NA JABIR JOHNSON
Salum Njewete 'Scorpion' akipelekwa katika karandinga la Jeshi la Magereza baada ya kesi yake kuahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika. |
MWALIMU wa sanaa za
mapigano Salum Njewete (34) maarufu Scorpion na mkazi wa Yombo Machimbo amepandishwa katika mahakama ya
Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka yanayomkabili likiwamo la wizi wa kutumia
silaha.
Shauri hilo lilifika
mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa tena ambako upande wa mashtaka uliiambia mahakama upelelezi wa kesi hiyo
bado haujakamilika.
Awali ilidaiwa mahakamani
hapo na Mwendesha Mashtaka wa serikali Munde Kalombola mbele ya Hakimu Adolf
Sanchore kuwa Septemba 6 mwaka huu katika maeneo ya Buguruni Shell jijini Dar
es Salaam mshtakiwa alimvamia na kumchoma visu kwenye macho,tumboni na mabegani
Said Mrisho kinyume na Kifungu cha Sheria Na.287A sura ya 16 ya makosa ya
jinai.
Mwendesha mashtaka alidai
mshtakiwa alimpora mkufu wa fedha gramu 38 wenye thamani ya Sh. 60,000; kidani
cha mkononi chenye thamani ya Sh. 85,000 na fedha taslimu Sh. 331,000.
Kesi hiyo ilitajwa kwa
mara ya kwanza Septemba 23 mwaka huu.
Hakimu aliahirisha kesi
hiyo hadi Oktoba 19 mwaka huu.
Hali ilivyokuwa
mahakamani
Mapema juzi akiwa
amevalia T-shirt nyekundu na suruali aina ya ‘Jeans’ alishuka katika karadinga
la Magereza chini ya ulinzi mkali huku akificha sura yake kuogopa
kamera za waandishi wa habari.
Umati mkubwa wa watu
ulifurika katika viwanja vya mahakama ya Ilala kumshuhudia mshtakiwa ambaye
minong’ono ya hadhira ilikuwa ikimtaja kama ‘mtoboa macho’.
Majira ya saa nane za
mchana mshtakiwa alirudishwa rumande huku kukiwa na hadhira ndogo ya watu.
Wakati akitolewa mahabusu
kurudishwa rumande Scorpion alitaka kuiahadaa hadhira kwa kubadilisha nguo zake
kuogopa kamera za waandishi wa habari (kama inavyoonekana pichani).
0 Comments:
Post a Comment