anasema hakuwahi kumuona kijana wake akijihusisha na masuala ya
wizi kwani katika mtaa wao wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi
kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
JESHI LA POLISI
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa
Temeke Gilles Muroto alisema kijana alizindukia mochwari yupo mikononi mwao na
baada ya mahojiano ya muda mrefu amewasaidia kujua mtandao wa kundi lao.
“Kijana huyu ametusaidia kuwapata vijana wengine kumi na
tunao tunatarajia kuwapandisha mahakamani kujibu mashtaka yao,” alisema Muroto.
Aidha Muroto alisema katika msako walioufanya wamewakamata
vijana 16 wakiwa na mapanga na bendera ya kundi lao iliyochorwa na kuandikwa ‘Taifa
Jipya…Makali yanaendelea…”
Hata hivyo kamishna huyo alisema wamewaita wazazi wa watoto
hao na wamefika katika makao makuu ya Kipolisi Temeke jana ambao watapandishwa
mahakamani muda wowote wiki hii kutokana na kukiuka sheria ya watoto ya mwaka
2009 kifungu cha saba hadi tisa.
Aidha Muroto alisema kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinatoa
adhabu kwa mzazi atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na
akitiwa hatiani atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh.
Milioni 5.
Imeandikwa katika Gazeti la Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na. 4337 Jumatano Oktoba 19, 2016 Uk. 2
0 Comments:
Post a Comment