Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga imemaliza mgogoro uliodumu kwa miaka mitatu wa nyumba ya marehemu Dickson Godfrey Singano iliyokuwa ikigombaniwa na ndugu wa pande mbili kwa mjane kushinda rufaa iliyokatwa na wifi wa mjane aliyetaka kumnyang’anya kinyume cha sheria.
Akitoa hukumu ya rufaa hiyo hivi karibuni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe Mussa Ngalu alisema anarejea Rufaa ya Mirathi Na. 01 ya mwaka 2019 ambapo Beatrice Shogholo (mkata rufaa) na dada wa marehemu alifungua dhidi ya mjane Zaituni Salimu Kassimu (Mjibu rufaa) katika kesi hiyo Na. 40 ya mwaka 2017.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mali iliyokuwa ikigombaniwa ni nyumba iliyojengwa kwa jitihada za pamoja za marehemu na mkewe, inayopatikana kata ya Masuguru wilayani Korogwe, ambayo mkata rufaa alijimilikisha kinyume cha sheria tangu mwaka 2017, marehemu alipofariki.
Katika kesi hiyo mkata rufaa alisimamiwa na Wakili Msomi Peter Wenceslaus huku mjibu rufaa akitetewa na Wakili msomi Mathias Nkingwa.
Mke marehemu alibarikiwa kupata mtoto mmoja, ajulikanaye kwa jina la Grace Dickson mwenye umri wa miaka minne.
Hakimu mkazi Ngalu alisema ushahidi wa pande zote mbili ulisikilizwa na Mahakama kumpa ushindi mjibu rufaa. Sambamba na ushindi huo, pia Mahakama iliamuru mkata rufaa kuhama mara moja katika nyumba hiyo ili kumpisha mke wa marehemu na mtoto wake kuendelea kuishi katika nyumba hiyo.
Aidha Hakimu Mkazi Ngalu alitoa wito kwa jamii kujifunza namna ya kuandaa wosia ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza pindi mmojawapo anapoaga dunia.
“Kimsingi, unapoacha Wosia unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kugawa mali zako utakavyo na hivyo kuepusha migogoro isiyo ya lazima inayoweza kupelekea kubaribu kabisa mahusiano ya wategemezi wako; pengine hata kuuana wao kwa wao. Jamani, huu ni ushauri wa bure. Tuandae Wosia. Ni kwa usalama wa wategemezi wetu. Ndugu zetu ni wema kwetu tukiwa hai tu, tukishatangulia tu mbele za haki wanageuka mbogo,” alisema Hakimu Mkazi Ngalu.
Awali katika shauri hilo lilioanza katika mahakama ya mwanzo kwa kupewa nguvu na Kifungu Na. 11 kilichorekebishwa mwaka 2019 pamoja na sheria Na. 10 ya mahakama za mwanzo (kuhusu usimamizi wa mali isiyohamishika) G.N Na. 49 ya mwaka 1971.
Ilidaiwa mahakama hapo kuwa kikao cha ukoo kilikaa ili kugawana mali za marehemu na kuamuriwa kuwa nyumba iliyopo katika eneo la Masuguru apewe mtoto wa marehemu.
Aidha ukoo ulifikia maamuzi kuwa mali za marehemu zikodishwe ili kumsaidia bibi wa marehemu, mke wa marehemu na mtoto wa marehemu.
Hatua hiyo ilimwinua mke wa marehemu ambaye hakukubali bibi wa mtoto afaidike na mali za marehemu wakati alishapewa eneo lake huko Kwamkole, Korogwe.
Katika mahakama ya mwanzo mjane wa marehemu alishinda shauri hilo ambapo mkata rufaa ambaye ni dada wa marehemu hakuridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo hivyo kupeleka shauri lake katika mahakama ya wilaya Korogwe ambako mkata rufaa alishindwa na mjibu rufaa ambaye ni mjane wa marehemu alishinda.
0 Comments:
Post a Comment