Historia ya Elimu Tanzania Bara imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni kabla na baada ya uhuru. Kabla ya kuja kwa wageni katika mwambao wa Tanganyika, kila kabila lilikuwa na mfumo wake wa elimu ya kijadi. Elimu ya Kijadi ilitokana na taratibu za kila siku za jamii za makabila mbalimbali.
Elimu hiyo iliyojumuisha maarifa, stadi, maadili, utamaduni, mbinu na taratibu nzuri za kufanya kazi na kujilinda kutokana na mabaa ya njaa, magonjwa na maadui wa usalama wa jamii na wa mali zao ilirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Mambo ya kujifunza yaligawanyika kirika na kutolewa na watu wazima nyumbani, kazini na katika nyanja nyingine za maisha. Mfumo huu ulianza kuwa na mabadiliko katika malengo na utoaji wake tangu wakoloni walipoingia nchini.
Wageni wa kwanza Tanzania Bara walikuwa Waarabu, wakifuatiwa na Wareno, Wajerumani na Waingereza.
Kwa kuwa wageni hao walipokezana madaraka ya sehemu ya nchi au nchi nzima, kila kundi lilibadili mfumo wa elimu kulingana na matakwa yao bila kujali yale yaliyokuwa na manufaa kwa Watanzania Bara.
Shule za mataifa mbalimbali zilitofautiana katika malengo, mitaala, sifa na taaluma za walimu, lugha ya kufundishia, na ubora wa majengo ya shule na nyumba za walimu.
Waarabu walipoingia walianzisha mafunzo ya Quran. Elimu hii ilitia mkazo uenezi wa dini ya Kiislamu na Utamaduni wa Kiarabu. Utawala wa Kijerumani na Kiingereza ulitanguliwa na ujio wa Wamisionari.
Walipofika, Wamisionari walitoa elimu kufuatana na imani yao na historia ya nchi walikotoka. Elimu ya Wamisionari ilisisitiza uenezi wa dini ya Kikristo. Utawala wa Kijerumani ulitoa elimu iliyotilia mkazo stadi, maarifa na mafunzo ya kazi na uraia mwema kwa Serikali ya Ujerumani.
Mfumo wa elimu ya Waingereza katika Tanzania Bara ulikuwa na misingi ya ubaguzi wa rangi na ulitoa nafasi na nyenzo bora zaidi za elimu kwa watoto wa Kizungu na Kiasia kuliko Waafrika.
Lengo kubwa la elimu lilikuwa ni kupata watumishi Waafrika ambao wangetumika katika kutetea matakwa ya wakoloni, na hivyo kuwafanya wasomi kuwa tegemezi.
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ukurasa wa 19 inasema, “Elimu ichukuliwe kama mkakati kwa kuweka mageuzi ya kifikra na kuunda taifalililoelimika vizuri, lenye maarifa ya kutosha yanayohitajika katika kutatua kwaufanisi na kiushindani changamoto ya maendeleo inayoikabili nchi. Kutokana na hilo, mfumo wa elimu hauna budi kupangwa upya na kubadilishwa kwa ubora unaolenga katika kukuza ubunifu na utatuzi wa matatizo.”
Serikali ya Tanzania imetambua umuhimu wa kuwekeza kwa watu wake kwa nia ya kupambanana magonjwa, umaskini na ujinga.
Mwenyezi Mungu ametujalia kuuona tena mwaka mwingine baada ya likizo ambayo ilienda sambamba na sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Watoto, wazee watu wa kila rika walifurahi katika sikukuu hizo na sasa tunakwenda katika kipengele muhimu katika maisha ya watoto na jamii kwa ujumla cha elimu, au kupeleka watoto na vijana shuleni, mzazi au mlezi sasa una wajibu gani kwa mtoto au kijana wako?
Jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu na sio kuhudhuria shule tu ni la jamii nzima na sio la mwalimu pekee.
Wajibu wa mzazi sio tu kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakula, anapata sare za shule dafttari na kalamu pekee. Mzazi ana nafasi kubwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba mwanafunzi au mwanae anahudhuria shule na anajifunza pia anakua na nidhamu ili aweze kufanya vizuri katika masomo yake.
Wazazi wengi wana shauku kubwa ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo yao, lakini hawako tayari kufuatilia maendeleo yao shuleni pamoja na mienendo yao kinidhamu wakiwa shuleni na hata nyumbani. Jukumu hilo wameachiwa walimu peke yao.
Na walimu wanapojaribu kuwanyoosha kinidhamu jamii inawanyoshea kidole na kuwalaumu.
Kutokana na ugumu wa maisha wazazi wamekua hawana muda wa kukagua daftari za watoto wao, kutembelea shuleni na kufanya mashauriano na walimu, kukaa na watoto na kuwashauri kuhusu maendeleo shuleni na changamoto wanazokumbana nazo na namna ya kuzitatua ili waweze kufikia malengo yao katika maisha.
Hivyo basi wakati shule zinapofunguliwa ni vema mzazi au mlezi akatambua kuwa kumpa mahitaji ya kwenda nayo shuleni sio mwisho wa kumhudumia mwanafunzi huyo bali kuna hatua zaidi zinatakiwa kwa ajili ya kufikia madhumuni ya kumpeleka shuleni ili baadaye aweze kukabiliana na changamoto za maisha.
Niwatakie kila la kheri katika msimu mpya wa masomo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
0 Comments:
Post a Comment