Mwandishi E. A. Alpers anaandika kwenye “African Slave-Trade (Biashara ya Utumwa ya Afrika); “Ushahidi zaidi kwamba biashara ya watumwa kwa vyovyote vile ilikuwa mashuhuri katika Afrika ya Mashariki kabla ya karne ya kumi na nane, imeletwa na Wareno.
Hakika Wareno, wakiwa ndiyo waasisi (waanzilishi) wa Atlantic Slave-Trade, wangejaribu kuendeleza biashara ya watumwa katika Afrika ya Mashariki kama wangeikuta tayari ipo na imekwisha shamiri. Lakini maandiko ya mwanzo ya Wareno yanataja tu biashara ya watumwa kwa kupitia tu.
Lililokuwa muhimu zaidi ni wale wafanyabiashara za dhahabu na pembe za ndovu walizipeleka Uarabuni na India. Wavamizi wa Kireno walielekeza juhudi zao kwenye bidhaa hizo wakati wa karne ya 16 na 17, sio tu kwenye pwani ya Kenya na Tanzania, bali pia katika Msumbiji na Zimbabwe.
Hata nta na ambari zinaonyesha zilikuwa bidhaa muhimu zaidi kuzidi watumwa wakati mrefu sana wa kipindi hiki. Kwani tofauti na wakoloni katika nchi ya Amerika, Wareno kamwe hawakuanzisha uchumi wowote wa kilimo huko India.
Biashara ya watumwa huko Brazil ilikuwa haramu kufanya biashara ya watumwa hadi mwaka 1645, na kamwe haikulitiliwa maanani hadi mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa. Hadi mwaka wa 1753, wakati misingi ya biashara mpya ya watumwa ilikuwa inawekwa Afrika ya Mashariki, palikuwepo na jumla ya watumwa 4399 tu wa Kiafrika katika India yote ya Wareno.
Licha ya kumbukumbu za utumwa wa wakati ule kushamiri na kupigwa marufuku bado mataifa ya Afrika yanakabiliwa na changamoto ya utumwa wa fikra.
Ni heri kuwa mtumwa wa pesa kuliko kuwa mtumwa wa fikra. Maana fikra yako itakukomboa kutoka katika huo utumwa wa pesa. Lakini si utumwa wa fikra. Utumwa wa fikra ni hali ya mtu kushindwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kufikiri katika mambo mbalimbali na hata akitumia uwezo wake bado hajiamini.
Kwa ufupi utumwa wa fikra ni hali ya kuwa tegemezi sana kimawazo. Aliye mtumwa wa fikra mara nyingi huwa pia ni mtumwa wa mwili, yaani huutumia zaidi mwili wake kuliko akili zake.
Mtumwa wa fikra mara nyingi fikra zake huwaza kwa kurudi nyuma, na huyaona matatizo sana kuliko mafanikio katika fikra zake, huwa haishii hapo kwani hizidi kuzitumikisha fikra zake kwa kuunda lawama mara kwa mara kwa kuona anaonewa (lawama haziishi katika kinywa chake maana huwa zimechoka kukaa katika fikra zake).
Kwa kutegemea fikra hasi zilizopita na kuzifikiri mara kwa mara hizo hizo kisha kuzidi kuzalisha hasi na kushindwa kufikiri chanya kisha kukuza uwezo wake wa kufikiri.
Linaweza likawa ndio tatizo kwa baadhi ya watanzania ambao mara kadhaa wamekuwa na fikra hasi kwa kila jambo na kinachosikitisha zaidi ni pale ambao badala ya kuangalia siku za usoni zitakuwaje wanasalia kuangalia walikotoka hali ambayo inazidisha fikra hasi badala ya fikra chanya.
Ili kuweza kutibu changamoto ya utumwa wa fikra ni vema kufanya yafuatayo; Matibabu bora na mazuri huanza baada ya utambuzi wa ugonjwa.. Ni vyema kutambua aina ya utumwa ambao unatukabili (kujitambua ndio dawa ya kwanza).
Pia watanzania inawapasa wajifunze kuifundisha akili juu ya fikra mpya; tabia na kanuni ya fikra ni toa kitu weka kitu, yaani fikra fulani inapotoka basi fikra fulani huja. Kwa kawaida mwanadamu mwenye utimamu wa akili kuwaza ni jambo la kawaida Kwake, ila tatizo ni fikra zipi zinatawala akili zetu.
Mawazo chanya hukuza na kuongeza uwezo lakini mawazo hasi yasiyo na mwendelezo wa kifikra hudidimiza na kudumiza fikra. Wengi wamekuwa wakijivuna kutokana na umri walio nao badala ya kujivuna kutokana na fikra chanya walizonazo.
Tunapoishi nje ya kusudi la kuwepo duniani hapo ndipo utumwa wa kifikra hutokea, je ni kwa nini? Kila mwanadamu katika ufahamu wake ana uwezo wa kufikiri na kutenda zaidi kuliko, kuendelea kutenda na kufikiri kupitia fikra za mwingine ni jambo lisilokubalika.
Kwanini una mwili wa kizee lakini akili zako ni changa, unaumiza kwa taifa kuwa na watu wa namna hiyo. Maendeleo ya nchi yanajengwa kutokana na fikra chanya. Biashara ya utumwa ilishamalizika lakini kuna kazi kubwa ya kuutokomeza utumwa wa fikra.
0 Comments:
Post a Comment