Tuesday, January 5, 2021

Wateja heshimuni wanaowahudumia

 

Ni kweli kuna msemo usemao, “Mteja kwetu ni Mfalme.” Na kibaya zaidi msemo huu umeonekana kuwabana zaidi watoa huduma kuliko wanaohudumiwa hata kama watafanya makosa kiasi gani.

Wazungumzaji wazawa wa Kiswahili wa Zanzibar wana desturi zao katika kuitana. Kabla ya jina hutanguliza neno la heshima. Hali hii hutokea kwa wakubwa na wadogo, wanaojuana na wasiojuana.

Kulingana na utafiti uliofanywa na African Journals Online (AJOL) unasema; maneno ya heshima yanatumika kulingana na rika za watu. Aidha, data imeonesha kuwa wazawa wa lugha ya Kiswahili huyatumia maneno ya heshima katika kuonesha uhusiano wa kifamilia na uhusiano usiokuwa wa kifamilia ili kujenga usuhuba na heshima katika mazungumzo.

Wazawa wa lugha ya Kiswahili huelimishana kuitana na kuyatumia maneno ya heshima tangu wanapokuwa wadogo kama data inavyoonesha kuwa mzazi anaweza kumwita mtoto wake baba au mama, bibi au babu, mjomba au shangazi na kadhalika.

Katika maofisi mengi yamekuwa na kanuni zake za maadili kwa wafanyakazi wake ili jina la kampuni lisiharibikiwe ili kumfanya mteja aonekane sahihi.

“Ni muhimu kujali tunavyofanya kazi. Tumejitolea kufanya kazi kwa kufuata na kuzingatia sheria zote husika kwa ukamilifu (hilo halina ubishi!), lakini pia ni muhimu, kufanya hivyo kwa kuzingatia maadili na kwa njia salama. Tunaunda thamani na kubuni imani miongoni mwa wadau wetu kwa kufanya yaliyo sahihi kila siku,” anakazia mkurugenzi mtendaji wa kampuni mojawapo.

Ni kweli kuna msemo usemao, “Mteja kwetu ni Mfalme.” Na kibaya zaidi msemo huu umeonekana kuwabana zaidi watoa huduma kuliko wanaohudumiwa hata kama watafanya makosa kiasi gani.

Unapoingia katika ofisi husika unakutana na maneno mazuri, “Tumejitolea kuwapa wateja wetu chaguo salama, nafuu na za ubora wa juu kabisa. Tunajihusisha katika jamii tunakofanya kazi na kuishi.” Iweje sasa mteja unaanza kutoa maneno yasiyo na heshima kwa anayekuhudumia.

Hakuna kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa.

Kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.

Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.

Kuna baadhi ya wateja wamekuwa wakikosa staha pindi wanapohudumiwa, vinywa vyao vimejaa matusi na dharau kwa kisingizio yeye ni mtoaji wa pesa imefikia mahali hata pa kutoa kauli chafu kuwa, kama sio yeye huyo mfanyakazi hawezi kupata mshahara kwani bosi wake anatamlipa nini wakati hauzi?

Tunatamani kuiona Tanzania ikisonga mbele katika kila nyanja kwani maendeleo hayawezi kuitwa maendeleo kama kuna ukosefu wa heshima na adabu eti kisa wewe ni mteja. Tukijrekebishe tunapouanza mwaka huu ili kuufanya kuwa mwaka wa mafanikio ya kweli.

Tambua kwamba unayehudumiwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.

Kuna baadhi ya wateja wamekuwa wakitafuta sifa zisizo na maana; marehemu Adolf Balingilaki, ambaye alikuwa mtalaamu wa falsafa za maisha aliwahi kusema; “Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”

Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.

Binafsi ni mwamini wa jambo hili la msingi; Ufanisi unaweza tu kupatikana ikiwa tunaheshimiana. Kila mmoja wetu ana haki ya kufanya kazi katika mazingira yasiyo na unyanyasaji, ubaguzi, ghasia na kisasi.

Kila mtu ana haki ya kufanya kazi katika mazingira yasiyo na unyanyasaji. Unyanyasaji ni tabia isiyofaa ambayo huathiri utendaji wa mfanyakazi au kufanya mazingira ya kazi yasiwe mazuri.

Unyanyasaji unajumuisha kumwendea mtu kwa namna yoyote asiyotaka kupitia maneno, kumwangalia, kumgusa au udhalilishaji (uwe wa ngono au la) unachukiza au kufanya mazingira ya kazi yasiwe mazuri. Unyanyasaji hauruhusiwi kabisa, wateja acheni tabia zisizofaa kwa wanaowahudumia.

Usisahau kwamba wahudumu hao huchangia muda, vipaji na rasilimali za kifedha kukusaidia katika kuleta tofauti kwenye jamii unakoishi na kufanya kazi; hivyo waheshimu ili kuifanya dunia mahali salama.

0 Comments:

Post a Comment