Monday, January 4, 2021

Louis Braille: Mwanzilishi wa Nukta Nundu

 

Licha ya kwamba alifariki Januari 6, 1852  lakini Louis Braille ameacha nukta muhimu katika ulimwengu huu kwani akiwa katika masomo; alifanikiwa kugundua namna ya vipofu wanavyoweza kusoma kwa kile ambacho sasa kinafahamika kwa jina la maandishi ya nukta nundu.

JANUARI 4, 1809 katika mji wa Coupvray uliopo umbali wa kilometa 40 kutoka jijini Paris alizaliwa mtoto aliyefahamika kwa jina la Louis Braille kutoka kwa wazazi Simon-Rene na Monique. Alizaliwa na kuishi katika eneo la ekari saba tu ambalo wazazi walikuwa wakilima zabibu.

Mzee Simon-Rene alifanikiwa sana katika kilimo lakini zaidi sana katika kiwanda chake cha ngozi kwani alikuwa mjasiriamali. Katika kiwanda chake hicho alikuwa mtengenezaji wa vifaa vya farasi ikiwamo mikanda ambayo ilitumika kuwaongezea farasi.  

Siku moja mzee Simon-Rene alipokuwa katika kazi yake kiwandani mtoto wake huyo Louis alikwenda kuungana na baba yake huko. Mwanaye huyo alikuwa na umri wa miaka mitatu.

Kwa bahati mbaya wakati akiendelea na kazi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngozi sindano ya kushonea katika vifaa hivyo iliruka na kutoboa jicho moja. Ilikuwa ni kilio kwa familia ya Simon-Rene ambaye alikuwa amejaliwa kuwa na watoto wanne.

Athari za tukio hilo zilimuathiri Louis ambaye siku za usoni alishindwa kabisa kutazama hatimaye akawa ni kipofu wa macho yote mawili.

Kuwa kipofu hakuifanya familia ile ikate tama ya kumwendeleza mtoto wao katika medani ya elimu ambapo Louis alikwenda kusoma hadi akawa Profesa wa Chuo nchini Ufaransa.

Licha ya kwamba alifariki Januari 6, 1852  lakini Braille ameacha nukta muhimu katika ulimwengu huu kwani akiwa katika masomo; alifanikiwa kugundua namna ya vipofu wanavyoweza kusoma kwa kile ambacho sasa kinafahamika kwa jina la maandishi ya nukta nundu.

Akiwa shuleni alivutiwa na mwandishi wa kijeshi Charles Barbier de la Serre (Mei 18, 1767 –Aprili 22, 1841). Barbier alikuwa mahiri enzi zake kwa kuwa mwanzilishi wa namna ya kusoma nyakati za usiku au kukiwa na giza.

Hivyo Braille aliweza kutengeneza namna bora ya kusoma kumzidi Barbier kwa watu wenye upofu ambapo kazi yake ya kwanza aliiweka hadharani mnamo mwaka 1824.

Kwa heshima ya ugunduzi huo kila Januari 4 kila mwaka huadhimishwa siku ya Nukta Nundu kukumbuka ubunifu na ugunduzi wa Braille kuwasaidia wenye upofu.

Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa (UN) mnamo mwaka  2019 uliadhimisha rasmi maadhimisho hayo kwa kutambua umuhimu wa machapisho ya nukta nundu kama njia muhimu ya mawasiliano kwa wasioona na pia kuwawezesha kundi hilo na wale wenye uoni hafifu kupata haki yao ya msingi ya mawasiliano.

Kwa kifupi nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.

Matumizi ya nukta nundu huwezesha kundi hilo kusoma vitabu na majarida na hivyo kuimarisha ubobezi wao, uhuru na usawa katika nyanja mbalimbali.

Ibara ya 2 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu inataja nukta nundu kama mbinu muhimu kwenye elimu, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.

Hali kadhalika nukta nundu inasaidia ujumuishaji kwenye jamii kwa watu wasioona na wenye uoni hafifu kama ilivyobainishwa katika ibara ya 21 na 24 ya mkataba huo wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, au CRPD.

Nchini matumizi ya maandishi ya nukta nundu ni jambo la kawaida kwenye taasisi za elimu ambapo Amon Mpanju, ambaye anahudumu katika serikali ya awamu ya tano ni miongoni mwa wanaotumia vitabu vya nukta nundu. Pia Mpanju ni mlemavu wa kwanza wa macho kushika wadhifa wa juu wa uongozi nchini humo ambaye aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kanuni na sheria nchini humo zinatambua maandishi ya nukta nundu kama njia rasmi ya mawasiliano kwa wasioona na wenye uoni hafifu.

Chuo cha Patandi mkoani Arusha hutoa mafunzo kwa walimu wa wanafunzi wasioona, ambapo nyuma yake kuna kundi kubwa la wasioona ambao wanahitaji msaada wa kujua namna ya kuwasiliana kwa kutumia nukta nundu.

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya Nukta Nundu ni vema jamii ikatambua wenye ulemavu wa kuona wanahitaji msaada wao ili waweze kufikia malengo kama watu wengi. Ni vema kujitolea kwa hali na mali ikiwemo kuwapeleka shule wenye ulemavu wa macho ili waweze kujifunza kwa kutumia nukta nundu.

Imetayarishwa na Jabir Johnson, Jan. 4, 2021

0 Comments:

Post a Comment