Thursday, November 29, 2018
LHRC: Mwezeshaji wa Haki za Binadamu Tanzania
NA JABIR JOHNSON
johnsonjabir@gmail.com
Mwandishi Dkt. Helen Kijo-Bisimba katika kitabu chake
‘Mwongozo wa Haki za Binadamu’ cha mwaka 2014 anatoa tafsiri ya Haki za
Binadamu kuwa ni zile haki ambazo kila mwanadamu anazo au anastahili kuwa nazo
kwa kuwa tu yeye ni binadamu.
Pia katika tafsiri hiyo kwenye ukurasa wa 13 anaandika
Haki za
binadamu hazitegemei au
kutolewa na hati
ya kisheria. Haki
hizi ni za
asili, binadamu huzaliwa nazo na hivyo inabidi zitambuliwe na
kuheshimiwa.
HISTORIA YA HAKI ZA BINADAMU
Katika historia ya
binadamu imebainika kuwa
jamii nyingi zilitambua
na kuthamini utu wa
haki za Binadamu. Hii ni kabla ya hata haki hizi kuandikwa au kutamkwa katika
mikataba au sheria za nchi
mbalimbali.
Kwa upande
mwingine, vitendo vya
uonevu, dhuluma na vya
kinyama vilikuwepo katika
jamii nyingi duniani.
Na hii ilifanya baadhi ya
jamii kuinuka na kudai haki za binadamu pale zilipokuwa
zinakiukwa au kutotekelezwa.
Historia inaonyesha
jitihada za mwanzo
zilizofanywa na baadhi
ya jamii mbalimbali katika kuzinadi haki za binadamu ili
kuweza kutekelezwa ipasavyo.
Jitihada hizi, ndizo
zimekuwa chimbuko la
kuandikwa kwa mikataba
mbalimbali ya haki
za binadamu.
Hati ya Magna Carta kwa mara ya kwanza iliandikwa mwaka 1215
na Mfalme John wa England akiwa na wenzake Stephen Langton Bishop Mkuu wa
Canterbury.
Hata hivyo kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945 ndio
kulileta changamoto rasmi ya kulinda na kuheshimu haki za bianadamu karibu
duniani kote.
Hii ni baada ya watu wengi kuteseka, kufa na pia kunyanyaswa
katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Hapo ndipo jumuiya ya Kimataifa ilianza kukubali, kuthamini
na kulinda haki za binadamu
Asasi zisizo za kiserikali kwa kiwango kikubwa zimekuwa
mstari wa mbele katika utoaji wa elimu
na mafunzo ya
haki za binadamu
katika nchi nyingi.
KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU (LHRC)
Nchini Tanzania Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu
kimekuwa kikiendelea mafunzo
mbalimbali ya haki za binadamu tangu mwaka 1995.
Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa kwa makundi na watu
mbalimbali kama vile viongozi na
watendaji wa serikali
mfano, wabunge, madiwani, mahakimu askari
polisi, viongozi wa
serikali za vijiji
na wananchi kwa
ujumla hasa walio vijijini.
Mafunzo hayo
daima yamekuwa yakilenga
katika kuisaidia jamii
nzima ya watanzania walio mijini
na vijijini kuelewa maana ya haki za binadamu katika maisha yao ya kila siku.
Kujua manufaa ya haki
za binadamu na kuchukua jukumu la kuheshimu, kutetea, kulinda na kuendeleza
haki za binadamu kwa manufaa ya watanzania wote.
Oktoba 30 hadi Novemba 2 mwaka huu LHRC iliendeleza shauku
yake ya kutoa elimu katika makundi mbalimbali na safari hii ilikuwa zamu ya
waandishi wa habari nchini ambao walikutana mjini Morogoro kwa ajili ya kupeana
uzoefu na ufafanuzi katika baadhi ya maeneo yanayohusu uhuru wa kujieleza na
uhuru wa kukusanyika.
UMUHIMU WA WANAHABARI
Wanahabari ni kiungo muhimu katika makundi yote katika jamii
katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuliko muhimili wowote na ndio sababu mhimili
huo unapewa jina la ‘Muhimili wa Nne usioonekana’.
Mtu yuko radhi asitoe taarifa zake katika uongozi wa
kiserikali au chama akatoa kwa waandishi wa habari akiamini kuwa ujumbe wake
utawafikia mamia kwa maelfu.
Licha ya uzuri huo lakini kumekuwapo na changamoto
mbalimbali ndani ya medani hiyo hali ambayo imekuwa ikitishia hata uhuru wa
utoaji wa taarifa.
Sheria mbalimbali zimekuwa zikitungwa kwa ajili ya kuminya
au kuwapendelea zaidi watawala kuliko wanahabari hali ambayo ni hatari kwa
jamii ambayo imekuwa ikitegemea msaada mkubwa kutoka kwa muhimili huo.
SHERIA KANDAMIZI ZA UPASHANAJI WA HABARI
Kila nchi ina utaratibu na kanuni zake katika upashanaji wa
habari lakini hizo zote zinapaswa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na zile za
kimataifa kutokana na ukweli kwamba walio wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN)
walikubaliana kuwapo na usimamizi mzuri wa haki za binadamu.
Hali ya upashanaji wa habari nchini Tanzania, imekuwa ikikua
siku baada ya siku licha ya changamoto za hapa na pale.
Mwanasheria wa LHRC William Kahale ambaye alikuwa miongoni
mwa wawezeshaji katika semina hiyo alisema, “Kuna maendeleo makubwa kwa maana
ya utoaji wa taarifa. Hapo awali kabla kwa kiasi kikubwa hakukuwa na sheria
ukiacha katiba ya Jamhuri ya Muungano (Tanzania) katika ibara ya 18 inatoa
uhuru wa kupokea, kutoa taarifa lakini kuna sheria ambazo zilikuwa zikiupoka uhuru huo."
Kwa kifupi Katiba
ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977
(kama ilivyorekebishwa) inalinda
haki za kiraia na kisiasa, na haki za kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni.
Licha ya kulinda kwake kuna sheria kandamizi kwa vyombo vya
habari Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu
ya mwaka 2016, Sheria ya Utoaji wa Taarifa, Sheria ya Uhalifu Mitandaoni na ile
ya Maudhui ya Mitandaoni.
Hizi zote zina nia ya kuvibana vyombo vya habari hali ambayo
inabana uhuru wa kujieleza na kuwasilisha taarifa mbalimbali.
UHURU WA HABARI NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Kahale alisema serikali ya awamu ya tano ya Dkt. John
Magufuli imejipambanua kuwa inapambana na rushwa waziwazi.
Endapo jamii haitakuwa huru katika utoaji wa taarifa zake na
mapambano ya rushwa hayatakuwa na maana yoyote kwani vita dhidi ya rushwa
haiwezi kufanywa na serikali peke yake bila kuhusisha wananchi wake.
Kuviminya vyombo vya habari ni njia mojawapo ya kufanya
mapambano ya rushwa kuwa magumu kwani watu watakuwa wakiogopa.
TANZANIA YA VIWANDA NA UHURU WA HABARI
Katika nukuu za Papa Francis wa Kanisa Katoliki anasema
(katika tafsiri isiyo fasaha), “Haki za Binadamu hazikiukwi na ugaidi pekee, au
ukandamizaji au mauaji bali kuwa na mifumo ya kiuchumi isiyostahili husababisha
pengo la usawa kuwa kubwa.”
Hivyo basi katika maendeleo ya taifa la Tanzania yatategemea
sana usimamizi mzuri wa haki za binadamu hususani katika ‘Tanzania ya Viwanda
Tunayoitaka.’
Kahale alisema, Tanzania ya viwanda inategemea namna ambavyo
wananchi wanabadilisha taarifa za kiuchumi kuhusu bidhaa zao, sasa kama Sheria
ikiwamo ya takwimu itabana uhuru wa takwimu za kiuchumi kufanyika watu
wataogopa kuwekeza hivyo itakuwa ndoto kufikia malengo.
Makala hii
imetayarishwa na Jabir Johnson, aliyekuwa Morogoro katika semina iliyotolewa na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Kwa maoni na ushauri barua pepe:
jaizmela2010@gmail.com
Tuesday, November 27, 2018
Chadema yamjibu Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda |
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimetetea sababu ya
wabunge wake kutoonekana kwenye baadhi ya shughuli za Maendeleo kwa kile
walichokidai kuwa wabunge wake hawakupewa mialiko na wengine wakiwa na kesi
mbalimbali mahakamani.
Majibu hayo ya CHADEMA yanakuja ikiwa ni saa chache
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akiwa kwenye uzinduzi wa
maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusema kuwa wabunge wa upinzani
hawaonekani kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mkurugenzi wa Itifaki na
Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, amesema Makonda anasahau sana kuwa wabunge
wetu walifukuzwa kwenye ofisi zao Kinondoni.
Akiwa kwenye uzinduzi wa maktaba hiyo
ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Paul Makonda amesema amekaririwa akisema
anashangaa kuona wabunge upinzani katika mkoa wake wakienda vyuoni kuwarubuni
wanafunzi wawapigie kura huku wakishindwa kutokea kwenye shughuli za maendeleo.
Makonda ambaye mara kadhaa amekaririwa kuwa na kauli tata aliongeza kuwa
wapinzani hao kazi yao ni kukosoa tu badala ya kusifia. Hata hivyo Waziri Mkuu
wa Zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Edward Lowassa alikuwepo katika
uzinduzi huo.
Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam |
Sol Campbell, kocha mpya Macclesfield
Mchezaji wa zamani wa Arsenal Sol Campbell ameteuliwa kuwa
kocha mkuu wa klabu ya daraja la pili ya Macclesfield.
Nyota huyo mwenye umri
wa miaka 44 amepewa kandarasi ya miezi 18 kukinoa kikosi hicho.
Sol Campbell
aliyestaafu soka mwaka 2012 anachukua mikoba ya kocha Mark Yates aliyetimuliwa Oktoba
mwaka huu. Kazi hiyo ni ya kwanza kwa mlinzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya
England na Arsenal. Sol Campbell alihusishwa na kuzinoa Oxford United, Oldham na
Grimsby zote za England.
Kabla ya kutua Kaskazini Magharibi mwa England Sol
Campbell alikuwa akifanya kazi na kikosi cha timu ya taifa chini ya umri wa
miaka 21. Sol Campbell anakumbukwa na mashabiki wa London katika uhamisho ambao
haukutarajiwa wa mwaka 2001 kutoka Tottenham kwenda kwa mahasimu wao Arsenal na
kuzua hasira kwa mashabiki na wapenzi wa Majogoo hao wa London.
Enzi za
uchezaji wake Sol Campbell alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu, Vikombe vitatu vya
FA na kikombe kimoja cha Ligi na katika timu ya taifa alicheza fainali tatu za
Kombe la Dunia na kufikisha mechi 73 akiwa na Simba Watatu.