Mkusanyiko wa makazi ya watu, shule, hospitali, ofisi,
maduka, viwanda n.k. ulio mkubwa kuliko ule wa kijiji huitwa Mji. Mji ukizidi
kukua unakuja kuitwa pia jiji.
Miji ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Nchini Tanzania miji inakua kwa kasi. Hivyo, ili dhamira ya Tanzania ya kufikia
uchumi wa viwanda, ni muhimu kufikiria namna miji inavyopaswa kukua.
Kimataifa kulikuwa na makubaliano kwenye mkutano wa
kimataifa ya takwimu ya mwaka 1887 ya kuhesabu kila mji mwenye wakazi zaidi ya
100,000 kama "mji mkubwa", miji kati ya wakazi 20,000 na 100,000 kama
miji ya wastani na miji kati ya wakazi 5,000 na 20,000 kama miji midogo.
Kufuatana na hesabu hii kulikuwa na miji mikubwa 1,700 duniani hadi mwaka 2002.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya mnamo mwaka 2007,
dunia ilikuwa na watu wengi zaidi waishio mijini.
Bara la Ulaya ilichukua miaka 110 (1800-1910) kupata
ongezeko la wakazi waishio mijini kutoka asilimia 15 hadi 40, Asia na Afrika
zimefanya hivyo ndani ya miaka 50 tu (1960-2010).
Kwa mujibu wa tafsiri ya Shirika la Makazi la Umoja wa
Mataifa (UN – Habitat), miji inabidi ijijengee uwezo wa kuhimili changamoto
zinazojitokeza na uwezo wa kujiendeleza.
Katika malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) Na. 11
linasema Kuweka Miji na Makazi ya Binadamu Kuwa Jumuishi, Salama, Imara na
Endelevu.
Lengo hili linawataka mameya wa miji na Serikali za
Majiji kutekeleza majukumu yao katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo
Endelevu; ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo endelevu kuanzia ngazi ya Mtaa hadi
Jiji au Miji kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi.
Pia linasisitiza, Serikali kuzuia ujenzi holela na
kuweka mipango miji na utaratibu wa upatikanaji wa soko la viwanja na nyumba
hasa kwa watu wa kipato cha chini ili makazi yao yawe na huduma zote muhimu kwa
binadamu, mfumo wa usafiri kwa umma wenye kuzingatia mahitaji maalum kwa watu
wenye ulemavu, wazee na watoto.
Lengo hili linasisitiza uwekaji wa mipango mikakati ya
kuendeleza huduma za msingi vijijini ilikuwepo uwiano kati ya Miji na Vijiji.
Mnamo mwaka 2018 katika Kongamano la Kuadhimisha siku
ya Ukuaji wa miji kati ya Tanzania na Ufaransa wakati huo akiwa Waziri wa nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira George Simbachawene
alisema Jiji la Dar es Salaam linatajwa kuwa Miongoni mwa majiji yanayokua kwa
kasi barani Afrika, baada ya Abuja nchini Nigeria na Kinshasa ya DRC na ifikapo
mwaka 2030 linafikia idadi ya watu milioni 10.
“Bila kuzingatia mipango miji uchumi wa watu wetu
utachangia kuongezeka kwa Uharibifu wa Mazingira, hivyo ni lazima tuchukue
hatua stahiki…na serikali ya Tanzania inachukua hatua za kuweka mipango miji,”
alisema Simbachawene.
Athari za COVID-19 zimebadili kwa kiasi kikubwa maisha
ya mijini kote ulimwenguni. Mitaa imekuwa na jukumu muhimu katika kuchangia
kuwaweka watu salama na kudumisha shughuli kadhaa za kiuchumi.
Hata hivyo kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja
na usimamizi mbovu wa mipango miji ni miongoni mwa sababu zinazochangia ujenzi
holela nchini Tanzania na hivyo kuathiri Maendeleo ya Ukuaji wa Miji.
Hii inatokana na kuwa miji imekuwa ikitoa aina mpya za
ujumuishaji wa kijamii, pamoja na usawa, upatikanaji wa huduma na fursa mpya,
na ushiriki na uhamasishaji ambao unaonyesha utofauti wa miji, nchi na
ulimwengu.
Oktoba 31 kila mwaka ni siku ambayo Umoja wa Mataifa
(UN) uliiwekwa kwa ajili ya kutoa hamasa katika ukuaji wa miji duniani kote.
Huadhimishwa huku ikiwa inatarajiwa kukuza maslahi ya
jamii ya kimataifa katika ukuaji wa miji ulimwenguni, kusukuma mbele
ushirikiano kati ya nchi katika kufikia fursa na kushughulikia changamoto za
ukuaji wa miji, na kuchangia maendeleo endelevu ya miji kote ulimwenguni.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
anasema, “Jamii za mijini zinaposhiriki katika kutengeneza sera na kufanya
maamuzi, na kuwezeshwa na rasilimali fedha, matokeo yanajumuisha zaidi na
kudumu. Hebu tuweke jamii zetu kwenye kiini cha miji ya baadaye.”
Kauli mbiu ya mwaka huu katika siku hii inasema, “Kuthamini
Jamii zetu na Miji.” Hii inatokana na
ukweli kuwa tangu miaka ya 1980 kumekuwa na utofauti wa miji duniani kote.
Uelewa wa wananchi juu ya tamko hili la kimataifa,
kuhusu ukuaji wa miji utawawezesha kuchukua hatua za makusudi kupitia vikundi
na majukwaa yao kutimiza wajibu wao na kufuatilia uwajibikaji wa serikali.