Thursday, October 20, 2016

‘Scorpion’ afunguliwa upya mashtaka, abadilishiwa hakimu

NA JABIR JOHNSON
Salum Njewete 'Scorpion' akitolewa nje ya ukumbi wa mahakama ya Wilaya ya Ilala
jijini Dar es Salaam jana chini ya ulinzi mkali baada ya kusomewa mashtaka upya.


MSHTAKIWA wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Salum Njwete (34) ‘Scorpion’  amefutiwa shtaka lake la awali na Mahakama ya Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam jana kisha kesi yake kuanza upya.
Hata hivyo kuanza kwa shtaka lake jipya kumeenda sanjari na kubadilishwa hakimu wa kuisikiliza kesi hiyo.
Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore aliiomba mahakamani kuwa upande wa mashtaka hawezi kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha Sheria Na. 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hakimu aliridhia ombi la mwendesha mashtaka kufuta shtaka lililokuwa likimkabili Scorpion.
Shtaka jipya ambalo Scorpion anashtakiwa nalo ni unyang’anyi wa kutumia silaha alilolitenda Septemba 6 mwaka huu Buguruni Shell kisha kumchoma na kisu mlalamikaji Said Ally Mrisho machoni, mabegani na tumboni.
Awali Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimpora mlalamikaji ambaye hakuwepo mahakamani hapo vitu vya thamani na fedha taslimu vyote vikiwa na jumla ya Sh. 476,000.
Mshtakiwa alikana kuhusika na kosa hilo.
Hakimu alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Na. 148(5)(a)(i) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mshtakiwa hawezi kupata dhamana hivyo atarudishwa mahabusu.
Ikumbukwe Septemba 23 mwaka huu, Scorpion alipandishwa mahakamani hapo na kufunguliwa shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya kifungu cha Sheria Na. 287A cha makosa ya jinai.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Scorpion aliyejipatia umaarufu ‘Mtoboa Macho’ mnamo Septemba 6 mwaka huu maeneo ya Buguruni Shell jijini hapa alimvamia na kumpora mali na fedha taslimu muathirika Said Ally Mrisho kisha kumchoma na kisu katika macho, mabegani na tumboni huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kesi hiyo ilikuwa chini ya Hakimu Mkazi Adelf Sanchore na Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola ambao wameisimamia hadi Oktoba 19 mwaka huu.

HALI ILIVYOKUWA MAHAKAMANI
Umati wa watu walikusanyika tangu asubuhi kusubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo ambapo Karandinga la Magereza lilitinga mahakama hapo saa 2:09.
Scorpion alishuka kutoka kwenye karandinga hilo saa 2:19 asubuhi akiwa katika kanzu nyeupe na barghashia yenye rangi nyeupe, njano na bluu.
Kilichowastaajabisha watazamaji  wakati anashuka alikuwa akitabasamu chini ya ulinzi mkali.
Baadhi ya watazamaji walifura kwa hasira, wengine wakiendeleza minong’ono ya kulaani kitendo hicho.
Saa 3:10 asubuhi kesi hiyo ilitua mezani Hakimu Mkazi Adelf Sachore  chini ya Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola.
Ilitumia dakika tano tu kusikilizwa hadi kufutwa kwake.
Jambo la kushangaza lilikuwa pale wakati mwendesha mashtaka alipokuwa akitamka Kifungu cha Sheria Na. 91(1),  wingu lenye manyunyu ya mvua lilishuka kwa ghafla kisha umati wa watu uliokuwa madirisha kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kutafuta mahali pa kujisitiri.
Hata hivyo alipomaliza kusoma na Hakimu Sachore kuridhia kufutwa kwa kesi hiyo manyunyu hayo yalikata ghafla na miale ya jua ikaendelea kupenyeza katika miili ya watu.
Baada ya kesi hiyo kufutwa Scorpion alirudishwa mahabusu kisha majira ya saa 6:19 mchana kukiwa na jua kali alipandishwa mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule chini ya Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole kusomewa mashtaka mapya.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo Scorpion alifunguliwa pingu alizofungwa mikononi mwake na Askari Polisi huku umati mkubwa ukifuatilia kwa karibu.
Ilimchukua dakika nne tu hakimu kuisikiliza kesi hiyo, kisha Scorpion akaondolewa mbele ya korti na kurudishwa mahabusu.

1 comment:

  1. Wandishi wengine kwanini mmetawaliwa na imani za kishirikina, kunyesha kwa nvua na kukatika ghafla na jua kuchomoza ni nambo la ajabu? Ni jambo jipya? Nvua na scorpion kuna uhusiano gani? Wandishi wa jinsi hii ni aibu kwa tasnia ya habari.

    ReplyDelete