ILALA, DAR ES SALAAM
SHAHIDI namba moja wa tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha
lililotokea Tabata Bima jijini Dar es Salaam Antimi Kimati ameiambia Mahakama ya
Wilaya ya Ilala kuwa alimwona mtuhumiwa namba moja Amir Mohamed ‘Songambele’
akiwa na bunduki siku ya tukio.
Kesi hiyo ilifika mahakamani hapo Aprili 21 mwaka huu na kufunguliwa
jalada CC. 88/2016
Washtakiwa wanne Songambele (52), Juma Kassim Mwishehe (50), Hassan
Seleman Said (45) na Denis Charles
Chacha (32) walipandishwa kortini kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja ilianza kwa
Mwendesha Mashtaka Florida Wenceslaus kuiomba mahakama kuanza kusikiliza
ushahidi wa unyang’anyi wa vocha zenye thamani ya laki tatu (300,000) na fedha taslimu milioni mbili
na laki nane (2,800,000) mali ya Matola Asenga katika tukio lililotokea Januari
31 mwaka huu.
Pia Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama kupokea vithibitisho ambavyo
ni vitambulisho na maandishi ya awali ya kukiri kwao kutenda tukio hilo
walipohojiwa na polisi.
Baada ya kuapa kuwa atasema kweli kuhusu tukio hilo, Hakimu alimtaka
shahidi huyo kuanza kutoa ushahidi wake.
Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa wakati tukio lilipokuwa likitokea
alikuwa ni mfanyakazi wa Grocery iitwayo Container Pub iliyopo Tabata Bima.
Akiwa na wenzake katika kontena akiendelea kupanga vinywaji kwenye
friji ghafla alisikia mlio wa risasi, alipoangalia nje, watu wote walikuwa
chini ya ulinzi mmoja tu akiwa amesimama na bunduki.
Antimi alidai kwasababu taa zilikuwa zikiwaka aliiona sura ya
aliyeshika bunduki, alipoinua uso wake walitazamana uso kwa uso ndipo
aliponyooshewa mtutu wa bunduki na kupiga risasi aliyoikwepa na kuishia kutoboa
TV.
Alipodondoka Antimi alidai alitembelea magoti na kupita kwa kutumia
mlango wa nyuma ambako alijificha.
Hata hivyo Machi 7 mwaka huu, aliitwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi
Tabata ili kuwatambua watuhumiwa wa ujambazi kama kuna miongoni mwao
aliyehusika na tukio la Januari 31 mwaka huu, ndipo alipomtambua mtuhumiwa
namba moja wa kesi hiyo ya unyang’anyi.
Kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 31 mwaka huu ambapo inatarajiwa
kuendelea kusikiliza ushahidi.
0 Comments:
Post a Comment