Thursday, December 24, 2020

Mtoto amuua baba yake kwa mapanga Hai

 

Mkazi wa Masama Kijiji cha Muroma katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro aliyefahamika kwa jina la Welanzari Kimaro (60) ameuawa kwa kukatwa na panga kichwani na kisogoni na mwanaye wa kumzaa kisha muuaji kutoweka kusikojulikana.

Aidha muuaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kabla hajatoweka kusikojulikana alimjeruhi mama yake mzazi  aliyekuwa jikoni akiandaa kifungua kinywa kwa ajili ya familia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashuhuda wa tukio hilo walisema muuaji anayefahamika kwa jina la James Welanzari alitekeleza azma yake mnamo Desemba 18 mwaka huu mapema asubuhi wakati baba yake akifanya usafi wan je ya nyumba.

“Siku ya tukio baba yake aliamka asubuhi akawa anakatakata fensi ya miti iliyopo nyumbani hapo na mkewe alikuwa akiandaa chai kwa ajili ya kifungua kinywa,” alisema shuhuda ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mashuhuda waliongeza kuwa marehemu ambaye alikuwa mkulima hakuwa na ugomvi na mtoto wake huyo ambaya alikuwa akiishi umbali mfupi kutoka ilipo nyumba ya baba yake.

“Kijana aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa anakaa nyumba ya pili ya shangazi yake  ambapo sio mbali sana na nyumba ya baba yake, na hatukuwahi kusikia ugomvi baina yao na mpaka sasa hatujui ni mazingira gani yalimpelekea kijana kuchukua uamuzi wa kumuua baba yake,” alisema shuhuda mwingine.

Hata hivyo mashuhuda hao walisema muuaji ni msomi wa kidato cha sita ambaye mwaka 2017 alifaulu kidato cha sita na mnamo mwaka 2018 alichaguliwa kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu ambapo kwa sababu zisizojulikana hakwenda kuendelea na masomo hayo.

“Inaweza ikawa ni sababu ya kuchanganyikiwa kwani tangu wakati alipofaulu kidato cha sita na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu alianza kuwa mkimya hakuwa anapenda kabisa kuongea na watu alikuwa mpweke aliyependelea zaidi kujitenga  ma wenzake, kiukweli hakujihusisha na makundi ya vijana wenzake,” alisema shuhuda.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa tukio hilo lilitokea saa 1:30 asubuhi ya Desemba 18 mwaka huu na kwamba aliyejeruhiwa amefahamika kwa jina la Joyce Exaud (51) ambaye ni mkulima na mkazi wa Masama.

Aidha Jeshi hilo limesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Hai  na majeruhi yupo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea kufanyika.

0 Comments:

Post a Comment