Sunday, December 27, 2020

Simanzi yatawala maziko baba aliyeuawa na mwanaye Hai

 

Waombolezaji wakiwa katika simanzi wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Welanzari Kimaro, tukio lililofanyika nyumbani kwa marehemu kitongoji cha Kiduruni, Masama Mura wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Desemba 23, 2020.

Simanzi ilitawala katika kijiji cha Muroma kilichopo kata ya Masama wilayani Hai wakati wa maziko ya mkazi wa kitongoji cha Kiduruni Welanzari Kimaro (60) aliyeuawa kwa kukatwakatwa na panga na mtoto wake asubuhi ya Desemba 18, 2020 huku wito ukitolewa kwa jamii kuwatunza vijana katika maadili mema ili kuepukana na vitendo visivyo vya kiungwana kwenye familia zao.

Ibada ya maziko ilifanyika nyumbani kwa marehemu Desemba 23, 2020 majira ya saa 9:40 alasiri ikishuhudiwa waombolezaji takribani ya 400 na mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika shamba la ukoo wake pembeni ya nyumba yake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waombolezaji katika msiba huo walisema kutokea kwa tukio hilo kumewapa funzo kubwa katika suala la malezi ya vijana wao na jamii kwa ujumla.

“Inasikitisha na inatuhuzunisha, hatukutegemea hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kila jambo, kwa kweli inauma, kuna kitu tumejifunza,” alisema muombolezaji aliyejitambulisha kwa jina la Hilda.

“Msiba huu umeshtua wengi, umesikitisha wengi, haukuwa umepangika, lakini maandiko matakatifu yanasema kuweni tayari muda unaofaa na usiofaa,” alikaririwa Kandata Kimaro ambaye ni Diwani wa Kata ya Masama Kati.

Kandata aliongeza, “matendo ya vijana wetu sio ya kufumbia macho, tunapaswa kulaumiana sisi wazazi hatujasimama kwenye nafasi zetu, vijana wetu wanatumia dawa za kulevya, familia zimekuwa chanzo ukiona mtoto wako ni mlevi, mvuta bangi toa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji ili hatua za kisheria zichukuliwe.”

Hata hivyo Kandata alijitolea kumpata mahitaji ya shule mtoto mmoja wa marehemu ambaye mwaka ujao atakuwa darasa la saba ukiwa ni utaratibu wake wa kuwasaidia watoto watano kila mwaka kwenye kata yake katika masuala ya elimu. 


 

Kwa upande wake Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) John Njau aliwataka waombolezaji kutambua kuwa hakuna kifo kizuri au kifo kibaya bali kifo ni kifo tu.

“Hakuna kifo kizuri au kifo kibaya; Kifo ni kifo tu, kifo ni adui kinakutenga na wale uwapendao, baba yeye amekwenda hatuwezi kuongeza zaidi, ” alisema katika ibada ya maziko.

Mchungaji Mstaafu Njau ambaye alishirikiana na Mwinjilisti Onesmo Makere wa Usharika wa Muroma kuongoza ibada hiyo alisema, “Naomba sana, watu wasiongeze chuki katika hili, funga mdomo wako katika hili, alaaniwa huyu Shetani, kijana huko aliko akutane na Yesu, arudi amwombe msamaha mama yake na ninaamini mama yake atamsamehe.”

Mke wa marehemu Bi. Joyce Kimaro (aliyeketi kwenye wheelchair) alishiriki kuuaga mwili wa mumewe katika tukio lililofunikwa na simanzi.

Katika suala la kuwatunza vijana, Mchungaji Mstaafu Njau alikemea vitendo vya vijana kutumia dawa za kulevya  ikiwamo bangi huku jamii ikikaa kimya na kuitegemea serikali badala ya kuchukua hatua  kuanzia ngazi ya familia.

“Watu pelekeni taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa kama kuna kijana katika familia yako anayejihusisha  na dawa za kulevya. Hii ni karne ya laana? Hapana sio karne ya laana kwanini tusimwite Yesu katika maombi ili atusaidie kuwaponya vijana wetu?, alisisitiza Mchungaji Mstaafu Njau.

Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) John Njau aliongoza mahubiri katika ibada ya maziko ya Welanzari Kimaro akisaidiwa na Mwinjilisti Onesmo Makere.
  

Awali mwili wa marehemu uliletwa katika nyumba yake kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho majira ya saa tatu asubuhi baada ya Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kuruhusu kufanyika kwa maziko huku uchunguzi zaidi wa kifo cha mkazi huyo wa Kiduruni ukiendelea.

Hata hivyo ibada ya maziko ilichelewa kuanza kutokana na mke wa marehemu aliyejeruhiwa mguu siku ya tukio kulazwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi ambapo madaktari walimruhusu kuhudhuria maziko baada ya kujiridhisha na hali yake kiafya.

Marehemu ameacha mjane na watoto watano (wa kike wawili na wa kiume watatu) na wajukuu wanne huku mtoto aliyefanya tukio hilo ni wa nne kati ya watano ambaye ametoweka kusikojulikana.

Alizaliwa Kirari wilayani Hai mnamo  Julai 1, 1960; alipata ubatizo Oktoba 6, 1960 katika usharika wa KKKT Lemulangaya, Muroma, alipata kipaimara mnamo mwaka 1973 alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mbosho kutoka mwaka 1968-1974 na mnamo mwaka 1975-1976 alisomea masomo ya ufundi katika Chuo cha Ufundi Muroma.

Welanzari aliachana na ukapera mnamo Mei 5, 1987 na kumwoa Joyce Swai ambaye ni mjane kwa sasa ambapo waliendelea kujikita katika shughuli za ujenzi, ufugaji na kilimo hadi mauti yalipomkuta wakati akiwa kwenye mipango ya kuandaa hafla ya kipaimara kwa ajili ya mjukuu wake iliyotarajiwa kufanyika Desemba 20, 2020.

 

0 Comments:

Post a Comment