NA
MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Mwanzo ya Ilala imemhukumu Muuza maji mkazi wa
Keko jijini Dar es Salaam Emmanuel Issa (38) kifungo cha miezi minane jela kwa
kosa la kuiba miti 12 aina ya mchikichi.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Asha Mpunga alisema mshtakiwa
alitenda kosa hilo Agosti 22 mwaka huu katika mtaa wa Ohio kwenye Hoteli ya
Serena.
Aidha Mpunga alisema ushahidi unaonyesha mtuhumiwa aliuiba miti
huo huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba mti huo ulikuwa na
thamani ya Sh. 1,800,000.
Awali mshtakiwa aliiomba mahakama isimpe adhabu kutokana na
kuwa bado ni mtafutaji.
Kwa upande wake karani wa mahakama hiyo Kassim Mtanga alidai
mshtakiwa hana kumbukumbu ya makosa hivyo adhabu atakayopewa iwe fundisho kwake
na kwa jamii.
Katika kesi nyingine Hamis Mtembezi (36) amehukumiwa kwenda
jela mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujeruhi kinyume cha
sheria.
Hakimu alisema mshtakiwa alimjeruhi Samweli Wambura kwa
kumkata na kisu eneo la mkononi Agosti 1 mwaka huu.
Awali wakati alipofikishwa kwa mara ya kwanza alikana
kutenda kosa hilo.
Aidha mshtakiwa Jerry Mushi (22) amehukumiwa kwenda jela
mwaka mmoja kwa kosa la kujeruhi na akimaliza atapaswa kulipa Sh. 250,000.
Mpunga alisema mshtakiwa akiwa eneo la Bilicanas, Ilala
Julai 31 mwaka huu alimjeruhi mlalamikaji Juma Hamis sehemu za tumbo kwa
kumkata na chupa na kumsababishia maumivu.
Hakimu alisema ushahidi wa PF3 ulithibitisha kuwa mshtakiwa
alimjeruhi mlalamikaji sehemu za tumbo.
Awali kabla ya kusomewa hukumu yake mshtakiwa alijitetea
kuwa ni baba wa familia na watoto wawili na wanamtegemea.
0 Comments:
Post a Comment