Dawa ya usingizi aina ya Chloroform |
Mhandisi wa visima anayefahamika kwa jina la Michael Mwingira (47), amejikuta katika wakati mgumu usiku wa kuamkia Desemba 24, 2020 baada ya kuibiwa kila kitu kwa kutiliwa dawa za usingizi wakati akijiandaa kusherekea Krismasi.
Hayo yalijiri ikiwa ni saa chache kabla ya mkesha wa Krismasi wakati mhandisi huyo alipowasili mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro akitokea Tanga kwa ajili ya sherehe hizo za kila mwaka na kubainika kutiliwa dawa za usingizi baada ya kuwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi majira ya saa 8:30 mchana akiwa na uchovu mkubwa uliosababishwa na kemikali hizo.
Ripoti ya vipimo vya madaktari wa kitengo cha dharura wa Hospitali hiyo ya Rufaa ilisema mhandisi huyo alitiliwa dawa za usingizi ikiwamo valium katika mojawapo ya vinywaji alivyokuwa akivitumia kabla ya tukio.
Aidha mhandisi huyo aliwekea dripu la maji kwa ajili ya kuongeza mzunguko wa damu ili kuondoa kemikali hizo za usingizi ambazo hapo awali ilidhaniwa kuwa huenda alitiliwa simu, tetesi ambazo kitengo hicho kiliziweka kando kutokana na ukweli kwamba ingekuwa sumu dalili zaidi zingejitokea kabla ikiwamo kuumwa tumbo.
“Tunamwekea dripu la maji ili kuondoa huo uchovu unaomfanya asijitambue, ingekuwa ni sumu za kupulizia na nyingine dalili zingeonekana lakini kwa hali aliyonayo alizowekewa ni za usingizi,” alisema daktari wa zamu ambaye hakutaka jina lake litajwe wakati muathirika wa tukio hilo akilazwa katika kitanda cha wagonjwa mahututi.
Awali mhandisi huyo aliwasili mjini Moshi na kuchukua chumba katika Nyumba ya Kulala Wageni ya People’s iliyopo Majengo mjini humo ambapo baada ya kupata chakula cha usiku alikwenda zake katika eneo la starehe linalofahamika kwa jina la Moshi Pazuri.
Akizungumza baada ya kupata fahamu na uchovu kupungua mhandisi huyo alisema wakati akipata kinywaji katika eneo hilo walikuja wanawake wawili ambao waliomba kampani yake katika kuendelea kunywa pombe.
Majira ya usiku aliamua kurudi zake alikochukua chumba na wakati akijiandaa kuondoa wanawake hao wawili waliomba lifti katika gari lake na walipofika huko People’s Guest House waliendelea kunywa pombe ambako wanawake hao inadaiwa walitumia mwanya huo kumwekea dawa za usingizi pasipo kujua.
Baada ya kuamka asubuhi ya Desemba 24, 2020 mhandisi huyo huku akiwa ahajitambua alijikuta hana kitu chochote zaidi ya nguo alizovaa, ndipo alipowataka wahudumu wa gesti ile kumsaidia simu ili afanye mawasiliano na ndugu, jamaa na marafiki kwa ajili ya msaada zaidi.
Mwingira aliongeza kuwa rafiki yake aliyepo mjini Moshi ndiye aliyetoa msaada mkubwa wa kumfikisha mikononi mwa Maafisa wa Jeshi la Polisi ambapo walikuja katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kuwachukua wahudumu waliokuwepo zamu kwa ajili ya maelezo zaidi.
Pia mhandisi huyo katika mahojiano na maafisa wa polisi mkoani humo alimwelezea mwanamke mmoja kati ya wale wawili jinsi alivyo ili kurahisisha uchunguzi zaidi kufanyika na kuwakamata wahalifu wanaotumia mbinu hizo kinyume cha sheria na kuvitaja vitu vilivyoibiwa zikiwamo simu, kadi za benki, vitambulisho na begi la nguo.
Shuhuda mmoja aliliambia gazeti hili kuwa mwanamke aliyefanya unyama huo ni mzoefu wa siku nyingi ambaye hufanya shughuli za ukahaba mjini Moshi kwa miaka mingi alikuwa akionekana katika maeneo ya starehe ya Malindi mjini humo.
Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku likitoa raia katika kipindi hiki cha sikukuu watu mbalimbali kuchukua tahadhari kukaa na watu wasiowafahamu ili kuepusha madhara zaidi.
0 Comments:
Post a Comment